JKCI: Wanaotaka kusaidia matibabu waje kuwatambua wagonjwa
Mwenyekiti wa Mfuko wa Hisani wa Kujitolea, Kuongoza na
Kubadilisha Beatus Rwechungura akimkabidhi risiti ya malipo ya Tshs.2,655,000/=
Edna Michael leo jijini Dar es Salaam
kwa ajili ya gharama za upasuaji wa moyo wa mtoto wake anayesubiri kufanyiwa
upasuaji katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwaeleza wadau kutoka Mfuko wa Hisani wa
Kujitolea, Kuongoza na Kubadilisha kuhusu magonjwa ya moyo kwa watoto walipotembelea
Taasisi hiyo leo kwa ajili ya kukabidhi
risiti za malipo ya Tshs.8,750,000/= ikiwa
ni gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto watatu. Kulia ni Ramadhani Iddi
ambaye mtoto wake amelipiwa
Tshs.2,895,000/= kwa ajili ya upasuaji wa moyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na wadau kutoka Mfuko wa Hisani wa Kujitolea, Kuongoza na Kubadilisha waliofika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kukabidhi risiti za malipo ya Tshs.8,750,000/= ikiwa ni gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto watatu.
*********************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Wananchi wanaohitaji kulipia gharama za matibabu ya wagonjwa wa moyo wameshauriwa kufika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuwatambua wagonjwa ambao hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu pia kufahamu gharama halisi za matibabu yao.
Ushauri huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea na wadau kutoka Mfuko
wa Hisani wa Kujitolea, Kuongoza na Kubadilisha waliofika JKCI kwa ajili ya kukabidhi risiti za malipo ya gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto
watatu.
Prof. Janabi alisema wananchi wanaotaka kulipia gharama za matibabu ya wagonjwa wa moyo wafike katika
Taasisi hiyo au wapige simu, wataoneshwa njia sahihi ya kufanya malipo
ikiwa ni pamoja kupewa gharama halisi ya
matibabu na kuoneshwa wagonjwa
wanaohitaji msaada wa matibabu.
“Siku hizi tumekuwa tukiona katika mitandao ya kijamii watu
mbalimbali wakichangisha fedha za matibabu ya wagonjwa. Kwa upande wa wagonjwa
wa moyo ninawaomba wananchi wanaotaka kusaidia wagonjwa wafike katika Taasisi
yetu , wataoneshwa wagonjwa husika na kupewa taratibu za kufanya malipo hii itawasaidia
kuepuka kutapeliwa”,.
“Ninawashukuru sana ndugu zetu hawa leo hii wamelipa Tshs.8,750,000/=
kwa ajili ya gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto watatu ambao walezi wao
hawana uwezo wa kulipia matibabu yao. Tumewaonesha watoto hao kabla ya
kufanyiwa upasuaji na watakuja tena kuwaona baada ya kufanyiwa upasuaji.
Wamechukuwa namba za simu za walezi wao ambao watawasiliana nao ili kujua maendeleo
ya watoto”, alisema Prof. Janabi.
Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo aliisistiza jamii kuwa na tabia ya kuchangia gharama za
matibabu kwa wagonjwa ambao hawana uwezo kwani Serikali peke yake haiwezi kwa
kuwa gharama za matibabu ni kubwa kuna vifaa ambavyo vinatakiwa kununuliwa na
vinapatikana nje ya nchi.
Kwa upande wake Beatus Rwechungura ambaye ni Mwenyekiti wa Mfuko
wa Hisani wa Kujitolea, Kuongoza na Kubadilisha alisema kikundi chao kina watu
sita ambao ni marafiki wa siku nyingi huwa wanatoa michango ya mara kwa mara kwa
ajili ya kusaidia jamii inayowazunguka.
“Tulichangishana tukapata kiasi cha Tshs.8,750,000/= fedha ambazo
tumelipia gharama za matibabu ya upasuaji wa moyo kwa watoto watatu na tuliamua
kusaidia watoto kwasababu wanauhitaji na
tunatengeneza maisha yao ya baadaye”, alisema Rwechungura.
Rwechungura alisema wamefika katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete na kutembelea wodini wameona kuna uhitaji mkubwa, waliomba watu wenye
uwezo wa kuchangia wasaidie chochote watakachoweza kitasaidia na kuwa na
matokeo mazuri katika maisha ya watoto.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Asha
Salum alishukuru kwa wageni waliowapata ambao wamewasaidia watoto wenye
matatizo mbalimbali kwa kuwalipia gharama za matibabu ya moyo.
Asha alisema uhitaji ni mkubwa kuna watoto wanaofika kutibiwa
katika Taasisi hiyo na hawana bima za afya na kuna ambao wanabima lakini gharama
za matibabu ni kubwa na wazazi hawana uwezo wa kulipia. Hivyo basi wanalazimika
kuomba msaada kwa wadau mbalibali ikiwa ni pamoja na Taasisi kulipia gharama
hizo.
“Watoto hawa pia wanamahitaji mengine ya muhimu kama vile diapers,
sabuni, dawa za meno, miswaki na vitu
vya kuchezea ninaomba watu mbalimbali ambao wataguswa waweze kuwasaidia”, alisisitiza
Asha.
Nao wazazi ambao watoto wao wamelipiwa gharama za matibabu
walishukuru kwa moyo wa upendo ulioonesha na wasamaria wema hao na kuwaomba
wananchi wengine waweze kuwasaidia watoto wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa
moyo ambao wazazi wao hawana uwezo wa kulipia gharama hizo.
Comments
Post a Comment