Wagonjwa sita wenye matatizo ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo wamepata matibabu katika kambi maalum ya matibabu JKCI
Wataalamu wabobezi wa moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri wakimtibu mgonjwa mwenye matatizo ya hitilamu ya mfumo wa
umeme wa moyo ambaye mapigo yake ya moyo
yanakwenda haraka kuliko kawaida (Tachyarrhythmia’s)
wakati wa kambi maalum siku mbili ya matibabu hayo iliyofanyika hivi karibuni katika
Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa sita walitibiwa katika kambi hiyo.
Na: JKCI
Wagonjwa sita wenye matatizo ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa
moyo ambao mapigo yao ya moyo yanakwenda haraka kuliko kawaida (Tachyarrhythmia’s)
wamepata matibabu katika kambi maalum ya matibabu hayo iliyomalizika hivi
karibuni katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Kambi hiyo ya siku mbili ilifanywa na madaktari wa Taasisi
hiyo kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mtaalamu mbobezi wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye pia ni mratibu wa kambi hiyo Dkt. Yona Gandye
alisema katika hali ya kawaida moyo hupiga kati ya mapigo 60 hadi 100 kwa dakika.
Dkt. Gandye alisema mtu akiwa na tatizo katika mfumo wa umeme
wa moyo ambalo anaweza kulipata aidha kwa kuzaliwa nalo au athali ya ugonjwa linapelekea
mfumo wa umeme wa moyo kubadili mapigo yake inaweza kuwa chini ya mapigo 60 kwa dakika au kuwa juu ya 100 kwa dakika.
“Sababu mbalimbali
zinaweza kuufanya moyo udunde kwa haraka kuliko kawaida hii ni pamoja na mtu kuzaliwa
na tatizo, kwa kurithi kutoka kwa wazazi hata kama wao hawakuwa na dalili.
Sababu ya pili ni ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, moyo kutanuka na kuwa na misuli mikubwa ya moyo (Hypertrophy).
“Mgonjwa anakuja kliniki akiwa na dalili za moyo kushindwa
kufanya kazi ambazo ni miguu kuvimba, pumzi kubana, kushindwa kulala vizuri
usiku. Ukimfanyia vipimo unakuta moyo wake umetanuka na umefika mahali umeme
wake wa moyo haufanyi kazi vizuri”, alisema Dkt. Gandye.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na
matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo Prof.
Mervat Aboulmaaty kutoka Hospitali
ya Shifa iliyopo nchini Misri alisema
amefurahi kuona taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefunga mtambo wa kisasa
wa Cathlab ambao umeungaishwa na mtambo wa
Carto 3 System 3D & mapping
electrophysiology System wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo.
Prof. Mervat alisema, “Kufungwa kwa mashine hii ya kisasa na
yenye teknlologia ya hali ya juu kutaweza kuokoa maisha ya watu wengi wenye
matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo nchini Tanzania”,.
Alisema katika katika kambi hiyo licha ya kutibu, wataalamu
walibadilishana ujuzi wa jinsi ya kutibu wagonjwa wenye tatizo hilo la moyo
unaokwenda kwa haraka.
Aliongeza kuwa kupitia chuo kikuu cha Ain Shams cha nchini
Misri wanatoa elimu kwa njia ya mtandao kuhusu matibabu hayo ambapo madaktari
wengi wa Afrika wakiwemo wa Tanzania wamekuwa wakishiriki.
“Hii inamaana kuwa baada ya miaka michache ijayo tutakuwa na
madaktari wengi wenye utaalamu wa kutoa matibabu ya hitilafu ya mfumo wa umeme
wa moyo ambao mapigo yake yanakwenda
haraka kuliko kawaida na kuweza kuokoa maisha ya wagonjwa wenye matatizo haya”, alisema
Prof. Shams ambaye pia ni mkufunzi katika chuo hicho.
Naye mtaalamu mbobezi wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Reuben Mutagaiwa ambaye alishiriki katika kambi hiyo alisema waliandaa wagonjwa
ambao walikuwa na dalili za ugonjwa wa
mfumo wa umeme wa moyo baada ya
kuwachunguza kwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Stress
Electrocardiography – ECG) waligundulika kuwa na tatizo.
“Ili kuchunguza na kubaini zaidi kuna vipimo ambavyo vinafanyika
kwa kitaalamu vinajulikana kama Electrophysiological (EP) studies & ablation ambapo
mgonjwa anaingizwa katika chumba cha upasuaji (Cathlab) kwa
ajili ya uchunguzi wa mfumo wa umeme wa moyo (electrophysiology) unasisimua
yale matatizo ambayo yalionekana katika
kipimo cha ECG (Induction of Arrhythmias) baada ya kuuleta umeme wa moyo ambao
hauna upangilio unaweza kufahamu ni upande gani umeme huo unatoka na kuweza kuudhibiti”,
alisema Dkt.Mutagaiwa.
Dkt. Mutagaiwa alisema baada ya kugundua kama tatizo liko kwenye upande wa kushoto au wa
kulia wa moyo kuna kifaa maalum kiitwacho
Ablator ambacho kinatoa joto na ukiliweka sehemu ambayo umeme wa moyo
hauna mpangilio unatoka unaweza kumtibu mgonjwa kwa kuziunguza njia hizo.
“Kwa kawaida wagonjwa hawa walikuwa wanawekwa katika dawa za
vidonge lakini dawa zinaukomo wake, hadi wanafanyiwa matibabu haya
walishashindikana kwenye dawa hivyo basi matumizi ya dawa tuliyasimamisha na kuwafanyia tiba hii”.
“Faida kubwa ya tiba hii ni mgonjwa kupona moja kwa moja na baadaye mgonjwa anashauriwa
kutumia dawa na kuendelea na kliniki yake kama kawaida”, alisisitiza Dkt.
Mutagaiwa.
Matibabu hayo yamefanyika kwa mara ya kwanza katika maabara
ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo (Catheterization Laboratory -
Cathlab) mpya ambapo mwanzoni mwa mwaka jana Serikali ilitoa kiasi cha shilingi
bilioni 4.6 kwa ajili ya kufunga mtambo huo ambao umeungaishwa na mtambo wa Carto 3 System 3D & mapping electrophysiology System wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo.
Matibabu ya tatizo la hitilamu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yake yanakwenda haraka kuliko kawaida (Tachyarrhythmia’s) yalianza kutolewa hapa nchini mwaka 2019 ambapo hadi sasa wagonjwa 11 wameshapata matibabu.
Comments
Post a Comment