Dkt. Kisenge ahimiza ushirikiano katika kutoa huduma bora
Mkurugenzi
wa Tiba Shirikishi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah
Kimambo akitoa taarifa ya kazi zilizofanywa na Taasisi
hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2022 katika kikao cha wafanyakazi wa JKCI
kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akijibu swali katika kikao cha wafanyakazi wa Taasisi hiyo kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete JKCI wakisikiliza kwa umakini uwasilishwaji wa taarifa ya kazi zilizofanywa na Taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2022 katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
***************************************************************************************************************************************************************
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amehimiza kuimarisha ushirikiano kwa
wafanyakazi wa Taasisi hiyo ili waendelee kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa.
Dkt. Kisenge alitoa rai hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati
wa kikao cha wafanyakazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo.
Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo alisema kila mfanyakazi anatakiwa kufanya kazi kwa bidii na
kujituma katika eneo lake la kazi kwa
kufanya hivyo wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo wataweza kupata huduma
iliyo bora na kwa wakati.
“Licha ya kufanya kazi kwa bidii na weledi tunatakiwa kufanya
kazi kwa ushirikiano kwa maana wafanyakazi wote tunahitajiana na kutegemeana
hivyo basi tuboreshe huduma kwa kutoa huduma bora kwa wateja wetu ili huduma
zetu ziendelee kutanuka zaidi na kujulikana mpaka nchi ya nje,” alisema Dkt.
Kisenge.
Kuhusiana na kuboresha maslahi ya wafanyakazi Dkt. Kisenge alisema menejimenti ya Taasisi
hiyo imekuwa ikijitahidi kuhakikisha wafanyakazi wanalipwa maslahi yao kwa
wakati ili kuwapa motisha ya kufanya kazi zaidi na kuboresha maisha yao.
“Tutaendelea kuboresha hali za wafanyakazi na hapa JKCI kwani
kila mfanyakazi ana umuhimu wake kuanzia mfanyakazi wa chini hadi wa juu wote
hao malipo yao yatazingatiwa, mimi kama Mkurugenzi Mtendaji naahidi
kulifuatilia swala hili kwa umakini wa hali ya juu sana ili kila mfanyakazi
alipwe kwa wakati malipo yake na stahiki,”
alisisitiza Dkt. Kisenge.
Akisoma taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi
cha Januari hadi Novemba 2022 Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi Dkt. Delilah
Kimambo alisema huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wagonjwa zimekuwa
zikiimarika hii ni kutokana na Serikali kununua mashine za kisasa katika Taasisi hiyo pamoja na
wafanyakazi kuwa na ujuzi wa kuweza kuzitumia mashine hizo.
“Wafanyakazi wa JKCI tunapaswa kuwa makini katika kutoa
huduma kwa wateja kwa kufanya hivyo wagonjwa wengi watakuja kutibiwa katika
Taasisi yetu na hivyo kuweza kutimiza mpango mkakati tuliojiwekea wa kutoa
huduma bora za ubingwa bobezi za matibabu ya moyo hapa nchini,”.
“Tutoe huduma nzuri kwa wateja wetu ili waridhirike na huduma
tunazozitoa na pia waendelee kuja kutibiwa katika Taasisi yetu kwa kufanya hivi
tutakuwa tumewasaidia watanzania pamoja na jirani zetu kutoka nje ya Tanzania
wenye matatizo ya moyo kupata huduma za matibabu hapa nchini,”alisema Dkt.
Delilah.
Nao wafanyakazi wa Taasisi hiyo waliishukuru menejimenti ya JKCI kwa kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira yanayoridhisha hii ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi, kuboresha maslahi yao pamoja na kulipia ada za wafanyakazi ambao wanasoma katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi jambo ambalo limewafanya waongeze ujuzi katika taaluma zao.
Comments
Post a Comment