Mtaalam wa kuendesha mashine ya kusaidia moyo na
mapafu kufanya kazi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sophia Lukonge
akiendesha mashine hiyo wakati wa kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto
inayofanywa na wataalam wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka kituo cha
King Salman Humanitarian and Relief cha nchini Saudi Arabia.
Wataalam
wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na
wenzao wa kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief cha nchini Saudi
Arabia wakimfanyia upasuaji wa moyo mtoto mwenye tundu lililopo kwenye moyo wakati
wa kambi maalum ya matibabu inayoendelea katika Taasisi hiyo. Jumla ya watoto
30 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo.
Picha
na JKCI
*********************************************************************** ****************************
Watoto 16
wenye magonjwa ya moyo wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu
inayoendeshwa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na wenzao kutoka Kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief
Centre ya nchini Saudi Arabia.
Kambi hiyo
maalumu imekusudia kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto 30 wenye matatizo ya
matundu kwenye moyo, mishipa ya damu iliyopishana, pamoja na mishipa ya
kupeleka damu kwenye mapafu kuziba kwa siku sita.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hii, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa moyo kwa watoto wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Felix Shonyela alisema ushirikiano kati
ya JKCI na Taasisi ya King Salman kwa kipindi cha miaka 10 umekuwa na mchango
mkubwa katika kuongeza idadi ya watoto wenye magonjwa ya moyo walilofanyiwa
upasuaji wa moyo nchini.
Dkt. Shonyela
alisema wazazi na walezi wanapaswa kuwafikisha watoto hospitali mapema pale
wanapowagundua kuwa na changamoto za kiafya ili kurahisisha matibabu yao na
kupata huduma mapema.
Kwa upande
wake daktari bingwa mshauri wa magonjwa ya moyo kutoka Kituo King Salman
Humanitarian Aid and Relief Centre ya nchini Saudi Arabia , Dkt. Aljohara
Hamza, amesema timu hiyo ilianza kutoa huduma mara baada ya kuwasili JKCI na
katika siku mbili za Jumamosi na Jumapili imefanikiwa kuwafanyia upasuaji
watoto 11.
Dkt. Aljohara
alisema kituo hicho kitaendelea kufanya kazi kwa weledi na kushirikiana na
madaktari wa JKCI kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa na watoto wengi
wanapata huduma kupitia kambi hiyo.
“Tumefurahishwa
na uwezo wa wataalamu wa JKCI katika kutoa huduma bingwa za upasuaji wa moyo
kwa watoto, uwezo wao ni tofauti na tulivyoanza kushirikiana miaka 10
iliyopita”, alisema Dkt. Aljohara
-
Comments
Post a Comment