Serikali yaombwa kuyaingiza magonjwa yasiyoambukiza katika bima ya afya kwa watu wote

Katibu wa Shirikisho la Vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) Prof. Kaushik Ramaiya akiwasilisha mada kuhusu ukubwa wa tatizo la magonjwa yasiyoambukiza wakati wa uzinduzi wa mkakati wa utetezi juu ya bima ya afya kwa watu wote inayojumuisha magonjwa yasiyoambukiza uliofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam. Uzinduzi huo uliandaliwa na Shirikisho la Vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA).

Katibu wa Shirikisho la Vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) Prof. Kaushik Ramaiya akizungumza na wadau wa afya walioshiriki katika uzinduzi wa mkakati wa bima ya afya kwa wote inayojumuisha magonjwa yasiyoambukiza uliofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam. Walioshiriki katika uzinduzi huo ni wadau mbalimbali  wakiwemo wizara ya Afya, wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Dawa za kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza, Kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza na wahariri wa habari.

Mdau wa Afya akielezea umuhimu wa bima ya afya kwa wote wakati wa uzinduzi wa mkakati wa bima ya afya kwa wote inayojumuisha magonjwa yasiyoambukiza uliofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam. Walioshiriki katika uzinduzi huo ni wadau mbalimbali  wakiwemo wizara ya Afya, wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Dawa za kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza, Kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza na wahariri wa habari.


Mbunge wa Jimbo la Mbozi mkoani Songwe Mhe. George Mwenisongole akielezea jinsi uwepo wa bima ya afya kwa watu wote itakavyowasaidia wananchi hasa wanaoishi vijijini wakati wa uzinduzi wa mkakati wa bima ya afya kwa wote inayojumuisha magonjwa yasiyoambukiza uliofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam. Uzinduzi huo uliandaliwa na Shirikisho la Vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA).

Picha na Henrick Chiwangu 


**************************************************************************************************************************

Serikali imeombwa kuingiza matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza katika bima ya afya kwa wote ili kupunguza changamoto zinazowapata watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza kwani tathmini iliyofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonesha zaidi ya asilimia 45 ya vifo vinavyotokea duniani hutokana na magonjwa hayo.

Ombi hili limetolewa hivi karibuni na Katibu wa Shirikisho la Vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) Prof. Kaushik Ramaiya wakati wa uzinduzi wa mkakati wa utetezi juu ya bima ya afya kwa watu wote inayojumuisha magonjwa yasiyoambukiza uliofanyika katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.

Prof. Ramaiya alisema mfuko wa Taifa wa bima ya afya una bima za aina mbalimbali ambazo zimekuwa zikitoa huduma za matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza pamoja na magonjwa mengine, lakini baadhi ya huduma za matibabu hazipatikani katika bima hizo na hivyo kuwanyima fursa wagonjwa kupata huduma iliyokamilia wanapofika hospitali kupata matibabu.

“Magonjwa yasiyoambukiza yanagharama kubwa katika kuyatibu, kupitia mfuko wa Taifa wa bima ya afya wananchi wamekuwa wakikata bima za afya za aina mbalimbali lakini kadi hizo zimekuwa zikitoa baadhi ya huduma, na huduma nyingine kama dawa, upasuaji na vifaa kutokuwepo katika bima hivyo kuwanyima fursa wagonjwa ya kupata matibabu kamili”,.

“Ninaiomba Serikali iliangalie hili kwani tathmini iliyofanywa na WHO inaonesha baada ya miaka mitano hadi kumi ijayo vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza vinaweza kuongezeka na kuwa zaidi ya asilimia 55”,

“Magonjwa yasiyoambukiza yasipotibiwa vizuri hupelekea mtu kupata madhara mengine kama vile kudhuru figo, mishipa ya damu, macho, kupata kiharusi na madhara mengine mengi ambayo humsababishia mtu kupoteza uhai wake”, alisema Prof. Ramaiya.

Aidha Prof. Ramaiya aliiomba Serikali kuratibu upatikanaji wa matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza katika maeneo yote yenye zahanati na vituo vya afya ili jamii iweze kupata huduma maeneo ya karibu na kwa wakati hivyo kupunguza madhara yanayoweza kutokea kama magonjwa hayo hayatatibiwa mapema.

“Kama wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza watapata huduma za matibabu kwa wakati katika vituo vya karibu vya afya wataweza kuendelea na shughuli zao za kiuchumi hivyo kukuza vipato vyao na pato la taifa”,.

“Jamii inapaswa kujikinga na magonjwa haya yasiyoambukiza kwani utafiti uliofanywa na WHO unaonesha kila dola moja unayoiweka katika kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza unapata nafuu ya dola 7 hadi 12 kwa kila dola uliyotumia kuwekeza katika kinga”, alisema Prof. Ramaiya

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mkoa wa Songwe Mhe. George Mwenisongole alisema suala la bima ya afya kwa wote likawe ajenda ya kitaifa ili kutoa fursa kwa kila mtanzania kuwa na matumaini ya kupata matibabu pale wanapougua  magonjwa mbalimbali.

“Bima ya afya kwa wote inapaswa kuwa bima isiyobagua lakini bima inayotoa huduma zote za matibabu ili watanzania wafaidike na huduma za matibabu hasa wale wenye magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakitibiwa kwa gharama kubwa”,

“Nimepata nafasi ya kushiriki semina iliyoandaliwa na TANCDA na kujifunza mengi kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza, wito wangu kwa Serikali ni kuhakikisha tunapata sera ya kitaifa ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo itaweza kuzuia uvutaji wa sigara hadharani ili kuokoa maisha ya watu wanaoathirika na moshi wa sigara”, alisema Mhe. Mwenisongole

Naye Mhariri wa Makala kutoka gazeti la Habarileo Gloria Tesha aliiomba Serikali iwekeze katika elimu ya magonjwa yasiyoambukiza kuanzia ngazi ya shule za msingi ili watoto wanapokuwa wawe na ufahamu wa kutosha juu ya magonjwa hayo, hii itawasaidia kujikinga na magonjwa hayo.

“Waandishi wa habari tupo tayari kutumia kalamu zetu kupaza sauti ili jamii ifahamu athari za magonjwa yasiyoambukiza na namna ambavyo itaweza kujikinga na magonjwa hayo. Ninaiomba Serikali pamoja na taasisi zinazojihusisha na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kututumia ili tuweze kuzifikia jamii na kuziokoa”,

“Wadau na Serikali kwa pamoja tukubaliane kupiga vita magonjwa yasiyoambukiza kwa kuyafanya magonjwa haya kuwa ajenda ya kitaifa katika kila kikao kinachofanyika kuanzia ngazi za mitaa, kata, wilaya na mikoa ajenda hiyo ikipewe kipaumbele ninaamini tutaweza kupunguza ama kuyaondoa kabisa magonjwa haya”, alisema Gloria.

Uzinduzi wa mkakati wa utetezi juu ya bima ya afya kwa watu wote inayojumuisha magonjwa yasiyoambukiza uliandaliwa na Shirikisho la Vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) na kushirikisha wadau mbalimbali  wakiwemo wizara ya Afya, wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Dawa za kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza, Kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza na wahariri wa habari.

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari