Hatua mpya JKCI: Huduma za moyo sasa zinakufuata kazini

Afisa Masoko wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Mndasha akimkabidhi Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA. Nicodemas Deogratius Mkama folder lenye taarifa za taasisi hiyo wakati wa kambi maalum ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika ofisi za CMSA zilizopo Garden Avenue Tower jijini Dar es Salaam.

Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wafanyakazi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa kambi maalum ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika ofisi za CMSA zilizopo Garden Avenue Tower jijini Dar es Salaam.



Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Maria Samlongo akitoa elimu ya jinsi ya kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo kwa kufuata mtindo bora wa maisha kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA) wakati wa kambi maalum ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika ofisi zao zilizopo Garden Avenue Tower jijini Dar es Salaam.

Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kliniki ya Oysterbay, Nyanjura Nyaruga akimpima kiwango cha sukari kwenye damu Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA) Charles Shirima wakati wa kambi maalum ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika ofisi za CMSA zilizopo Garden Avenue Tower jijini Dar es Salaam.

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Theophil Ludovic akiwafundisha wafanyakazi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika ofisi zao zilizopo Garden Avenue Tower jijini Dar es Salaam.

**************************************************************************************************************************************************************************************************************

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kusogeza huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa jamii kwa kuwalenga wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi hatua inayolenga kuwafikia wale ambao mara nyingi hukosa muda wa kufuatilia afya zao kutokana na majukumu ya kazi.

Huduma hizo hutolewa moja kwa moja katika kampuni, mashirika ya serikali na taasisi binafsi ambapo wafanyakazi hufanyiwa uchunguzi wa afya, matibabu pamoja na elimu ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.

Akitoa elimu ya magonjwa ya moyo hivi karibuni kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Daktari Bingwa wa JKCI, Theophil Mushi alisema taasisi hiyo imepanua wigo wa utoaji wa huduma ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa bila kuathiri muda wao wa kazi.

“Tumesogeza huduma na sasa tunawafuata wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi. Tunawafanyia uchunguzi, kutoa matibabu na kuwapa elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Theophil.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA. Nicodemas Mkama, aliipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa hatua hiyo, akisema imewasaidia wafanyakazi kupata huduma bila kupoteza muda wa kazi.

“JKCI imefanya uamuzi mzuri kutufikia na kutupa huduma hizi muhimu. Wafanyakazi wetu wameweza kuchunguza afya zao bila kuathiri muda wao wa kazi”, alisema CPA. Mkama.

Aliongeza kuwa baada ya huduma hizo, wafanyakazi wa CMSA sasa wana uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kufuatilia afya zao na wanaweza kuendelea kupata huduma katika matawi ya JKCI ya Oysterbay na Kawe Kliniki.

Naye Afisa Lishe wa JKCI, Maria Samlongo alisema taasisi hiyo imetoa elimu ya lishe kwa wafanyakazi wa CMSA ili kuwasaidia kuchagua vyakula bora na kuelewa madhara ya mifumo isiyo sahihi ya maisha.

“Kupitia huduma hizi tumetoa ushauri wa mtu mmoja mmoja kuhusu umuhimu wa lishe bora katika kujenga afya ya moyo. Uelewa wa jamii kuhusu makundi sahihi ya chakula bado ni mdogo, ndiyo maana JKCI tumekuwa tukiwafuata wananchi kule waliko ili kuwajengea uelewa wa pamoja”, alisema Maria.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo