319 wachunguzwa moyo Dodoma Festival
****************************************************************
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Wananchi 319
wafanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika tamasha la Karibu Dodoma
Festival
Wananchi 319 walitembelea
katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo
kwenye tamasha la karibu Dodoma Festival lililofanyika katika viwanja vya
Chinangali Park kuanzia tarehe 25-29/10/2021.
Watu wote waliotembelea
katika banda la Taasisi hiyo walifanyiwa vipimo vya urefu na uzito, kiwango cha
sukari mwilini, uwiano kati ya urefu na uzito, shinikizo la damu (BP) na
walipata elimu ya magonjwa ya moyo ikiwemo lishe bora kwa afya ya moyo.
Waliofanyiwa vipimo vya
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography- ECHO) na mfumo wa
umeme wa moyo (Electrocardiography - ECG) walikuwa 230. Kati ya hawa 230
waliofanyiwa vipimo hivi 159 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo na hivyo
kupewa dawa za kwenda kutumia. Dawa hizi zilitolewa bila malipo yoyote yale na kampuni ya uagizaji na usambazaji wa dawa za binadamu
ya Sun Pharmaceutical Industries Ltd.
Wagonjwa 26 walikutwa na
matatizo mbalimbali ya moyo na hivyo kupewa rufaa za kwenda kufanyiwa uchunguzi
wa kina zaidi pamoja na kutibiwa katika hospital ya mkoa ya Dodoma, hospitali
ya kanda ya Benjamini Mkapa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
Matatizo waliyokutwa nayo wagonjwa
waliopewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ni
kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo hawa walikuwa 5, umeme wa moyo kupita katika
njia ya ziada tofauti na ile ya kawaida (Wolff – Parkinson - White syndrome)
alikuwa mmoja, mshipa mkubwa wa damu wa moyo umetanuka na valvu ya Aorta
inarudisha damu nyuma alikuwa mmoja, mapigo ya moyo yanakwenda haraka kuliko
kawaida zaidi ya mapigo 100 kwa dakika
moja na inafika wakati anazimia alikuwa mmoja.
Mgonjwa mmoja moyo wake ulikuwa umetanuka na ni
mjamzito kitu ambacho kinahatarisha maisha ya mama na mtoto aliyepo tumboni na
mgonjwa mmoja alikuwa na shida ya valvu ya moyo (Rheumatic Heart disease)
ugonjwa huu unasababishwa na bakteria wanaoshambulia valvu za moyo.
Asilimia kubwa ya wagonjwa
tuliowagundua katika upimaji huu wakiwemo wagonjwa wote 26 tuiowapa rufaa
hawakuwa wanafahamu kuwa na matatizo ya
moyo.
Taasisi inaendelea kutoa
wito kwa wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara pia kujitokeza
kwa wingi kupima magonjwa ya moyo wakati tunapotoa huduma mbalimbali za upimaji
kwa wananchi. Kwani upimaji huwa unafanyika bila malipo yeyote yale na kama
kutakuwa na malipo ni kwa ajili ya vipimo ambapo mwananchi anachangia kiasi
kidogo cha fedha na kuna ambao hawachangii kabisa.
Imetolewa na:
Anna Nkinda
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
31/10/2021
Comments
Post a Comment