JKCI yapokea mashine ya kisasa kuboresha uangalizi wa wagonjwa ICU
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akipokea
kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya kusambaza vifaa tiba ya Computech
Healthcare Tanzania Sandip Datta msaada wa monitor ambayo inapokea taarifa za hali
za wagonjwa zaidi ya 16 kwa wakati mmoja (Monitoring Central Station). Monitor
hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 68 itasaidia kukusanya taarifa za hali
za wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu
(ICU).
Mkurugenzi
wa kampuni ya kusambaza vifaa tiba ya Computech Healthcare Tanzania Sandip
Datta akimuonesha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge namna Monitor ya kupokea taarifa za hali za wagonjwa zaidi ya
16 (Monitoring Central Station) inavyofanya kazi wakati kampuni hiyo ilipotoa
msaada wa monita hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Picha na
JKCI
********************************************************************************************************
Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepokea msaada wa monitor ya kisasa yenye uwezo wa
kufuatilia taarifa za wagonjwa zaidi ya kumi na sita kwa wakati mmoja (Central
Monitoring Station) waliolazwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi
maalum (ICU).
Msaada huo
wa monitor moja yenye thamani ya shilingi milioni 68 umetolewa leo jijini Dar
es Salaam na kampuni ya kusambaza vifaa tiba ya Computech Healthcare Tanzania.
Akizungumza
mara baada ya kupokea msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliishukuru kampuni hiyo kwa msaada walioutoa
na kusema monitor hiyo itasaidia kuboresha huduma za uangalizi kwa wagonjwa
waliolazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).
Dkt. Kisenge
ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa
ya damu ya moyo alisema mashine hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza
ufanisi wa utoaji huduma kwa kuwa inafuatilia hali za wagonjwa wengi kwa wakati
mmoja kwa njia za kidijitali.
“Kupitia Central Monitoring Station hii
wauguzi wataweza kufuatilia mapigo ya moyo, shinikizo la damu na umeme wa moyo
wa wagonjwa kwa wakati mmoja. Teknolojia hii itarahisisha ufanyaji wa kazi,
kupunguza changamoto za ufuatiliaji wa mgonjwa mmoja mmoja na kuongeza usahihi
katika utambuzi wa matatizo ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge
aliongeza kuwa taasisi hiyo inaendelea na mpango wa kuhakikisha huduma zote za
kitabibu zinakuwa za kidijitali ili kuboresha ufanisi na kupunguza matumizi ya
nguvu kazi ya kibinadamu.
“Hivi sasa
tunalenga wagonjwa wote wawe wanafuatiliwa kidijitali. Vifaa hivi vina akili
bandia (AI) inayoweza kugundua mapema mabadiliko ya kiafya kwa mgonjwa na
kusaidia kutoa huduma za haraka na zenye ubora zaidi”, alifafanua.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa kampuni ya kusambaza vifaa tiba ya Computech Healthcare
Tanzania Sandip Datta alisema msaada huo ni sehemu ya ushirikiano endelevu kati
ya kampuni yake na JKCI katika kuboresa ubora wa huduma za afya nchini.
“Tumeamua
kuleta teknolojia hii ya Central Monitoring Station ili kusaidia wauguzi na
madaktari kufuatilia wagonjwa kwa urahisi zaidi. Hii ni hatua muhimu katika
safari ya kidigitali ya sekta ya afya Tanzania”, alisema Datta.
Naye
Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert
Mallya alisema monitor hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wauguzi katika
kuhakikisha wagonjwa wote wanapata uangalizi wa karibu kupitia mfumo mmoja.
“Kwa sasa
muuguzi mmoja anaweza kukaa kwenye kituo kimoja na kufuatilia wagonjwa zaidi ya
mmoja kwa wakati mmoja. Kifaa hiki kitaunganisha monitors zote za wagonjwa na
kuonyesha taarifa zao sehemu moja, jambo litakaloongeza kasi na ubora wa utoaji
wa huduma kwa wagonjwa walioko ICU”, alisema Mallya.




Comments
Post a Comment