Wahasibu JKCI wagusa mioyo ya wagonjwa

***************************************************************************************************************
Jamii imetakiwa kujenga utamaduni wa kusaidia watu wenye mahitaji mbalimbali wakiwemo wagonjwa, wazee na makundi mengine yenye uhitaji maalumu ili kukuza mshikamano na utu.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa
Fedha na Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA. Agnes Kuhenga wakati
akikabidhi zawadi kwa watoto wenye matatizo ya moyo wanaotibiwa katika taasisi
hiyo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahasibu.
CPA. Agnes alisema wahasibu wa JKCI waliamua kuadhimisha siku
hiyo kwa kufanya jambo la kijamii ili kuwafariji wagonjwa na kuonesha moyo wa
upendo kwa jamii.
“Tumetoa zawadi mbalimbali zikiwemo nepi, sabuni, mafuta,
sukari, biskuti na juisi zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni mbili.
“Tuliona katika kuadhimisha siku hii tujichangishe fedha na
kununua mahitaji ya watoto, ni vyema tukawagusa wagonjwa wanaopokea huduma
katika taasisi yetu, hasa watoto wenye matatizo ya moyo”, alisema CPA. Kuhenga.
Aliongeza kuwa wagonjwa wengi wanaotibiwa JKCI wanatoka
mikoani na baadhi yao kutoka familia zenye kipato cha chini, hivyo msaada huo
ni njia ya kuwafariji na kuwapa matumaini mapya wakati wa matibabu.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliwapongeza
wahasibu wa taasisi hiyo kwa moyo wa upendo na kujitolea, akisema kuwa kitendo
hicho ni cha kuigwa na idara nyingine ndani ya taasisi.
“Ni jambo la kufurahisha kuona wahasibu wetu wakitumia siku
yao ya kimataifa kuwasaidia wagonjwa wanaowahudumia kila siku. Kwa kawaida
tumekuwa tukipokea msaada kutoka makundi ya nje, lakini leo tumepokea msaada
kutoka ndani ya familia ya JKCI. Huu ni mfano mzuri wa uzalendo na utu wa kweli”,
alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo
na Mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo, alisema wahasibu ni nguzo
muhimu katika mafanikio ya taasisi yoyote kwa kuwa usimamizi mzuri wa fedha
unaiwezesha taasisi kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Tangu kuanzishwa kwa taasisi hii mwaka 2015, JKCI imekuwa
ikipata hati safi za ukaguzi kila mwaka kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG). Hii ni ishara ya uadilifu na uwajibikaji wa hali
ya juu walionao wahasibu wetu”, alisema Dkt. Kisenge.
Aliongeza kuwa usimamizi mzuri wa fedha umeiwezesha JKCI
kupanua huduma zake na kuifikia zaidi ya mikoa 22, kupitia kliniki za moyo
zinazowafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu wa JKCI CPA. Reuben Nyiti alisema
maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo “Kukuza Uwajibikaji na Utendaji
Bora Kupitia Teknolojia na Uchangiaji kwa Jamii” ambayo inalenga kuwahamasisha
watumishi kufanya kazi kwa bidii huku wakikumbuka kuwajali wanaowahudumia.
“Tunatambua wagonjwa wetu wanatoka sehemu mbalimbali za nchi,
hivyo ni wajibu wetu kuonesha upendo, huruma na mshikamano.Tumeamua kutumia
siku yetu kama wahasibu kuwa karibu na wagonjwa badala ya kusherehekea tukiwa
ofisini”, alisema CPA. Nyiti.
Nao wazazi wa watoto waliopokea zawadi hizo hawakuficha
furaha yao, wakieleza kuwa msaada huo umeleta faraja kubwa kwao na kuwapa
matumaini mapya wakati watoto wao wakiendelea na matibabu.
“Tumejawa na furaha kubwa, leo hii tumeguswa kwa upendo.Tunawashukuru
wahasibu wa JKCI kwa moyo wao wa utu na kujali”, alisema Sophia Albano mkazi wa
Mtwara ambaye mtoto wake anatibiwa katika taasisi hiyo.
Sophia alisema zawadi walizopewa si tu msaada wa mahitaji ya
kila siku, bali pia ni ishara ya upendo unaoonesha kuwa jamii bado inajali
wagonjwa na familia zao.
“Zawadi hizi zimeleta tabasamu, hasa kwa watoto wanaopitia matibabu
magumu. Ni jambo dogo kwa wengine, lakini kwetu lina maana kubwa sana”.
“Tumefarijika sana kwa zawadi hizi. Hii ni ishara ya kuwa
familia yetu haiko peke yake katika changamoto hizi. Tunapenda kuwashukuru
wahasibu wote wa JKCI kwa moyo wao wa huruma na kujali”, alisema Lilian Mwita mkazi wa Dar es Salaam ambaye mtoto wake anatibiwa katika taasisi hiyo.


Comments
Post a Comment