JKCI yapongezwa kwa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za moyo kwa wananchi

 


Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dkt. Saada Mkuya akipokea zawadi kutoka kwa Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hania Bwahama alipotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa mkutano wa Mabunge wanawake wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (WPC) uliokuwa ukifanyika katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo jijini Dar es Salaam



Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dkt. Saada Mkuya akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa mkutano wa Mabunge wanawake wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (WPC) uliokuwa ukifanyika katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo jijini Dar es Salaam.


Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Moses Manumbu akimpima uzito mshiriki wa mkutano wa Mabunge wanawake wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (WPC) uliokuwa ukifanyika katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo jijini Dar es Salaam


Fundi sanifu wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Gerson Mpondo akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) mshiriki wa mkutano wa Mabunge wanawake wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (WPC) uliokuwa ukifanyika katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo jijini Dar es Salaam


Washiriki wa mkutano wa Mabunge wanawake wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (WPC) wakisubiri kupata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo kutoka kwa wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa mkutano huo uliokuwa ukifanyika katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo jijini Dar es Salaam.

Picha na JKCI.


*********************************************************************************************************************************

Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Mhe. Dkt. Saada Mkuya ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa jitihada zake za kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za matibabu ya moyo nchini na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi kupitia matawi yake.

Pongezi hizo zimetolewa leo alipotembelea banda la JKCI lililopo katika mkutano wa Mabunge Wanawake wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (WPC) uliokuwa ukifanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Mhe. Saada alisema JKCI imekuwa ikifanya kazi nzuri katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu afya ya moyo hivyo kuwawezesha kupata huduma kwa urahisi zaidi.

“JKCI imejitahidi kujijengea utambulisho mzuri kutokana na ubora wa huduma zake pamoja na kuwa na wataalamu wa afya waliobobea katika uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo, na jambo la kufurahisha zaidi ni kuona kwamba sasa hata wagonjwa kutoka nje ya nchi wanakuja Tanzania kupata huduma katika taasisi hii, hili ni jambo la kujivunia”, alisema Mhe.Saada

Nao baadhi ya viongozi wa taasisi, mashirika ya kiraia na washirika wa maendeleo wameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa elimu kuhusu afya ya moyo na kusogeza huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo karibu na maeneo ya kazi.

“Huduma hizi ni nzuri, niwaombe wale ambao hawajapata fursa ya kupima wakati mwingine wafike ili waweze kujua hali zao mapema kwani wanapobaini tatizo la kiafya katika hatua za awali wanapata fursa ya kupata huduma stahiki bila kuchelewa”, alisema Mkurugenzi wa Idara ya Ushauri wa Kisheria wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Nasra Awadhi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Wanasheria Wanawake Tanzania TAWLA Tike Mwambipile ameipongeza taasisi hiyo kwa kuendesha kliniki ya magonjwa ya moyo katika mkutano huo kuwawezesha viongozi hao kupata huduma kwa urahisi na kuokoa muda.

“Nimefurahi kupata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo hapa, hii imenisaidia sana kwa kuwa awali nilikuwa napata hofu ya kufika JKCI kupata huduma za moyo. Nimekutana na daktari bingwa katika kliniki iliyoweka katika mkutano huu na kunisaidia kujua hali ya afya ya moyo wangu”, alisema Tike.






Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma