Pinda: Huduma za afya kibingwa zipelekwe kila Kanda
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia , Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima akizungumza kuhusu umuhimu wa
kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi alipotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kwa ajili ya kuona huduma za upimaji na matibabu ya moyo zilizokuwa zinazotolewa
na wataalamu wa taasisi hiyo katika tamasha la Karibu Dodoma festival lililofanyika
katika viwanja vya Chinangali park. Kushoto ni Mkurugenzi wa JKCI Prof. Mohamed
Janabi.
Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Geophrey Pinda ameiomba wizara ya Afya kusogeza huduma za matibabu
ya kibingwa ya kuwafuata wananchi mahali
walipo katika ngazi ya mikoa na kanda kwa kufanya hivyo wananchi wengi
watafikiwa na huduma hizo.
Pinda ambaye pia ni Mbunge wa jimbo
la Kavuu alitoa ombi hilo kwa waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Dkt. Doroth Gwajima katika tamasha la Karibu Dodoma festival lililofanyika
katika viwaja vya Chinangali park ambalo lilikwenda sambamba na zoezi la
ushauri, upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali.
Naibu Waziri huyo ambaye alifika katika banda la Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu
ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa taasisi hiyo alifurahia huduma zilizokuwa
zinatolewa kwa wananchi.
“Ninawapongeza wataalamu wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi
walioko hapa, sijawahi kuona huduma kama hii ikitolewa ninaomba huduma hizi ziende
kwa wananchi hadi ngazi ya mikoa na kanda ili watu wengi zaidi wafikiwe na huduma
hizi”,.
“Huko vijijini kuna watu
wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali yanayohitaji matibabu ya kibingwa lakini
wanashindwa mahali pa kupata huduma hizi, kama watu hawa watafikiwa itawasaidia
sana kufanya vipimo na kupata matibabu kwa wakati”, alisema Pinda.
Kwa upande wake Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima alisema
amepokea ombi hilo, atakaa na watalamu wake ili waone ni jinsi gani huduma hizo zinaweza kutolewa kwa
wananchi kila baada ya miezi mitatu
katika kanda mbalimbali.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan
amenunua magari yenye x-ray na maabara za
kisasa pia wataalamu wako wa kutosha hivyo basi ni rahisi huduma hizi kuwafikia
wananchi mahali popote pale walipo”,.
“Ili wataalamu waweze kufika huko
wanahitaji kuwezeshwa hivyo basi ni muhimu wapenda maendeleo wakaanzisha kapu
la pamoja ambalo litatusaidia kwenda kutoa huduma katika Kanda kwani faida ni kubwa ikiwa ni pamoja na wananchi
kugundua matatizo mapema na kupunguza msongamano katika Hospitali za Taifa”,
alisema Dkt. Gwajima.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof.
Mohamed Janabi alisema Taasisi hiyo imekuwa ikitoa huduma za kuwafuata
wananchi mara kwa mara na imewasaidia kuwafikia wananchi wengi zaidi
ambao wamepata huduma za matibabu kwa wakati.
“Kuwepo kwa huduma hii kumetufanya
tufahamu kuwa wananchi wengi wanamatatizo ya moyo hasa shinikizo la juu la damu
na hawafahamu kuwa na matatizo haya ndiyo maana kila tunapokwenda kutoa huduma
zetu tunaambatana na wenzetu wa kampuni za dawa ambao wanatusaidia kutoa dawa bila
malipo kwa wale wote wanaokutwa na shida”, alisema Prof. Janabi.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kavuu Geophrey Pinda akizungumza na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Naiz Majani wakati alipotembelea banda la taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma za upimaji na matibabu ya moyo zilizokuwa zinazotolewa na wataalamu wa taasisi hiyo katika tamasha la Karibu Dodoma festival lililofanyika katika viwanja vya Chinangali park. Katikati ni Mbunge wa viti maalum (CCM) Dkt. Alice Kaijage.
Mkuu wa wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri akimuuliza swali daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli Rweyemamu wakati alipotembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma za upimaji na matibabu ya moyo zilizokuwa zinazotolewa kwenye tamasha la Karibu Dodoma festival lililofanyika katika viwanja vya Chinangali park. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi hiyo Anna Nkinda.
Mfanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aliston Jovin akimpatia vipeperushi vinavyoonesha huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo mwananchi aliyefika katika banda la JKCI kwa ajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zilizokuwa zinazotolewa kwenye tamasha la Karibu Dodoma festival lililofanyika katika viwanja vya Chinangali park jijini Dodoma.
Comments
Post a Comment