JKCI yajivunia mafanikio ya miaka 11 yaweka mikakati ya kupanua huduma ndani na nje ya nchi
Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Hassan Mahmoud Mshinda, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge, wajumbe wa bodi ya wadhamini na menenjimenti ya taasisi hiyo wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mafunzo ya siku moja kwa viongozi hao yaliyofanyika leo katika hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Hassan Mahmoud Mshinda akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wajumbe wa bodi ya wadhamini na menejimenti ya taasisi hiyo yaliyofanyika leo katika hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya siku moja kwa wajumbe wa bodi ya wadhamini na menejimenti ya taasisi hiyo yaliyofanyika leo katika hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam.
Na JKCI
******************************************************************************************************
Ubunifu katika kutoa
huduma za matibabu ya moyo, usimamizi madhubuti na utendaji kazi uliotukuka
vimetajwa kuwa miongoni mwa nguzo zinazoiwezesha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kupata mafanikio na kutambulika ndani na nje ya nchi katika kipindi cha
miaka 11 tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza kuhusu
mafanikio ya Taasisi hiyo wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wajumbe wa bodi ya
wadhamini na menejimenti ya JKCI Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema utambuzi ambao JKCI imekuwa ikiupata
kupitia tuzo mbalimbali inazopokea unatokana na juhudi za pamoja za Bodi ya Wadhamini
na Menejimenti ya Taasisi hiyo katika kuhakikisha taasisi inaendelea kutoa
huduma bora za matibabu ya moyo.
Dkt. Kisenge alisema
mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa kuwekeza katika ubunifu, kuimarisha mifumo
ya usimamizi na kuhakikisha wataalamu wanatekeleza majukumu yao kwa weledi ili
kuongeza uwezo wa Taasisi kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.
“Tumekuwa tukipata tuzo
zinazotambua kazi nzuri inayofanywa na JKCI, matokeo hayo yanatokana na
usimamizi mzuri wa Bodi ya Wadhamini pamoja na utendaji kazi mzuri wa
Menejimenti ya Taasisi”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema
kipindi cha miaka 11 tangu kuanzishwa kwa JKCI Taasisi hiyo imefanikiwa kufanya
upasuaji wa moyo wa kufungua kifua kwa wagonjwa zaidi ya 8,000 hatua
inayoonesha uzoefu na uwezo wake katika kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya
moyo.
“Mafanikio ya JKCI ni
sehemu ya safari ya Taasisi katika kupanua wigo wa huduma na kuongeza mchango
wake katika matibabu ya moyo nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na
Kati”, alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Mtendaji
Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole
Gabriel alisema wajumbe wa Bodi hiyo wana jukumu kubwa la kuhakikisha Taasisi
inaendelea kukua na kutekeleza wajibu wake wa kutoa huduma za kibingwa bobezi
za matibabu ya moyo kwa wananchi.
Prof. Elisante ambaye
alitoa mafunzo ya uwajibikaji kwa viongozi hao alisema JKCI ni taasisi yenye
umuhimu mkubwa katika mfumo wa huduma za afya nchini hivyo Bodi hiyo inapaswa
kusimamia kwa umakini maendeleo yake, kuhakikisha rasilimali zinapatikana na
kuweka mikakati itakayoiwezesha Taasisi kuendelea kutoa huduma na kuokoa maisha
ya wagonjwa.
“JKCI ni taasisi ambayo
ni tegemeo hapa nchini katika kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo
hivyo wajumbe wa bodi wa Taasisi hii mnapaswa kujua kuwa mmebebeshwa jukumu
kubwa ambalo mnatakiwa kulisimamia ili kuhakikisha Taasisi hii inaendelea
kukua”, alisema Prof. Elisante.
Prof. Elisante alisema
Bodi ya wadhamini ya JKCI inapaswa kusimamia upatikanaji wa bajeti ya kutosha
na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha JKCI inakuwa na vyanzo endelevu vya
mapato na rasilimali za kutosha ili kukidhi mahitaji ya utoaji wa huduma,
kuimarisha maendeleo ya Taasisi na kuhakikisha wagonjwa wanaendelea kupata
matibabu wanayohitaji.
Ushirikiano kati ya
Bodi ya Wadhamini na Menejimenti ni msingi muhimu wa kuhakikisha JKCI
inaendelea kuwa na uwezo wa kutoa huduma bora, kuendeleza ubunifu na kutekeleza
maono yake ya kupanua huduma za matibabu ya moyo ndani na nje ya nchi.




Comments
Post a Comment