DC Ubungo, msanii wa mziki G Nako wahamasisha wananchi kujua Namba Zao za Afya
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Albert Msando pamoja na msanii wa bongo
fleva George Mdemu almaarufu kama G Nako alipofika katika Taasisi hiyo tawi la
Oysterbay kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya.
Mkuu
wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Albert Msando amewahimiza wananchi kuwa na utamaduni
wa kupima afya zao mara kwa mara ili kujua namba zao mapema na kupata matibabu
sahihi kwa wakati.
Rai
hiyo imetolewa jana na Mhe. Msando alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) tawi la Osterbay akiwa ameongozana na msanii wa Bongo Fleva George Mdemu
almaarufu kama G Nako kwa ajili ya kufanya vipimo vya afya na kujua namba zake.
Mhe.
Msando alisema wananchi wanapaswa kuchukulia uzito suala la afya zao na
kuhakikisha wanafahamu namba zao ili waweze kupata ushauri na matibabu kwa
wakati.
“Kama
tunavyofahamu sasa hivi taasisi yetu ya JKCI wanaendesha kampeni ya kuhamasisha
kila mwananchi kufahamu namba zake na mimi nimeongozana na G Nako kwa ajili ya
kufanya vipimo na kufahamu namba zake”, alisema Mhe. Msando
Aidha
Mhe. Msando alimpongeza msanii huyo kwa kuitikia wito wa kushirikiana na JKCI
katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kupima afya mara kwa mara.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Peter Kisenge alisema Taasisi hiyo imeendelea kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali
lengo likiwa ni kuiwezesha jamii kufahamu afya zao.
“Leo
tumetembelewa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Albert Msando na mwanamuziki G
Nako ambaye amekuja kwa ajili ya kupima afya yake na kujua namba zake, ni
muhimu wasanii wakaiga mfano wake na kujitokeza kupima kuepuka madhara
yanayoweza kujitokeza kama hawatapima afya zao mara kwa mara”, alisema Dkt.
Kisenge.
Dkt.
Kisenge alisema JKCI imekuwa ikipanua huduma zake kwa kuzisogeza karibu na
wananchi, kutoa huduma kwa makundi mbalimbali ikiwemo wasanii, wanamichezo,
waandishi wa Habari, na makundi mengine yaliyopo katika jamii.
Akizungumzia
umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya msanii wa Bongo Fleva George Mdemu almaarufu
kama G Nako alisema wananchi hususan wasanii wanapaswa kuwa na utamaduni wa
kupima afya zao mara kwa mara pale wanapopata nafasi.
“Kuna
wakati tunaona baadhi ya wasanii wanaanguka wakiwa katika steji, kuna wengine
wamekuwa wakipata matatizo ya shinikizo la damu lakini kuna ambao hawajui wingi wa sukari yo kwenye
damu, uzito au wingi wa mafuta kwenye damu hivyo ni muhimu kufanya uchunguzi wa
afya kabla ya kupata maradhi”, alisema G Nako.
Kampeni
ya JKCI ya kuhamasisha wananchi kujua namba zao za afya inaendelea kuwa sehemu
ya juhudi za taasisi hiyo katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchunguza
afya na utambuzi wa mapema wa changamoto mbalimbali za kiafya.
Comments
Post a Comment