Watu 1,089 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo kambi maalumu ya Mhe. Makonda

Wananchi kutoka mikoa mbalimbali ya Kaskazini wakiwa katika foleni ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya kupima na kutibu magonjwa ya binadamu iliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge wa Arusha mjini Mhe. Paul Makonda na kufanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Jumla ya watu 1,089 wamepimwa moyo.

Daktari wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Adda Justine akimpatia maelekezo mwananchi aliyefika kufanya uchunguzi wa afya wakati wa kambi maalumu ya kupima na kutibu magonjwa ya binadamu iliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge wa Arusha mjini Mhe. Paul Makonda na kufanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Jumla ya watu 1,089 wamepimwa moyo.

Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Mhe. Paul Makonda akizungumza na wananchi waliokuwa wakisubiri kupata huduma katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kambi maalumu ya kupima na kutibu magonjwa ya binadamu iliyokuwa ikifanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kumalizika leo jijini Arusha. Jumla ya watu 1,089 wamepimwa moyo.

Na JKCI

***************************************************************************************************

Watu 1,089 wakiwemo wanawake 818 na wanaume 271 wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya uchunguzi wa magonjwa ya binadamu iliyomalizika leo jijini Arusha.

Kambi hiyo iliyoandaliwa na Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Mhe. Paul Makonda imeshirikisha hospitali zinazotoa huduma bingwa bobezi nchini ambapo watu zaidi ya elfu 13 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ya binadamu.

Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) Salehe Mwinchete alisema watu 739 walifanyiwa uchunguzi kwa kupimwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography - ECHO).

“Kupitia kambi hii tumeweza kuwafanyia watu 777 kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography - ECG) ambapo baadhi yao waligundulika kuwa na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo na kuwapa rufaa kwaajili ya uchunguzi zaidi”, alisema Dkt. Salehe

Dkt. Salehe alisema katika kambi hiyo pia kulikuwa na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto ambaye alitoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watoto 63 waliohitaji huduma za moyo.

“Tumetoa rufaa kwa watu 119 kwenda katika matawi yetu kwaajili ya uchunguzi zaidi, watu hawa tumewakuta na matatizo mbalimbali ya moyo ikiwemo magonjwa ya shinikizo la damu, sukari kwenye damu, matatizo ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo, moyo kutanuka, matatizo ya kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo, moyo kushindwa kufanya kazi na matundu ya moyo kwa watoto”, alisema Dkt. Salehe

Kwa upande wa wananchi waliopata huduma katika banda la JKCI wakati wa kambi hiyo wamewapongeza wataalamu wa JKCI kwa kutoa huduma kwa upendo bila kuchoka na kuhakikisha watu wote waliohitaji huduma za moyo wanazipata.

Daud Olesekei alisema huduma aliyoipata katika banda la JKCI imemsaidia kujitambua, kuchukua hatua za mapema na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ile magonjwa ya moyo aliyonayo yasimdhuru zaidi.

“Nimefurahi sana kupata huduma katika banda la JKCI, tunamuomba Mhe. Makonda aendelee kutuletea wataalamu hawa ili hata sisi tusiokuwa na uwezo wa kuzifuata huduma bingwa za uchunguzi wa magonjwa ya moyo mahali zilipo tuweze kuzipata”, alisema Daud.

Naye Catherine Tarimo mkazi wa Kilimanjaro aliiomba Serikali iangalie namna ya kufanya kambi kama hiyo katika mikoa yote ya Tanzania kuwasaidia wananchi wake kupata huduma za afya na dawa pale inapohitajika.

“Nimetoka Kilimanjaro hadi hapa Arusha kwaajili ya kambi hii ya Mhe. Makonda, nimefurahi nimepata huduma na baada ya huduma nimepata dawa bila gharama yotote”, alisema Catherine.

Kambi maalumu ya uchunguzi wa magonjwa ya binadamu mkoani Arusha inayoratibiwa na Ofisi ya Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Mhe. Paul Makonda imefanyika kwa siku saba na kuhudumia wananchi kutoka mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani.

 

Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma