Watu 429 wafanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo Mkoani Mtwara
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ally
Athuman akimpima wingi wa sukari mwilini mwananchi wa Mkoa wa Mtwara aliyefika
katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini (SZRH) kwa ajili ya kufanyiwa
uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalum ya siku tatu iliyokua
ikifanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa SZRH na kumalizika
jana kwa kuwafanyia uchunguzi na matibabu ya moyo wananchi 429.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari
akiwaelezea namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo wananchi wa Mkoa wa Mtwara
waliofika katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini (SZRH) kwa ajili ya
kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalum ya siku tatu iliyomalizika
jana kwa kuwafanyia uchunguzi na matibabu ya moyo wananchi 429.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nuru Letara akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) mtoto aliyefika katika Hospitali ya
Rufaa Kanda ya Kusini (SZRH) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya
moyo wakati wa kambi maalum ya siku tatu iliyomalizika jana katika Hospitali
hiyo.
Jumla ya watu 429 wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo
katika kambi maalum ya matibabu iliyofanywa na wataalam wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya
Kusini (SZRH)
Kambi hiyo ya matibabu ya moyo iliyofanyika kwa siku tatu
ilianza tarehe 28 hadi 30 Novemba 2022 kwa kutoa huduma za uchunguzi wa
magonjwa ya moyo kwa watu wazima 408 pamoja na watoto 21
Akizungumzia kambi hiyo Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na
Mafunzo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo alisema
upande wa watu wazima ugonjwa wa shinikizo la juu la damu umeonekana kuwa
tatizo kubwa kwani asilimia 51 ya watu wazima waliofanyiwa vipimo wamekutwa na
tatizo hilo.
“Katika asilimia 51 ya watu wazima tuliowakuta na matatizo ya
shinikizo la juu la damu asilimia 23 wamegundulika kwa mara ya kwanza wakati wa
upimaji huu huku asilimia 28 ya waliokutwa na shinikizo la juu la damu walikuwa
wanajitambua lakini tatizo hilo halikua likitibiwa vizuri hivyo wataalam wetu
kuwabadilishia dawa ili presha zao ziwe vizuri”, alisema Dkt. Pedro
Dkt. Pedro alisema ugonjwa wa kutanuka kwa moyo na ugonjwa wa
kuziba kwa mishipa ya damu ni miongoni mwa magonjwa ambayo yalifuatia kuwa na
watu wengi kwa upande wa watu wazima.
“Kwa upande wa watoto jumla ya watoto 21 wamefanyiwa vipimo
vya moyo kati yao watoto 17 wamekutwa na matatizo mbalimbali ya moyo yakiwemo
matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo yaliyogundulika kwa watoto 15”,
“Tumetoa rufaa kwa wagonjwa 73 kufika katika Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete kwa lengo la kufanyiwa matibabu ya juu zaidi ya uchunguzi na
matibabu ya mishipa ya damu na kwa upande wa watoto kufanyiwa upasuaji mkubwa
wa moyo na upasuaji wa kutumia tundu dogo ili kuweza kuziba matundu kwenye
mioyo yao na kurekebisha kasoro ambazo wamezaliwa nazo”, alisema Dkt. Pedro
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda
ya Kusini (SZRH) Dkt. Herber Masigati ameushukuru uongozi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete kwa kuwezesha wataalam mabingwa wa magonjwa ya moyo kufika SZRH kwa
ajili ya kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Mtwara ambao walikua na kiu kubwa ya
kupatiwa uchunguzi na matibabu ya moyo.
Dkt. Masigati alisema hali ya magonjwa ya moyo mkoani Mtwara
inaonekana kuwa kubwa kutokana na kliniki mbalimbali zinazofanywa na Hospitali
hiyo kliniki inayohudumia wagonjwa wengi kuwa ni ile yenye wagonjwa wa
Kisukari, Shinikizo la damu pamoja na magonjwa ya moyo hivyo kupitia kambi hiyo
kutaongeza zaidi idadi ya wagonjwa wa moyo katika kliniki zao.
“Mwitikio wa wananchi kufika katika kambi hii umekuwa mkubwa,
wagonjwa ni wengi wanaohitaji huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo na huu ni
mwanzo wakufikisha huduma za kibingwa kwani hatutaishia hapa bali kila tutakapopata
nafasi tutaendelea kushirikiana”, alisema Dkt. Masigati
Naye mkazi wa Mtwara Pudensiana Sungura alisema amepata
taarifa kupitia vyombo vya habari kuhusu ujio wa madaktari bingwa wa magonjwa
ya moyo hivyo kutokana na hali yake ya kusumbuliwa mara kwa mara na shinikizo
la juu la damu akaona ni vyema kutumia nafasi hiyo ili aweze kufanyiwa
uchunguzi zaidi.
“Nina tatizo la shinikizo la juu la damu, tatizo la sukari na
kuna wakati nasikia moyo wangu ukiuma, nashukuru nimefika hapa nimepata huduma
nzuri za kufanyiwa vipimo kuangaliwa kama moyo wangu hauko vizuri lakini
namshukuru Mungu majibu yametoka vizuri”,
“Wananchi wenzangu nawaomba tukisogezewa huduma karibu
tusizipuuze kama hawa wenzutu wameamua kuacha shughuli zao na kutufuata kwanini
sisi tushindwe kuacha shughuli zetu na kupatiwa matibabu ambayo labda bila wao
kuja huku leo nisingekuwa najua afya ya moyo wangu”, alisema Pudensiana
Comments
Post a Comment