Benki ya NBC kuchangia kiasi cha shilingi bilioni 1 matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 200 Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI iliyotolewa na Benki ya NBC kupitia mbio za NBC zilizofanyika jana jijini Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akisalimiana na Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa wakati wa mbio za NBC zilizofanyika jana katika  uwanja wa michezo Jamhuri uliopo jijini Dodoma.


 

Mjumbe wa bodi ya wadhamini wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Kassim Hussein akishiriki katika mazoezi ya viungo wakati wa mbio za NBC zilizofanyika jana katika uwanja wa michezo Jamhuri uliopo jijini Dodoma kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI. 

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakionesha medali zao mara baada ya kushiriki katika mbio za NBC zilizofanyika jana katika uwanja wa michezo wa Jamhuri uliopo jijini Dodoma kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.



Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani na wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakifurahia mara baada ya kushiriki katika mbio za NBC zilizofanyika jana jijini Dodoma kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.


Na JKCI
***********************************************************************************************************************************************************************************************

Benki ya NBC kuchangia shilingi bilioni 1 kwaajili ya matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Fedha hizo zinatarajiwa kutolewa kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo kupitia mbio za NBC ambapo mwaka huu zimefanyika jana jijini Dodoma na kuchangia shilingi milioni 200 kwaajili ya matibabu ya watoto hao.

Akizungumza wakati wa mbio hizo jana jijini Dodoma Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mwigulu Nchemba alisema matumizi ya fedha zilizotolewa kusaidia matibabu yaendane na thamani ya fedha hizo huku yakitumika kwa uwazi ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kuonekana.

“Ni muhimu kuona thamani ya kila senti inayotolewa na wadau hawa kwa kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa kusudi lililokusudiwa na kuwafikia walengwa wanaohitaji huduma za matibabu” alisema Mhe. Nchemba.

Mhe. Mwigulu alisema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwekeza katika Sekta ya Afya na kuhakikisha kuwa wadau wanaounga mkono jitihada za serikali wanasaidiwa kwani kusudi la wadau na Serikali ni kuhakikisha kuwa uhai wa watanzania unathaminiwa na kulindwa.

Aidha Mhe. Mwigulu aliwataka watanzania kuendelea kufanya mazoezi kwaajili ya afya zao kwani afya bora ndio inayojenga taifa lenye uchumi imara.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Benki ya NBC Theobald Sabi alisema benki hiyo imeendelea kutekeleza wajibu wake kwa jamii kwa kuwekeza katika sekta ya afya, elimu na maendeleo ya jamii, ambapo mwaka huu imetoa kiasi cha shilingi milioni 200 kwa JKCI kama sehemu ya kurudisha kwa jamii na kuleta furaha kwa watoto wenye magonjwa ya moyo.

“Tunatambua kuwa gharama za matibabu ya moyo ni kubwa hivyo mchango huu umelenga kuwasaidia watoto wengi kupata huduma za matibabu kwa wakati na kurejesha matumaini kwa familia zao. NBC itaendelea kuwa mshirika wa maendeleo katika sekta ya afya kwa manufaa ya jamii”, alisema Sabi.

Sabi aliongeza kuwa mbio za NBC zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha wadau mbalimbali katika kusaidia jamii huku zikihamasisha wananchi kufanya mazoezi na kuchangia katika huduma za afya.



 

Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma