Jamii yatakiwa kuchunguza afya mara kwa mara ili kuzuia magonjwa yasiyoambukiza
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Edward Martin akiwafundisha wafanyakazi
wa TATA Africa Holdings Limited umuhimu wa kupata vipimo na matibabu ya
magonjwa ya moyo mapema wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyofanyika katika ofisi za kampuni
hiyo zilizopo vingunguti Dar es Salaam.
Fundi sanifu wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikiwete (JKCI) Renata
Kulwa akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography
- ECHO) mfanyakazi wa TATA Africa Holdings Limited wakati wa kambi maalum ya uchunguzi na
matibabu ya moyo iliyofanyika katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo vingunguti
Dar es Salaam.
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji
akimfundisha namna ya kuzingatia lishe bora mfanyakazi wa TATA Africa
Holdings Limited wakati wa kambi
maalum ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyofanyika katika ofisi za kampuni
hiyo zilizopo vingunguti Dar es Salaam.
Na JKCI
***************************************************************************************************************
Jamii imetakiwa kujenga utaratibu wa kufanya uchunguzi wa
afya mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo mara nyingi
hukua kimya kimya bila dalili za awali na hatimaye kuhatarisha maisha ya watu
wengi.
Wito huo umetolewa na Daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Edward Martin wakati wa kambi maalumu ya
uchunguzi na matibabu ya moyo iliyofanyika kwa wafanyakazi wa kampuni ya TATA
Africa Holdings Limited eneo la Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Dkt. Martin alisema bado kuna hitaji kubwa la kuongeza elimu
kwa umma kuhusu umuhimu wa kupima afya mapema, kwani ongezeko la magonjwa
yasiyoambukiza linachangiwa kwa kiasi kikubwa na mifumo duni ya maisha pamoja
na kukosa uelewa sahihi wa afya.
“Watu wengi hugundulika na matatizo ya moyo wakiwa katika
viwango vya juu vya hatari kwa sababu ya kutofanya uchunguzi wa afya mara kwa
mara",alisema Dkt. Martin.
“Tumekuwa tukikutana na wagonjwa wenye shinikizo la damu 200
juu ya 120 bila kujua kama wako hatarini. Wanapopata kiharusi ndipo hugundua.
Kama wangefanya uchunguzi mapema, wangeepuka hali hiyo",aliongeza.
Kwa upande wake Meneja wa Rasilimali Watu kutoka kampuni ya
TATA Africa Holdings Limited Kissa Mwasomola alisema zoezi hilo la upimaji
limeenda sambamba na maadhimisho ya wiki ya maadili ya kampuni hiyo ambayo
mwaka huu imejikita katika uwadilifu kwa vitendo.
“Tunawashukuru wataalamu wa JKCI kwa kutupatia huduma hizi
muhimu. Afya ni kipaumbele kwetu na ujio wao umetusaidia sana kupata vipimo na
elimu ya moyo bila usumbufu", alisema Kissa.
Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo walieleza kufurahishwa
na huduma hiyo huku wakisema imekuwa msaada mkubwa kutokana na changamoto ya
kukosa muda wa kwenda hospitalini.
“Mimi ni mvivu wa kwenda hospitali, lakini ujio wa JKCI hapa
kazini umenisaidia kupata vipimo vya moyo kirahisi", alisema Davis Moshi.
“Kwa upande wangu nina uzito mkubwa na madaktari wamenipa
ushauri wa kupanga mlo wangu vizuri kuanzia asubuhi hadi jioni. Nilikuwa nakula
bila mpangilio na ndiyo uliosababisha niongeze uzito", alisema Amina
Mweta.
Huduma za uchunguzi na elimu inayotolewa na Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) katika taasisi mbalimbali nchini zinalenga kuhakikisha
jamii inapima afya mapema, kutambua dalili hatarishi na kuchukua hatua kabla ya
magonjwa ya moyo kufikia hatua mbaya.





Comments
Post a Comment