Waagizaji na wasambazaji wa dawa za binadamu za moyo waahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo wapate dawa kwa wakati
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa katika
picha ya pamoja na waagizaji
na wasambazaji wa dawa za binadamu za moyo mara baada ya kumalizika kwa mkutano
baina yao ambao ulijadili changamoto zinazowakabili na jinsi ya kuzitatua ikiwa
ni kuboresha upatikana wa dawa kwa
wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo. Mkutano huo ulifanyika hivi karibuni
katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) umekutana na waagizaji na wasambazaji wa dawa za binadamu za moyo ili kujua changamoto zinazowakabili na jinsi ya kuzitatua ikiwa ni kuboresha upatikana wa dawa kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Kikao
hicho cha wadau hao kilifanyika hivi
karibuni katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam ambapo wawakilishi
zaidi ya 30 kutoka kampuni mbalimbali za dawa walihudhuria.
Akizungumza mara baada ya kumalizika
kwa kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Prof. Mohamed Janabi alisema lengo la
kukutana na wadau hao ilikuwa ni kuangalia
changamoto zinazowakabili na namna ya kuzitatua.
Prof.Janabi ambaye pia ni daktari bingwa
wa magonjwa ya moyo alisema ukikosa dawa za moyo unahatarisha maisha ya mgonjwa
hivyo basi kujenga uhusiano na wadau hao ni jambo la muhimu. Siku za nyuma mawasiliano yao yalikuwa kwa kupitia
mitandao (barua pepe), simu na sio kuonana uso kwa uso kama ilivyotokea katika
kikao hicho wameweza kufahamiana jambo
ambalo litawasaidia katika utendaji wao
wa kazi wa kila siku.
“Kulikuwa na changamoto za
mawasiliano, kutokufuatwa kwa taratibu za kuagiza dawa, kutokufahamu maoteo ya
dawa sawa sawa, kutoletwa dawa zote kamili kama zilivyoagizwa haya yote
tumeyazungumzia na kupata utatuzi.
Katika Taasisi yetu hatukuwa na matatizo ya upatikanaji wa dawa kwa asilimia 85,
ninaamini baada ya kikao hiki tutakuwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa kwa
asilimia 100 na mgonjwa atapata dawa zote alizoandikiwa na daktari”.
“Tutakuwa na maoteo ya dawa sahihi zaidi baada ya
mazungumzo yetu, kwani ukiwa na dawa za kutosha kwa kipindi cha miezi 3 hadi 4
na ikifika katikati ya miezi miwili ukaagiza zingine una uhakika wa kuwa na
dawa za kutosha muda wote. Haya ni baadhi ya mambo ambayo tumekubaliana”,
alisema Prof. Janabi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema tangu
kuanzisha kwa Taasisi hiyo sasa ni mwaka wa sita na hii ni mara ya kwanza kuwa
na mkutano na wasambazaji wa dawa. Wamekubaliana kadri hali itakavyoruhusu watakutana
angalau mara moja kwa mwaka.
“Sisi tunanunua dawa zetu kutoka
Bohari ya Dawa (MSD) kama MSD hawana baadhi ya dawa tunazohitaji tunatangaza
zabuni hivyo basi hawa waigizaji na wasambazaji wa dawa ni wadau muhimu kwetu”, alisisitiza Prof.
Janabi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha
Ununuzi na Ugavi cha Taasisi hiyo Bunare Danieli aliwajulisha washiriki kuwa
ununuzi wa umma unaongozwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.7 ya mwaka 2011 pamoja na Kanuni zake za
mwaka 2013 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016. Hivyo, aliwaasa wajumbe
hao kuifahamu vyema sheria hiyo na kuizingatia wakati wote wanaposhiriki katika
zabuni za umma na utekelezaji wa mikataba.
Aidha, aliwakumbusha kushiriki mafunzo
mbalimbali ya Sheria ya Ununuzi wa Umma yanayoandaliwa na taasisi
zilizothibitishwa kutoa mafunzo hayo hapa nchini.
Bunare pia aliwakumbusha watoa huduma
hao kuwa kuanzia Januari, 2020 Ununuzi
wa Umma ulianza kufanyika kupitia Mfumo
wa Kielektroniki (Tanzania eLectronic Procurement
System – TANePS). Mfumo huo una
lengo la kuongeza ufanisi na uwazi katika ununuzi wa umma.
“Changamoto kadhaa zinazotukabili wakati wa utekelezaji
wa mikataba ya ununuzi ni pamoja na ucheleweshaji wa bidhaa tofauti na muda
ulioainishwa kwenye mkataba hali inayosababisha Taasisi kukosa dawa na malipo
kwa wazabuni kuchelewa, baadhi ya wazabuni wanawasilisha mahitaji nusu nusu
badala ya kuwasilisha kwa pamoja na pia wazabuni wamekuwa wakichanganya oda
zaidi ya moja kwenye hati moja ya madai bila kutoa maelezo yanayojitosheleza”,
alifafanua Bunare.
Nao waingizaji na wasambazaji wa dawa walishukuru kwa mkutano
huo ambao umeonesha ni jinsi gani Taasisi hiyo ina nia ya kufanya nao kazi na kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati
sahihi na kuziomba Taasisi zingine kuiga
mfano huo.
Wazabuni wengi walionesha nia ya
kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kurekebisha kasoro zilizoainishwa kwenye
kikao hicho kwa lengo la kuhakikisha wao pia wanakuwa sehemu ya mafanikio ya
Taasisi hiyo.
Emmanuel Kasembe mwakilishi kutoka
kampuni ya Laborex Tanzania Ltd alisema kuitishwa kwa mkutano huo kunaonesha ni
jinsi gani Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamejipanga kuboresha huduma
za matibabu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati sahihi
“Changamoto kubwa tuliyokuwa
tunakutana nayo ni jinsi ambavyo tenda ilikuwa inatangazwa kwa muda mfupi na
utunzaji wetu wa kumbukumbu. Katika mkutano huu
maelezo ya kina yametolewa ya
jinsi ya kukabiliana na changamoto hizi na ninaamini tutakuwa na matokeo bora
zaidi katika utendaji wetu wa kazi”, alisema Kasembe.
“Mkutano huu umesaidia kujenga na
kuimarisha uhusiano kati yetu na JKCI. Ninaomba uendelee kuwepo kwani tumeweza
kuzifahamu changamoto zinazowakabili JKCI nasi pia tumesema changamoto zetu na
kufikia muafaka. Hii itatusaidia kuimarisha huduma za usambazaji wa dawa
tunazozitoa siyo tu JKCI hata katika maeneo mengine”, alisema Jackline Mally
kutoka Horizon Pharmacy Ltd.
“Kitu kizuri kwa Taasisi hii wanalipa
madai yetu kwa wakati ndio maana leo unatuona tupo hapa makampuni zaidi ya 30
lakini hamna mwenye kuidai Taasisi hii”, alipongeza Rupesh Pillai Mkurugenzi
Mtendaji wa Philips Pharmaceutical (T) Ltd.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed
Janabi akizungumza na waagizaji
na wasambazaji wa dawa za binadamu za moyo wakati
wa mkutano baina yao ambao ulijadili changamoto zinazowakabili na jinsi ya
kuzitatua ikiwa ni kuboresha upatikana
wa dawa kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo. Mkutano huo ulifanyika
hivi karibuni katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya dawa ya Philips Pharmaceutical (T) Ltd. Rupesh Pillai akieleza namna ambavyo kampuni yake inavyofanya kazi na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa mkutano baina ya uongozi wa JKCI na waagizaji na wasambazaji wa dawa za binadamu za moyo ulifanyika hivi karibuni katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi kutoka kampuni ya dawa ya Astrazeneca Bernard Rokat akichangia mada wakati wa kikao na uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa mkutano baina ya uongozi wa JKCI na waagizaji na wasambazaji wa dawa za binadamu za moyo uliofanyika hivi karibuni katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment