Mwelekeo mpya wa huduma za moyo: JKCI yaunganisha timu yake kuunda mpango mkakati wa 2026/2031
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mpango mkakati wa watu
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya
Tiba Shirikishi Dkt. Naizihijwa Majani akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi
wakati wa kikao cha kuwashirikisha wafanyakazi kuhusu mpango huo kilichofanyika
leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Fedha na Katibu wa maandalizi ya mpango mkakati
wa tatu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA. Agnes Kuhenga akizungumza
na wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakati wa kikao cha kuwashirikisha wafanyakazi
kuhusu mpango huo kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI uliopo
jijini Dar es Salaam.
Na JKCI
***************************************************************************************************
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na
Hospitali ya Dar Group wameshirikishwa kikamilifu katika maandalizi ya Mpango
Mkakati wa Tatu wa Taasisi hiyo hatua inayolenga kuhakikisha mpango huo unazingatia
mahitaji halisi ya watumishi na kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Ushirikishwaji huo umefanyika leo katika kikao cha pamoja cha
wafanyakazi wote ambapo Kamati ya Maandalizi ya Mpango Mkakati wa Tatu
iliwasilisha tathmini ya mpango uliopita na kueleza malengo mapya
yanayotarajiwa kwenye mpango ujao.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya
Maandalizi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Shirikishi Dkt. Naizihijwa
Majani alisema wafanyakazi wameonyesha kufurahishwa na mafanikio ya mpango
mkakati uliotangulia na kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa katika kuboresha
maeneo yanayohitaji kuimarishwa.
“Wafanyakazi wengi wanapenda kuona Mpango Mkakati wa Tatu
ukijikita katika matumizi ya teknolojia, kuifanya JKCI kujitegemea zaidi na
kuwafikia wananchi wengi kwa ufanisi mkubwa", alisema Dkt. Naizihijwa.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Tiba Mionzi wa JKCI Amani Materu
aliishukuru Taasisi hiyo kwa kuwapa nafasi wafanyakazi kushiriki katika hatua
za awali za uundaji wa mpango huo muhimu.
“Mpango huu utakuwa kielelezo cha mawazo ya wafanyakazi wote,
unatupa nafasi kuona mahali tulipotoka, tulipo sasa na tunapokusudia
kwenda".
“Ushirikishwaji huu unarahisisha safari ya kufikia malengo
yetu. Tutaendelea kutoa maoni na mchango wetu ili kuijenga Taasisi yetu",
alisema Materu.
Naye Mfamasia wa JKCI Ndenashe Kimaro alisema wafanyakazi
wamefarijika kuona wamepewa jukwaa la kutoa maoni na kuwa sehemu ya uundaji wa
mwelekeo mpya wa taasisi.
“Tutajitahidi kwa pamoja kuhakikisha taasisi yetu inaendelea
kung’ara na kuwa mfano wa kuigwa Afrika Mashariki na Kati katika utoaji wa
huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo", alisema Ndenashe.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyakazi wa Taasisi hiyo
tawi la Hospitali ya Dar Group waliuomba uongozi kutoa mafunzo zaidi kwa
wafanyakazi wa tawi hilo ili waweze kufahamu zaidi kwani wameingia katika
utumishi wa umma hivi karibuni hivyo bado baadhi ya vitu hawavifahamu.
Daktari wa Hospitali ya JKCI Dar Group Phocus Kibira alisema
mpango mkakati uliopita wafanyakazi hao hawakuwa sehemu ya JKCI hivyo
maandalizi ya mpango huu wanahitaji mafunzo na ushirikishwaji wa kutosha ili
nao waweze kufahamu na kuwa sehemu ya maandalizi ya mpango huo.
Rehema Stephano ambayo ni Mhasibu ya Hospitali ya JKCI Dar
Group alisema kikao cha leo kimewatambulisha uwepo wa mpango mkakati wa Taasisi
lakini mambo hayo kwao bado ni mageni hivyo kuomba kupata mafunzo maalumu
yatawasaidia kupata mwangaza.
Mpango Mkakati wa Tatu wa JKCI unatarajiwa kukamilika mwezi
Machi 2026 na kuanza kutumika rasmi katika mwaka wa fedha 2026/2027.




Comments
Post a Comment