Wananchi wapongeza huduma zinazotolewa na JKCI Maonesho ya Sabasaba

Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Lingido akimfundisha aina na makundi ya vyakula mwananchi aliyetembela banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Idd Kimario akimpima joto la mwili mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.


Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce akizungumza na mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Na JKCI

******************************************************************************************************

Wananchi wanaotembelea Kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) wamepongeza huduma za uchunguzi wa afya, elimu na ushauri wa kitaalamu zinazotolewa na wataalamu wa taasisi hiyo.

Wamesema huduma hizo zinawasaidia kutambua mapema hali zao za afya na kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza hususan magonjwa ya moyo pamoja na kuwajengea uelewa wa namna ya kuishi maisha yenye afya ili kujikinga na magonjwa hayo.

Mwanasheria kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Muhidin Mapeyo alisema ameridhishwa na hatua ya JKCI kusogeza huduma hizo muhimu za afya karibu na wananchi kupitia maonesho hayo.

“Nimepata fursa ya kutembelea banda la JKCI kwa sababu linatoa huduma muhimu zinazowawezesha wananchi kufahamu hali zao za afya. Nimepokelewa vizuri, na kabla ya kufanyiwa vipimo nilipatiwa maelezo yaliyonifanya nijisikie huru na tayari kupata huduma”, alisema Mapeyo.

Aliongeza kuwa mbali na vipimo vya afya wananchi pia wanapatiwa elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza na namna ya kubadili mtindo wa maisha ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa hayo.

Kwa upande wake mkazi wa Kilimanjaro Barakaeli Mrema alisema ametembelea banda la JKCI na kunufaika na elimu ya lishe bora pamoja na ushauri wa kitaalamu ambao hakuwahi kuupata hapo awali.

“Kilichonifurahisha zaidi ni ushauri wa lishe nilioupata, nimejifunza mbadala wa ulaji unaoweza kunisaidia kuboresha afya yangu na kupunguza utegemezi wa dawa”, alisema Mrema.

Naye mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam Habiba Ally alisema ametumia fursa ya maonesho hayo kupima afya yake na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu bingwa wa magonjwa ya moyo.

“Nimepima uzito, urefu na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu hawa wa moyo, pia nimeshauriwa kupunguza uzito ili uendane na urefu wangu jambo ambalo litasaidia kuboresha afya yangu”, alisema Habiba.

JKCI inaendelea kutoa huduma za uchunguzi wa afya, elimu na ushauri wa kitaalamu katika kliniki yake iliyopo Sabasaba ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kutambua mapema hali zao za afya na kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.


Comments

Popular posts from this blog

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi