Watu 10 wafanyiwa upasuaji wa moyo kutumia tundu dogo (Minimum Invasive Surgery) katika kambi maalum ya matibabu iliyofanyika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
Wataalam wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na mwenzao kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India Dkt.
Viveka Kumar wakimfanyia mtoto upasuaji wa kumbadilishia betri ya moyo iliyoisha
muda wake kwa kutumia tundu dogo (Minimum Invasive Surgery) katika kambi maalum
ya siku nne iliyomalizika leo katika Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam. Jumla
ya wagonjwa 10 wenye matatizo ya hitilafu ya mfumo wa moyo na wale ambao mioyo
yao imeshindwa kufanya kazi (Heart failure) wamefanyiwa upasuaji mdogo wa moyo
katika kambi hiyo.
Wataalam wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kwa
kushirikiana na mwenzao kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India Dkt.
Viveka Kumar wakiusoma mfumo wa umeme wa moyo wa mgonjwa ambaye ana hitilafu ya
mfumo wa umeme wa moyo wakati wa upasuaji mdogo wa moyo kwa kutumia tundu dogo (Minimum
Invasive Surgery) katika kambi maalum ya siku nne iliyomalizika leo katika
Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
****************************************************************************************************
Wagonjwa 6 wenye hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo na
wagonjwa wanne ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi (Heart failure)
wamefanyiwa upasuaji mdogo wa moyo kwa kutumia tundu dogo (Minimum Invasive
Surgery) katika kambi maalum ya matibabu ya siku nne iliyofanywa na madaktari
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka
Hospitali ya Max iliyopo nchini India.
Akizungumzia kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na
mfumo wa umeme wa moyo wa JKCI Yona Gandye amesema kuwa lengo kubwa la kambi
hiyo ni kubadilishana uzoefu na kutoa elimu kwa madaktari ambao wapo masomoni
hivo kuendeleza gurudumu la kuzalisha madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo.
“Tumekuwa tukishirikiana na madaktari kutoka maeneo
mbalimbali hivyo kutusaidia kuwa na mahusiano mazuri na hospitali nyingi
duniani, lakini pia kutoa fursa kwa hospitali hizo kuruhusu wataalam wetu
kwenda kujifunza kwao na kuzalisha madaktari wabobezi wengi zaidi”, alisema
Dkt. Gandye
Dkt. Gandye amesema kuwa katika kambi hiyo wameweza kuwapatia
matibabu wagonjwa wenye hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo na wagonjwa ambao
mioyo yao imeshindwa kufanya kazi (heart failure) ambao walihitaji matibabu ya
kina.
“Dalili za wagonjwa wenye hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo
ni pamoja na mapigo ya mioyo yao kwenda haraka sana, na wakati mwingine
kupoteza fahamua. Tunapojiridhisha kuwa wagonjwa wana hitilafu ya mfumo wa
umeme wa moyo uangalia ni aina gani ya matibabu inawafaa kwa wakati huo, kwani
wapo tunaowaanzishia dawa na kuangalia muenendo wa mfumo wa umeme wa moyo na
wengine uhitaji upasuaji mdogo wa moyo kurekebisha ile sehemu inayozalisha
mapigo ya umeme yanayoleta athari kwa mgonjwa”, alisema Dkt. Gandye
Aidha Dkt. Gandye amesema kuwa katika kambi hiyo pia wameweza
kuwatibu wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi (heart failure) ambao
mara nyingi wagonjwa hao mioyo yao hutanuka hivyo kupelekea hitilafu ya mfumo
wa umeme wa moyo yaani pande zote mbili za moyo kushindwa kufanya kazi kwa
kushirikiana.
“Katika matibabu ya wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa
kufanya kazi (heart failure) tunarekebisha mfumo wa umeme wa moyo ambao una
hitilafu kiasi kwamba mgawanyo wa umeme upande wa kushoto na kulia utokea kwa
wakati mmoja hivyo kuuwezesha moyo kusukuma damu pande zote za kushoto na kulia
kwa wakati mmoja”,
“Wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi vizuri mara
nyingi hupata changamoto za pumzi kubana, kuchoka sana na wengine ukutana na
changamoto ya kusikia kukabwa wakati wa usiku kutokana na pumzi kubana
inayosababishwa na athari iliyopo katika moyo”, alisema Dkt. Gandye
Sambamba na hilo Dkt. Gandye ameishukuru serikali kwa
kuwezesha vifaa vya matibabu vilivyopo JKCI, kuweka mazingira rafiki
yanayoruhusu wataalam wa afya kutoka sehemu mbalimbali kuingia nchini kwa ajili
ya kushirikiana nao katika kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo hivyo
kupunguza idadi ya wagonjwa wengi waliokuwa wanaenda nje ya nchi kwa ajili ya
matibabu ya moyo
“Wito wangu kwa watanzania, wasiwe na mazoea ya kwenda
hospitali wanapoumwa tu kwani magonjwa ya moyo yaliyo mengi hadi ifikie hatua
unaona dalili tatizo linaweza likawa limeshasababisha uharibufu mkubwa katika
moyo, hivyo tuwe wepesi kuchunguza afya na kubaini matatizo mapema ili tuweze
kuyadhibiti na kupunguza madhara yanayotokana na magonjwa ya moyo”, alisema
Dkt. Gandye
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka
Hospitali ya Max iliyopo nchini India Viveka Kumar amesema kuwa madaktari
kutoka Hospitali ya Max wamekuwa wakishirikiana na madaktari wa JKCI kutokana
na Taasisi hiyo (JKCI) kuwa moja ya vituo vichache katika bara la Afrika
inayotoa huduma bora na za kibingwa za magonjwa ya moyo.
“Tunafurahi kuwa sehemu ya taasisi hii, kutokana na huduma za
bingingwa zinazotolewa hapa na kuifanya taasisi hii kuwa hospitali ya kibingwa
ya magonjwa ya moyo”,
“Ni mara yangu ya kwanza kufika Tanzania na najivunia kuwa
hapa, uwepo wangu hapa ni sehemu ya kulipa fadhila kwa watanzania ambao
wamekuwa wakarimu kwa ndugu zangu kutoka India ambao waliishi Tanzania”,
alisema Dkt. Kumar
Aidha Dkt. Kumar alisema kuwa hapo awali India ilipokea
wagonjwa wengi wenye matatizo ya moyo kutoka Tanzania lakini sasa wagonjwa hao
wamepungua kutokana na uwepo wa hospitali za kibingwa hapa nchini.
“Sasa naelewa kwanini wagonjwa wa moyo kutoka Tanzania wamepungua
nchini India, Taasisi hii ina kila sababu ya kupunguza wagonjwa kwenda india
kutibiwa kwani ina vifaa vya kutosha na huduma za kibingwa, huduma za uangalizi
maalum ni za kisasa kutokana na mashine zilizopo na madhari ya vyumba vya
wagonjwa kuwa nzuri hivyo kuwapunguzia watanzania gharama za kwenda nje ya nchi
kutibiwa”, alisema Dkt. Kumar
Comments
Post a Comment