Wagonjwa 20 wafanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi maalum ya matibabu iliyofanywa na madaktari wa JKCI na mwenzao kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na mwenzao kutoka
Hospitali ya Max ya nchini India Dkt. Subhash Sinha wakimbadilisha mshipa
mkubwa wa moyo (Aorta) mgonjwa ambaye mshipa
wake uliokua umetanuka zaidi ya sentimita 5 wakati wa kambi maalum ya matibabu ya moyo ya
siku saba iliyofanyika katika Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam. Jumla ya
wagonjwa 20 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo
Wataalam wa Afya kutoka Idara ya Upasuaji mkubwa wa Moyo wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja na Daktari
bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka hospitali ya Max iliyopo
nchini India Subhash Sinha baada ya kumalizika kwa kambi maalum ya matibabu ya
moyo ya siku saba iliyofanyika katika Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
*********************************************************************************************
Wagonjwa 20 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua
kifua katika kambi maalum iliyofanywa na madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na
mishipa ya damu kutoka hospitali ya Max iliyopo nchini India na kumalizika jana
Jijini Dar es Salaam.
Kambi hii maalum ya matibabu ya moyo iliyoanza tarehe 18 hadi
25 Aprili 2022 imefanyika kwa wagonjwa ambao mioyo yao ilikua imechoka na
kiwango cha ufanyaji kazi wa moyo umeshuka chini ya asilimia 35%.
Akizungumzia kambi hiyo Mkurugenzi Idara ya Upasuaji JKCI
Dkt. Angela Muhozya amesema kuwa wagonjwa 7 (saba) wamefanyiwa upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa moyo (Aorta) uliokuwa umetanuka zaidi ya sentimita
5 (5cm)na hivyo kuwa katika hatari ya kupasuka wakati wowote na mgonjwa
kupoteza Maisha.
““Upasuaji huu hufanyika kwa kuondoa sehemu iliyotanuka na
kupandikiza kipande cha mshipa wa bandia (graft) inayoendana na ukubwa wa
mshipa wa moyo wa mgonjwa (ascending aorta replacement) ambapo wagonjwa wote
wanaendelea na matibabu na afya zao zinazidi kuimarika”, alisema Dkt. Angela
Aidha Dkt. Angela amesema kuwa pamoja na wagonjwa hao saba waliobadlilishiwa
mishipa mkubwa wa moyo, wagonjwa wengine 13 wamepandikizwa mishipa iliyokuwa
imeziba katika moyo (bypass) isiyopungua miwili.
“Wagonjwa tuliowapandiza mishipa niwale ambao walikuwa na
mishipa zaidi ya miwili iliyoziba lakini
pia kiwango cha ufanyaji kazi wa mioyo yao
kilikuwa kimeshuka sana”,
“Tofauti ya mishipa hii tunayopandikiza na ile amboyo
tumekuwa tukipandikiza siku zote ni kuwa wagonjwa wengi waliofanyiwa katika kambi
hii wana kiwango kidogo cha ufanyaji kazi wa moyo yaani chini ya 35 (ejection
fraction)” alisema Dkt. Angela
“Kama Taasisi tumeshaanza kidogo kidogo kufanya upasuaji wa
kupandikiza mishipa kwa wagonjwa lakini tunapokutana na wagonjwa ambao mioyo
yao imechoka sana tunahitaji utaalam zaidi wa kufanya upasuaji bila
kuusimamisha moyo na ndio maana tumekuwa na kambi hii kwa ajili ya kupata
mafunzo zaidi na kutoa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji upasuaji wa kupandikiza
mishipa.
“Naamini baada ya kambi hii madaktari wazawa wataweza kufanya
upasuaji huu kwa wagonjwa ambao mioyo yao ina kiwango kidogo cha kufanya kazi
chini ya 35 kwani hapo awali tulilazimika kuwafanyia kwa kusimamisha moyo au kuwatuma
wagonjwa hao nje ya nchi” alisema Dkt. Angela
Kwa upande wake Daktari kutoka Hospitali ya Max iliyopo
nchini India Subhash Sinha amesema kuwa hii ni mara yake ya tatu kufika na kushirikiana
na madaktari wa JKCI kwa sababu maalum za kusaidia kuwafanyia upasuaji wagonjwa
ambao mioyo yao inafanya kazi kwa kiwango kidogo yaani chini ya 35.
“Kila ninapokuja tumekua tukifanya upasuaji kwa wagonjwa kati
ya 20 hadi 25 na wakati huu tumeweza kuwafanyia upasuaji wagonjwa 20 ambao
walikua katika hali mbali kutokana na mioyo yao kufanya kazi kwa kiwango cha chini”,
“Idara ya upasuaji ya JKCI inakua kwa kasi katika kutoa
huduma za upasuaji, Madaktari wanajituma sana katika kutekeleza majukumu yao ya
kila siku na wamekua wepesi kupokea mbinu mpya tunazotumia katika upasuaji kila
ninapokuja”, alisema Dkt. Sinha
Naye Mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji mkubwa wa kufungua kifua
katika kambi hiyo Abdalla Bakari Mkazi wa Dar es Salaam ameishukuru serikali ya
awamu ya nne ya Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwa na wazo la kanzisha Taasisi
ya Moyo hapa nchini ili kuweza kuwahudumia watanzania ambao wengi wao hawana
uwezo wa kufuata matibabu ya moyo nje ya nchi.
“Nashindwa kuongea na haya machozi ninayoyatoa ni ya furaha
baada ya kuona tatizo langu la mishipa ya damu iliyokua imeziba na kunipa
changamoto za kuchoka mara kwa mara na kukosa pumzi wakati nikiwa naongea sasa
limetatuliwa, Nawashukuru sana wataalam hawa waliojitoa kuokoa maisha yetu”,
“Uwepo wa Taasisi hii umeweza kuwasaidia watu wa maisha ya
chini kupata huduma za matibabu ya moyo kupitia bima ya afya mimi nikiwa mmoja
wao, naipongeza serikali ya awamu ya nne ya Mhe. Kikwete kwa kuanzisha Taasisi
hii na serikali za awamu ya tano na sita kuendelea kuipa kipaumbele Taasisi hii
ili sisi watu wakawaidi tuweze kupata huduma za kibingwa hapa nchini”, alisema
Bakari.
Comments
Post a Comment