JKCI kushiriki maonesho ya kimataifa nchini Comoro
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza kuhusu JKCI kushiriki maonesho ya kimataifa nchini Comoro
*********************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inatarajia kushiriki
maonesho ya bidhaa na huduma zinazozalishwa Tanzania yanatakayofanyika nchini
Comoro kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 20 Desemba mwaka huu.
Katika maonesho hayo Taasisi hiyo itaonesha huduma za
kibingwa za matibabu ya moyo inazozitoa kwa wananchi wa Comoro.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema Taasisi hiyo imeona ni
muhimu kushiriki katika maonesho hayo ili kutangaza huduma za kibingwa za
matibabu ya moyo ambazo zimekuwa zikihitajika na watu kutoka nchini humo.
Dkt. Kisenge alisema
JKCI imeendelea kukuwa kwa kasi na kuwa bora Afrika Mashariki na kati hivyo
kuifanya kuwa moja ya Taasisi kubwa inayotoa matibabu ya moyo na upasuaji wa
moyo nchini Afrika.
“Sisi kama Taasisi tunaendelea kutoa huduma zetu kwa wananchi
hapa Tanzania na sasa tunaenda kutoka nje ya mipaka ya Tanzania kuwafikia wagonjwa
wa moyo katika nchi mbalimbali za Afrika ili nao wafaidike na huduma zetu na
kupunguza gharama za kuwapeleka wagonjwa wao nchi zilizo nje ya bara la Afrika,”
“Sambamba na kushiriki
katika maonesho hayo tumejipanga kwenda nchini Comoro mwezi Februari 2023 kwa
ajili ya kufanya kambi maalum ya matibabu ya moyo ili wananchi wa Comoro waweze
kuona vizuri huduma zetu zilivyo na kutoa nafasi kwa wananchi hao kuchunguza
afya zao,” alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema kwa sasa JKCI inajulikana barani Afrika
kwa kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwani hivi karibuni wanatarajia
kumpokea Katibu Mkuu Wizara ya Afya wa nchini Zambia pamoja na Mkurugenzi wa
Hospitali ya Moyo wan chi hiyo kwa ajili
ya kusaini mkataba wa kushirikiana katika kutoa mafunzo ya huduma zinazotolewa
JKCI.
“Mkataba huo pia utahusisha makubaliano ya JKCI kupokea
baadhi ya wagonjwa kutoka nchini Zambia ambao hapo awali walikuwa wanapelekwa
nchini India ili waweze kupatiwa matibabu ya moyo hapa nchini,” alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema mkakati wa kuvuka mipaka ya Tanzania
unakusudia pia kuzifikia nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na
nchi nyingine barani Afrika ambazo kwa namna moja zitafaidika na huduma za
kibingwa na bobezi za matibabu na upasuaji wa moyo zinazotolewa JKCI.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema Taasisi hiyo imekuwa ikipokea
wagonjwa kutoka nchi za jirani ikiwemo Visiwa vya Comoro hivyo sasa imeona ni
muda muafaka wa wao kwenda na kuzitangaza huduma wanazozitoa katika nchi hizo.
Dkt. Angela ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na
wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum alisema kwa sasa JKCI inatoa huduma zote
za dharura na huduma za matibabu ya moyo kwa masaa 24 ili kuweza kutoa huduma
kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.
Comments
Post a Comment