Wataalamu wa
usingizi na wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a
Child’s Heart – SACH) la nchini Israel wakimlaza mtoto kabla ya kufanyiwa upasuaji wa kuzibua
mshipa wa damu wa moyo kwa kutumia tundu dogo (Minimum Invasive Surgery) katika kambi maalum ya siku tano ya matibabu
ya moyo iliyomalizika leo jijini Dar es Salaam. Katika kambi hiyo watoto 40
wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo walifanyiwa uchunguzi ambapo 21 kati
yao walifanyiwa upasuaji wa kuziba matundu na kuzibuliwa mishipa ya damu ya
moyo.


Wataalamu
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s
Heart – SACH) la nchini Israel wakimfanyia mtoto upasuaji wa kuziba tundu
kwenye moyo kwa kutumia tundu dogo (Minimum Invasive Surgery) katika kambi maalum ya siku tano ya matibabu
ya moyo iliyomalizika leo jijini Dar es Salaam. Katika kambi hiyo watoto 40
wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo walifanyiwa uchunguzi ambapo 21 kati
yao walifanyiwa upasuaji wa kuziba matundu na kuzibuliwa mishipa ya damu ya
moyo.
Na: JKCI
***************************************************************************************************************************
Watoto 40 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa
nayo wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa hayo ambapo 21 kati yao
wamefanyiwa upasuaji wa moyo kwa kutumia tundu dogo (Minimum Invasive Surgery) katika
kambi maalum ya matibabu ya moyo iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart –
SACH) la nchini Israel.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Daktari
bingwa wa magonjwa ya moyo ya watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya kIkwete (JKCI)
Stella Mongella ambaye pia ni mratibu wa kambi hiyo ya matibabu ya siku tano iliyoanza
tarehe 28/3/2022 na kumalizika tarehe 1/4/2022.
Dkt. Stela alisema watoto waliofanyiwa
uchunguzi na waliotibiwa ni wale wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo
ni mishipa ya damu ya moyo na matundu kwenye
moyo. Hali za wagonjwa zinaendelea vizuri na kuna ambao tayari wamesharuhusiwa
kurudi nyumbani na wengine wataruhusiwa wakati wowote kuanzia sasa.
Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya moyo ya
watoto alisema uchunguzi huo pamoja na tiba ulifanyika kwa njia ya upasuaji wa
bila kufungua kifua kwa kupasua sehemu ndogo kwenye paja kwa kutumia mtambo wa
Cathlab (Catheterization Laboratory) ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalum
kwa ajili ya uchunguzi wa matatizo na tiba za magonjwa ya moyo.
“Faida za upasuaji wa aina hii ni mtoto anakaa wodini siku chache kwani baada saa
moja baada ya upasuaji anaweza kula
chakula na baada ya siku moja anaruhusiwa
kurudi nyumbani, vifaa vinavyotumika kuziba matundu ni vya kisasa na ni salama
kwa ukuaji wa mtoto. Pia watoto wanaofanyiwa upasuaji wa aina hii hawahitaji
kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kufungua kifua”,
alisema Dkt. Stela.
Dkt. Stela alisema watoto ambao walifanyiwa
uchunguzi na hawakufanyiwa upasuaji ni wale ambao walikuwa na uzito mdogo pia
kutokana na umri wao kuwa mdogo waliachwa ili matundu hayo yaweze kujiziba yenyewe
kwani kuna matundu ambayo yanaweza kuziba kabla ya mtoto kufikia umri wa miaka
mitano.
“Katika kambi hii tulimfanyia upasuaji mtoto
aliyekuwa na umri wa miezi minne ambaye alikuja kama dharula kutokana na mshipa
wake unaotoa damu kwenye moyo kupeleka kwenye mapafu kuziba kabisa kwa asilimi 100 na
hivyo kuhitaji matibabu ya dharula”,.
“Wakati tunamfanyia upasuaji tulikutana na
changamoto ya mapigo ya moyo kwenda haraka sana na wakati mwingine kuwa chini tunamshukuru
Mungu tulimfanyia upasuaji salama hivi sasa anaendelea vizuri na ananyonya vizuri”,alisema
Dkt. Stela.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya
moyo kwa watoto kutoka hospitali ya Wolfson iliyopo nchini Israel Assa Sagi alisema
katika kambi hiyo licha ya kufanya matibabu kwa watoto pia walitoa mafunzo kwa
wataalamu wa JKCI ambao wanafanya upasuaji huo wa kuzibua mishipa ya damu na
kuziba matundu ya moyo kwa watoto.
“Ninawashauri wazazi wakiona mtoto haongezeki
uzito, anapumua kwa shida midomo yake na vidole
imebadilika rangi na kuwa rangi
ya bluu wasichelewe, wampeleke hospitali mapema ili akafanyiwe vipimo na kupata
matibabu kwani wakichelewa mtoto anaweza kushindwa kutibiwa”, alisisitiza Dkt.
Sagi.
Naye Simon Fisher ambaye ni Mkurugenzi Mtedaji
wa Shirika hilo la SACH alisema tangu mwaka 1999 walianza kuja nchini kutoa
huduma ya matibabu ya moyo kwa watoto lakini kutokana na janga la UVIKO - 19 lililoikumba Dunia mwaka 2020 hawakuweza kuja,
lakini sasa hivi wamekuja na kukuta badadiliko
makubwa ya vifaa tiba vilivyopo JKCI hii ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa mtambo
mpya wa kisasa wa Cathlab na mtambo wa Carto 3 System
3D & Conventional System.
“Nimefurahi kuona mashine ya Intra-Aortic
balloon pump kwani kuwepo kwa kifaa hiki
kinachotumika kwa ajili ya wagonjwa ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo
lakini mioyo yao ufanyaji wake wa kazi uko katika kiwango cha chini hivyo basi anawekewa kifaa hiki ili kuusaidia moyo
kufanya kazi kabla na wakati wa upasuaji kutawasaidia wataalamu kufanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa
na wagonjwa kupata huduma ya matibabu kwa wakati”, alisema Fisher.
Fisher alisema Shirika hilo litaendelea kutoa
vifaa tiba pamoja na wataalamu ambao watakuja nchini kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu
ya moyo kwa watoto pia kwa kushirikiana na wataalamu waliopo JKCI wanatarajia
kwenda kutoa huduma ya matibabu ya moyo na mafunzo katika Hospitali ya moyo
iliyopo nchini Zambia.
Nao wazazi ambao watoto wao walitibiwa katika
kambi hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa baada ya watoto
hao kufanyiwa upasuaji wameona mabadiliko kwa watoto hii ikiwa ni pamoja na kuhema vizuri, kucheza
vizuri na kula chakula vizuri tofauti na ilivyokuwa kabla hawajapata matibabu .
Loveness Ngowi alisema mwaka 2020 mtoto wake akiwa na umri wa mwaka mmoja na
miezi miwili aligundulika kuwa na tatizo
la ugonjwa wa moyo baada ya kuona mtoto anahema vibaya na anapata tatizo la ugojwa
wa nimonia mara kwa mara alimpeleka hospitali na kufanyiwa vipimo ambavyo
vilionesha ana tundu kwenye moyo.
“Baada ya kufanyiwa upasuaji na kuzibwa tundu lililokuwepo kwenye moyo
mtoto anacheza vizuri, anakula na anahema vizuri tofauti na ilivyokuwa kabla ya
kupata huduma hii. Ninawashauri wanawake wenzangu wakiona mtoto hakui vizuri,
anashindwa kuhema na anachoka haraka wakati anacheza wwampeleke hospitali mapema
ili aweze kupata matibabu”, alisema Loveness.
Mama Tatu Mbaruku ambaye mjukuu wake alifanyiwa
upasuaji wa kuziba tundu la moyo anasema mtoto alipokuwa na umri wa miaka
miwili alikuwa na tatizo la kukohoa , maumivu kwenye mbavu na kuchoka baada ya kufanyiwa vipimo aligundulika
kuwa na shida ya matundu mawili kwenye moyo na kuandikiwa dawa za kutumia.
“Baada ya kuanza kutumia dawa hali ya mtoto
ilibadilika na kuendelea vizuri. Alifanyiwa tena vipimo ambavyo vilionesha tundu moja limeziba na kubakia
tundu moja ambalo limezibwa jana baada ya kufanyiwa upasuaji mdogo wa moyo sasa
hivi anaendelea vizuri”, alisema Mama Tatu.
Comments
Post a Comment