Profesa Janabi: Wahudumu wa afya wawe wa kwanza kuchanja chanjo ya UVIKO – 19
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati
akitoa elimu ya chanjo kwa watumishi wa afya wa hospitali ya taifa ya magonjwa
ya akili Mirembe na wanafunzi wa chuo cha uuguzi Dodoma kilichopo chini ya hospitali hiyo.
Prof.
Janabi ambaye pia ni mhamasishaji wa kitaifa wa mpango wa jamii shirikishi na
harakishi wa elimu na uhamasishaji wa
chanjo dhidi ya UVIKO – 19 alisema mwitikio wa wataalam wa afya kutoka
Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya akili Mirembe umekuwa mkubwa na elimu waliyoipata itawasaidia kuwa
mabalozi wazuri katika jamii zinazowazunguka na kuwafanya wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu chanjo
ya UVIKO –
19 .
“Wataalam wa afya ukiacha kwamba tupo
hospitali kwa muda mwingi pia tupo katika nafasi kubwa ya kupata ugonjwa wa UVIKO –
19 hii
ni kutokana na mazingira tuliyonayo hivyo kuziweka familia zetu katika hatari
ya kupata ugonjwa huu, ni vyema tukapata taarifa sahihi na kuwa mstari wa mbele
kuchanja na kulinda afya zetu”, alisema Prof. Janabi
“Leo
hii nimetoa elimu kwa wahudumu wa afya kwasababu tuna imani kubwa wafanyakazi
wa afya wakiwa na uelewa wa kutosha na
kujitokeza kuchanja itatoa motisha pia kwa jamii kujitokeza kwa wingi lakini
pia watakuwa wahamasishaji wakubwa kutoa elimu hiyo ya kisayansi kwa wananchi
wanaowazunguka”, alisema Prof. Janabi.
Kwa
upande wake kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya akili Mirembe
Dkt. Japhet Swai alisema wafanyakazi wa Mirembe wamekuwa na shauku ya kupata
elimu kama waliyoipata kupitia Prof. Janabi ambayo kwa hakika itafuta rekodi ya
wataalam kutoka Hospitali ya Mirembe ya kuwa nyuma katika suala ya kuchanja
chanjo ya UVIKO – 19.
“Kati
ya watumishi 190 tulionao watumishi waliochanja hadi sasa ni 28 tu kutokana na
maswali mengi ambayo yalikuwa hayajapatiwa ufumbuzi lakini sasa ujio wa Prof.
Janabi umekuwa ni bahati kwa watumishi wa Mirembe kupatiwa ufumbuzi wa maswali
waliyokuwa nayo, naamini sasa watajitokeza kuchanja na kuelimisha jamii
inayowazunguka”, alisema Dkt. Swai
Naye
daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya akili
Mirembe na Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Tafiti Innocent Mwombeki alisema amepata
elimu mpya kuhusu chanjo ya UVIKO – 19
ambayo sasa anaweza kuitoa na kuipeleka
kwa wafanyakazi wenzake ili kuhakikisha kuwa wafanyakazi wote wamejikinga na
ugonjwa huo pamoja na kujitokeza kuchanja.
“Maswali
mengi ambayo watu wamekuwa nayo katika jamii kuhusu chanjo ya UVIKO –
19 leo
tumepata majibu yake kupitia elimu iliyotolewa na Prof. Janabi hivyo naamini
elimu hii itasaidia sana kupunguza hofu waliyokuwa nayo wafanyakazi wa afya na
kuwapa motisha ya kujitokeza kuchanja”, alisema Dkt. Mwombeki.
Naye
mwanafunzi wa udaktari bingwa wa magojwa ya akili wa mwaka wa pili katika Hospitali ya Mirembe
Suluma Aslan alisema chanjo ya UVIKO – 19 ilivyoingia
nchini aliogopa kuchanja kutokana na hali yake ya ujauzito aliyokuwa nayo kwamba ungemletea shida yeye pamoja na
mtoto wake lakini baada ya elimu sahihi ya chanjo amekuwa ni miongoni mwa watu
waliochanja siku ya leo.
Takwimu zinaoesha kuwa hadi sasa chanjo karibu bilioni 6.9 zimeshatolewa na nusu ya dunia imeshachanja wakati Bara la Afrika asilimia 3 ya watu ndio waliopata chanjo.
Comments
Post a Comment