JKCI na BMH kuokoa maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo kutoka nchini Burundi
Wataalamu wa upasuaji
wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na
wenzake wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kumfanyia upasuaji wa moyo mtoto
mwenye tundu kwenye moyo kutoka nchini Burundi wakati wa kambi maalumu ya
upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanyika katika Hospitali ya Benjamini Mkapa
iliyopo jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Prof. Abel Makubi akizungumza na wataalamu wa
upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walipofika
katika Hospitali hiyo kwaajili ya kubadilishana ujuzi pamoja na kufanya kambi
maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto.
Daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella
Mongela akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO) mtoto
kutoka nchini Burundi wakati wa kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto
inayofanyika katika Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo jijini Dodoma.
Na JKCI
************************************************************************************************
Watoto watano
kutoka nchini Burundi wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo kufanyiwa
upasuaji wa moyo na wataalamu wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Benjamin
Mkapa (BMH).
Upasuaji huo
kufanyika baada ya watoto hao kufanyiwa uchunguzi wa afya na kujadiliwa na jopo
la wataalamu katika kambi maalumu ya siku tano inayofanyika katika Hospitali ya
Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hii Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kwa Watoto wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau alisema kambi hiyo imelenga
kuwapatia matibabu ya kibingwa watoto hao na kuwapa nafasi ya kuishi bila ya kuwa na maumivu.
Dkt. Sharau
alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa kati ya watoto sita waliotakiwa
kufanyiwa upasuaji huo mtoto mmoja hatofanyiwa upasuaji kutokana na hali yake
ya kiafya kuwa dhaifu hivyo kuendelea na matibabu mengine hadi hali yake
itakapokuwa sawa.
“Tumewapokea
watoto sita kutoka nchini Burundi lakini baada ya uchunguzi wa kina imeonekana
mtoto mmoja hatutaweza kufanyiwa upasuaji wa moyo kwa kipindi hiki kutokana na
hali yake ya kiafya, Leo tumewafanyia upasuaji watoto wawili, mmoja alikuwa na
tundu katika vyumba vya juu vya moyo na mwingine mshipa wake wa damu uliopaswa
kufunga baada ya kuzaliwa ulikuwa haujafunga”,
alisema Dkt. Godwin
Kwa upande wake
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH)
John Meda alisema ushirikiano kati ya wataalamu wa Hospitali ya BMH na wenzao
wa JKCI utaboresha huduma na kutoa ujuzi kwa wataalamu hao.
“Tunaamini baada
ya kambi hii wataalamu wetu watabaki na ujuzi ambao utasaidia hapo baadaye
katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa watoto wenye magonjwa ya moyo”,
alisema Dkt. Meda.
Naye Daktari
Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Rehema
Yona alisema watoto wote wamefanyiwa uchunguzi wa afya wa kina ili kuwawezesha
wataalamu kubaini matatizo waliyonayo watoto hao na kujiridhisha kabla ya
kuwafanyia upasuaji wa moyo.




Comments
Post a Comment