Wagonjwa 19 ambao mishipa yao ya damu ya moyo ilikuwa imeziba kwa asilimia 100 na kushindwa kupitisha damu na ambao valvu zao za moyo zilikuwa zimeziba wafanyiwa upasuaji mdogo
Upasuaji huo unafanyika kwa kutumia mtambo wa Cathlab
(Catheterization Laboratory) ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalum kwa
ajili ya uchunguzi wa matatizo na tiba za magonjwa ya moyo.
Kati ya hao wagonjwa 15
ni wenye matatizo ya mishipa ya damu ya moyo iliyoziba sehemu kubwa kwa
asilimia 100 na haikuwa inapitisha damu kabisa wamefanyiwa upasuaji mgumu
(Complex Percutaneous Coronary Intervention – PCI) na wanne ambao valvu zao
zilikuwa zimezibwa na ilibidi wafanyiwe upasuaji mkubwa wa kufungua kifua na kuzibadilisha valvu hizo wamezibuliwa valvu kwa njia ya upasuaji mdogo (Balloon Mitral Valve -BMV).
Akizungumzia kuhusu kambi hiyo ya siku tano ambayo ilianza
tarehe 14 hadi 18 mwezi huu daktari
bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka JKCI Peter Kisenge alisema wanafanya matibabu
hayo kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika lililopo
nchini Marekani.
“Kwa kushirikiana na madaktari wenzetu ambao wanautaalamu
mkubwa kuliko sisi wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo ambayo imeziba kwa
asilimia 100 na kushindwa kupitisha damu na valvu ambazo zimeziba hazipitishi
damu vizuri tumefanya matibabu kwa
wagonjwa 19 ambao hali zao zinaendelea vizuri, kuna ambao wapo wodini na wengine wamesharuhusiwa kurudi nyumbani”,.
“Moja ya sababu ya valvu za moyo kuziba kwa kiasi kikubwa na
kushindwa kupitisha damu vizuri ni pamoja na kupata ugonjwa wa mafindofindo na homa kali ambayo hupelekea
kuharibu valvu na kuzisababishia kushikamana na kushindwa kupitisha damu,
wagonjwa wa aina hii huwa tunawafanyia upasuaji mkubwa wa kufungua kifua lakini
katika kambi wamefanyiwa upasuaji mdogo na kuzibuliwa valvu zilizoziba”,
alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge aliongeza kuwa wagonjwa ambao valvu zao zilikuwa
zimeziba kama wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu mgonjwa mmoja
ingemgharimu kulipia gharama ya matibabu zaidi ya shilingi milioni 20 lakini
kwa kupata matibabu hayo hapa nchini mgonjwa amelipia shilingi milioni sita fedha
ambazo kwa wengi wao zimellipwa na bima
za afya wanazozitumia na pia mgonjwa anapata
nafasi ya kuwa karibu na familia yake kipindi chote anachopatiwa matibabu.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka
Shirika la Madaktari Afrika Mazen Albaghdadi alisema mara nyingi wamekuwa
wakifanya kambi za matibabu ya moyo ambapo kambi hizo zimekuwa zikienda
sambamba na utoaji wa mafunzo kwa wataalamu waliopo JKCI pia wamekuwa wakibadilishana ujuzi wa kazi jambo
ambalo limeifanya JKCI kuweza kutoa huduma za kisasa na za kibingwa kwa
wagonjwa.
“Tunapenda kuja JKCI mara kwa mara kubadilishana ujuzi na madaktari
hawa kwani wamekuwa wakihamasika kujifunza vitu vipya kila wakati na kuvifanyia
kazi, na kuyafanya matibabu ya moyo kuwa
ya kibingwa hapa Tanzania”, alisema Dkt. Mazen.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Khuzeima Khanbai alisema Madaktari kutoka Shirika la Madaktari
Afrika wapo kwa ajili ya kuwaongezea ujuzi wa kazi wataalamu wa JKCI ili waweze kupata mbinu mpya za kutoa huduma
kwa kutumia njia za kisasa kwa wagonjwa wenye matatizo ya mishipa ya damu ya moyo
iliyoziba kwa kiwango kikubwa na wale
wenye matatizo ya valvu za moyo zilizoziba.
“Ujuzi tulioupata katika kambi hii umetuwezesha kutumia njia
maalum ambazo zimeweza kutufikisha katika moyo kupitia tundu dogo linalotobolewa
kwenye paja na kuweza kuzibua mishipa ya damu pamoja na Valvu zilizoziba.
Mafunzo tunayoyapata katika kambi hii tutaendelea kuyafanyia kazi”, alisema
Dkt. Khuzeima .
Nao wagonjwa waliopata huduma ya matibabu katika kambi hiyo
walishukuru kwa huduma waliyoipata na kuipongeza Serikali kwa kujenga Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete, kuhakikisha inavifaa tiba vya kisasa na kuwasomesha wataalamu
wa magonjwa ya moyo.
Christopher Taji mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam alisema
alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo lililomfanya kushindwa kulala usingizi
mzuri kwa muda mrefu kutokana na maumivu makali aliyokuwa anayapata katika eneo la kifua.
“Nilipofika JKCI madaktari walinifanyia vipimo na kugundua mishipa
ya damu kwenye moyo wangu imeziba hivyo kunishauri nifanyiwe upasuaji wa
kuzibua mishipa hiyo na sasa nimeshafanyiwa upasuaji ambao madaktari wamekiri
kuwa umefanyika kwa mafanikio makubwa”,.
“Sasa nalaa vizuri bila kusikia maumivu yoyote, madaktari
wangu wamefanya kazi kubwa sana, nawashukuru kwa kujitoa kwao kwa ajili yangu.
Wito wangu kwa jamii pale wanapopata changamoto yoyote ya kiafya wafike katika
hospitali zetu kwani huduma za kibingwa zinapatikana”, alisema Christopher
Ally Mahamud mkazi wa Mombasa jijini Dar es Salaam alisema alikuwa na tatizo
la kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo kwa muda mrefu baada
ya kuzibuliwa kumeondoa kabisa maumivu
makali aliyokuwa akiyapata kabla ya kufanyiwa upasuaji huo.
Sitaacha kuwashukuru madaktari waliookoa maisha yangu tena
kwa dharura kwani nililetwa hapa kwa dharura nikiwa na hali mbali na maumivu
makali lakini leo nipo hapa naongea kwa furaha nikiwa sina maumivu yoyote,
Mungu awabariki kwa kazi hizi ngumu wanazofanya madaktari na wauguzi za kuokoa
maisha yetu”, alisema Mahamud.
Katika kambi hiyo maalum ya matibabu wataalamu hao mabingwa
wa magonjwa ya moyo na wazibuajji wa mishipa ya damu ya moyo wanatarajia
kufanya upasuaji kwa wagonjwa 19 wenye matatizo ya mishipa ya damu ya moyo
iliyoziba kwa asilimia 100 na wagonjwa 6 wenye matatizo ya valvu za moyo ambazo
zimeziba na hazipitishi damu vizuri.
Comments
Post a Comment