Benki ya Absa yachangia milioni 20 matibabu ya watoto wanaotibiwa JKCI
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akipokea hati ya makubaliano ya shilingi milioni 20 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania Obedi Laiser kwaajili ya kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa hafla fupi ya kusaini na kupokea hati ya makubaliano ya shilingi milioni 20 kutoka Benki ya Absa kwaajili ya kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania Obedi Laiser akizungumza wakati wa hafla fupi ya kusaini na kukabidhi hati ya makubaliano ya shilingi milioni 20 kwaajili ya kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa JKCI, Absa Benki na Global Medicare mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kusaini hati ya makubaliano ya shilingi milioni 20 kwaajili ya kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
PICHA JKCI.
**************************************************************************************
Benki ya Absa Tanzania imechangia kiasi cha shilingi milioni 20 kwaajili ya kusaidia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaopatiwa huduma katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kusaini hati ya makubaliano ya kupokea fedha hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema mchango huo unaonesha ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali katika kuhakikisha watoto wenye uhitaji wanapata matibabu ya moyo.
“Magonjwa ya moyo yanaendelea kuongezeka duniani ambapo sehemu kubwa ya watoto ni wale wanaozaliwa nayo na takwimu zinaonesha kuwa kati ya watoto 100 wawili huzaliwa na matatizo ya moyo hivyo tunawashukuru Absa Benki kwa kutambua umuhimu wa kuwasaidia watoto hawa ambao ni taifa la kesho”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema JKCI hupokea wastani wa watoto 1500 wanaohitaji matibabu ya moyo kila mwaka huku gharama za matibabu za kila mtoto zikianzia milioni nane na kuendela kulingana na aina ya tatizo hivyo msaada huo utasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili watoto na familia kwa ujumla.
“Huu ni uwekezaji muhimu kwa kizazi kijacho, Absa Benki imerejesha matumaini kwa watoto na familia zao kwa kurudisha upendo na matumaini kwa familia ambazo zina watoto wenye magonjwa ya moyo na hazina uwezo wa kugharama ia matibabu”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania Obedi Laiser alisema benki hiyo ina dhamira ya dhati katika kuleta mema na matumaini ya kuendelea kuishi hivyo kupitia dhamira hiyo ikaona ichangie matibabu ya watoto wanaotibiwa JKCI.
“Tunaamini kwamba nyuma ya kila mchango tunaoutoa kuna maisha ya watoto, kipaji, na ndoto zinazostahili kupewa nafasi ili ziweze kutimizwa bila kujali hali ya kiuchumi ya familia, hivyo kupitia msaada huu wa milioni 20 tutawapa watoto wanaohitaji matibabu nafasi ya kuendelea kutabasamu na kuishi maisha yenye matumaini”, alisema Laiser
Naye Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Global Medicare Daniel Lazaro aliishukuru JKCI kwa ushirikiano wake katika kufanikisha utolewaji wa msada huo kupitia taasisi ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) ambayo imekuwa mstari wa mbele kusaidia familia zisizokuwa na uwezo kupata matibabu ya moyo.
“Naiomba jamii na wadau wa maendeleo na taasisi mbalimbali kuendelea kushirikiana na JKCI katika kuwasaidia watoto wanaohitaji matibabu ili wapate nafasi ya kuishi na kutimiza ndoto zao”, alisema Lazaro
Wakitoa neno la shukrani wazazi watakaonufaika na msaada huo waliishukuru Taasisi ya Global Medicare kwa kuifikia Benki ya Absa Tanzania na kuwaomba kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo kwani kupitia mchango huo maisha ya watoto wao yameguswa.
“Kwa niaba ya wazazi wa watoto waliolazwa katika Taasisi hii tunawashukuru sana Absa Benk kwa kutugusa, tunaomba Taasisi zingine nazo ziige mfano huu ili watoto wengi zaidi wenye changamoto za moyo waweze kupatiwa huduma na kurejea katika maisha yao ya kawaida”, alisema Adam Nuhu.
- Mwisho -
.jpeg)
.jpeg)

.JPG.jpeg)
Comments
Post a Comment