Watu wengi waliojitokeza kupima magonjwa ya moyo wilayani Kigamboni wamebainika kuwa na shinikizo la juu la damu. Kati ya watu 173 waliopimwa 58 wamethibitika kuwa na tatizo hilo
Jumla ya watu 173 wamefanyiwa upimaji wa magonjwa ya moyo
wakati wa maadhimisho ya siku ya moyo Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya
Hospitali ya wilaya ya Kigamboni iliyopo Gezaulole.
Upimaji huo uliofanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya wilaya ya Kigamboni.
Watu wote 173 walifanyiwa vipimo vya kuangalia uwiano wa
urefu na uzito, wingi wa sukari kwenye damu na shinikizo la damu, waliokutwa na
viashiria vya magonjwa ya moyo walifanyiwa vipimo zaidi ambapo 124 walifanyiwa vipimo vya kuangalia jinsi
moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram - ECHO) na mfumo wa umeme wa moyo
(Electrocardiogram – ECG).
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka JKCI Baraka Ndelwa
alisema baada ya kufanyika kwa vipimo vya ECG na
ECHO watu 58 walikutwa na matatizo
mbalimbali ya moyo ikiwemo shinikizo la
juu la damu ambalo halijadhibitiwa na 12 kati yao walipewa Rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Watu 115 hawakukutwa na matatizo yoyote yale ya moyo hivyo
basi tuliwapa ushauri wa jinsi ya kutunza mioyo yao ili wasipate magonjwa ya
moyo ambayo ni magonjwa yasiyo ya kuambukiza na mtu akifuata ushauri wa
wataalamu na mtindo bora wa maisha ataweza kuyaepuka”,.
“Wagonjwa tuliowapa rufaa ni wale waliokutwa na matatizo ya kutanuka kwa moyo, dalili ya kansa ya koo, tatizo la mfumo wa chakula, matatizo ya mishipa
ya damu ya moyo na magonjwa ya valvu za moyo”, alisema Dkt.
Ndelwa.
Dkt. Ndelwa alisema kuna baadhi ya wagonjwa ambao waliwaona
walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu zaidi ya 198 ambalo
halijadhibitiwa inawezekana ni kutokana
na mtu kutokufahamu kama anatatizo hilo au alitumia dawa za moyo na kuacha
kuzitumia.
Akizungumza na wananchi waliofika katika upimaji huyo Mkuu wa
wilaya ya Kigamboni Mhe. Fatma Nyangasa aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa kutoa wataalamu wake na kwenda kufanya upimaji kwa wakazi wa
wilaya hiyo.
Mhe. Fatma aliwahimiza wananchi hao kufuata maelekezo ya
wataalamu na kuyafanyia kazi kwani hakuna elimu nyingine ya magonjwa ya moyo
watakayoipata tofauti na watakayopewa na wataalamu wa afya.
“Fursa hii ya matibabu mliyopata ni adimu kupatikana kwani
wataalamu wamewafuata huku mnakoishi, ninawasihi wakati mwingine zitakapotokea fursa
kama hizi mjitokeze kwa wingi ili mpate huduma za matibabu”, alisema Mhe.
Fatma.
Aidha Mhe. Fatma alimuagiza Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya
wilaya ya Kigamboni kuhakikisha dawa za
magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo za ugonjwa wa moyo zinapatikana katika Hospitali
hiyo ili wagonjwa wanaotibiwa hapo wapate dawa hizo kabla hawajaenda kutibiwa katika
Hospitali za Taifa.
Kuhusu ugonjwa wa UVIKO -19 alisema ni tatizo la Dunia nzima na kuwahimiza
wananchi kuchanja ingawa suala la kuchanja ni la hiari kwani wataalamu wamethibitisha
chanjo hiyo ni salama na watumie fursa ya kusogezewa chanjo katika maeneo yao kuchanja
kwa kufanya hivyo watakuwa salalama.
Kwa upande wao wananchi waliopata huduma ya kufanyiwa
uchunguzi wa magonjwa ya moyo bila malipo waliishukuru Serikali kwa kuwasogezea
huduma hiyo ya kibingwa na kuomba huduma kama hizo ziwe zinatolewa mara kwa
mara.
“Wanangu walisikia wataalamu wanakuja kupima wakanileta,
baada ya kufanyiwa vipimo nimekutwa na tatizo la kutanuka kwa moyo sikuwa
nafahamu kama ninatatizo hilo nimepewa dawa za kutumia kwa muda wa siku 10
pamoja na rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo”, alisema mzee Crosteri Tarubera.
Katika upimaji huo kampuni za uagizaji na usambazaji wa dawa
za binadamu na vifaa tiba za Samiro Pharmaceutical Ltd na Ajanta Pharma Ltd
zilitoa dawa bila malipo kwa watu waliokutwa na matatizo ya moyo.
Comments
Post a Comment