Kwa mara ya kwanza wataalamu wazawa wazibua mishipa pacha ya moyo iliyoziba kwa asilimia 95
Kwa mara ya kwanza wataalamu wazawa wa magonjwa ya
moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) wamezibua mishipa miwili iliyokuwa inapeleka damu kwa wakati mmoja
kwenye moyo (mishipa pacha ya damu – bifurcation lesion) ambayo ilikuwa imeziba
kwa asilimia 95 na kupata shida ya kupitisha damu.
Uzibuaji wa mishipa
hiyo ulifanyika kwa njia ya upasuaji wa moyo kwa kutumia tundu dogo (Minimum
Invasive Surgery) bila kufungua kifua kwa kutoboa mshipa kwenye paja (Percutaneous
Coronary Angioplasty) kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization
Laboratory) ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalum kwa ajili ya uchunguzi
na tiba za magonjwa ya moyo.
Hayo yamesemwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na daktari mbobezi wa magonjwa ya moyo Tulizo Shemu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati akiongea na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kumaliza kufanya upasuaji huo uliochukuwa masaa mawili na nusu na kuhusisha jopo la madaktari wabobezi watatu.
Dkt.Shemu alisema uzibuajia wa mishipa miwili pacha ambayo imeziba kwa wakati mmoja walikuwa wanafanya kabla ya Dunia kukumbwa na janga la UVIKO-19 kwa kushirikiana na wataalamu wenzao kutoka nje ya nchi ambao walikuwa wanafika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu na mafunzo lakini sasa hivi wataalamu wazawa wameweza kufanya wenyewe upasuaji wa aina hiyo.
Alisema mishipa ya damu ya moyo inaziba kutokana na kuwepo kwa mafuta mengi
katika mishipa (cholesterol) hiyo ambayo inapatikana kwa kula kiasi kikubwa
cha vyakula vyenye wanga, sukari na vyenye mafuta mengi kwani katika mwili wa
binadamu mafuta yanahifadhiwa sehemu
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye ini, figo, moyo na mishipa ya damu.
Dkt. Shemu alisema magonjwa ya mishipa ya damu ya moyo
yamekuwa yakisababisha vifo vya ghafla na kiharusi na kuwataka watu
wanapojisikia moyo kuuma, mwili kuchoka baada ya kufanya kazi kidogo au
kutembea umbali mfupi kuwahi hospitali mapema kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi
ili kama watakutwa na matatizo ya moyo waweze kupata matibabu mapema na kwa
wakati wakikaa nyumbani shida zitaongezeka zaidi pamoja na kupoteza maisha.
“Sasa hivi magonjwa ya mishipa ya damu ya moyo yanasababisha vifo vya watu wengi ni muhimu kubadili
mtindo wa maisha kwa kula chakula bora, kufanya mazoezi, kunywa pombe kwa
kiasi, kuacha kuvuta sigara na kupunguza msongo wa mawazo wanaokutana nao katika maisha
kwa kufanya hivyo unaweza kuepuka kupata magonjwa haya”, alisisitiza Dkt. Shemu.
Kwa upande wake Mama Sada Haji kutoka Zanzibr ambaye
alizibuliwa mishipa hiyo ya damu alishukuru kwa huduma aliyoipata na kusema alikuwa
anapata maumivu makali eneo la kifuani upande wa kushoto, akibeba mizigo mdogo anakosa nguvu
pia anatoka jasho jingi.
“Baada ya kujisikia maumivu nilipelekwa Hospitali ya kwanza
na kuandikiwa dawa za kutumia nilizitumia dawa hizo kwa muda wa miaka nane
lakini tatizo likawa linaendelea. Watoto wangu walinipeleka Hospitali nyingine na kufanyiwa vipimo na
kugundulika kuwa na tatizo kwenye moyo daktari akanituma kuja kutibiwa hapa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete. Baada ya kufika hapa na kufanyiwa vipimo siku
ya Alhamisi iliyopita niliambiwa mishipa miwili ya damu ilikuwa imeziba na
inatakiwa kuzibuliwa”,.
“Siku ya Jumatatu tarehe 4/04/2022 nilifanyiwa upasuaji wa
kuzibuliwa mishipa hiyo baada ya kufanyiwa upasuaji huo sasa hivi najisikia
vizuri, maumivu hakuna tena kama ilivyokuwa awali, ninakula chakula vizuri na
daktari ameniambia nitaruhusiwa kurudi nyumbani siku chache zijazo”, alisema
Mama Sada.
Mama Sada aliwashauri watu wenye matatizo kama yake wasikate
tamaa wakisikia maumivu waende Hospitali wakafanyiwe uchunguzi kwani vifaa vipo
na wataalamu wapo wanaotoa huduma za kuzibua mishipa ya damu ya moyo.
Im so proud of you🇹🇿
ReplyDelete