Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA. Agnes Kuhenga akiwasilisha rasimu ya bajeti ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24 wakati wa kikao na viongozi wa JKCI cha kupitia na kujadili bajeti ya Taasisi hiyo ya mwaka wa fedha 2023/24 kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akielezea namna ambavyo JKCI itatekeleza majukumu yake wakati wa kikao cha viongozi wa
Taasisi hiyo cha kupitia na kujadili
rasimu ya bajeti ya JKCI kwa mwaka wa
fedha wa 2023/24 kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Mipango wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Vida Mushi akiwasilisha baadhi ya vifungu vilivyopo
katika bajeti ya Taasisi hiyo wakati wa kikao cha viongozi wa Taasisi hiyo cha kupitia
na kujadili rasimu ya bajeti ya Taasisi ya mwaka wa fedha 2023/24 kilichofanyika
jana jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mawasilisho mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa wakati wa kikao cha viongozi wa Taasisi hiyo kupitia na kujadili rasimu ya bajeti ya Taasisi ya mwaka wa fedha 2023/24 kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi hiyo mara baada ya kumaliza kikao cha kupitia na kujadili rasimu ya bajeti ya Taasisi ya mwaka wa fedha 2023/24 kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
*********************************************************************************************************************************************************************************************************
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) wametakiwa kujiendeleza kielimu ili waweze kutoa huduma bora zinazoendana
na teknolojia za kisasa zinazotumika duniani kwa ajili ya kutoa matibabu kwa
wagonjwa.
Rai hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na viongozi
wa JKCI katika kikao cha kupitia na kujadili rasimu ya bajeti ya Taasisi hiyo
kwa mwaka wa fedha wa 2023/24.
Dkt. Kisenge alisema kutokana na maendeleo na
teknolojia kumekuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya afya jambo ambalo
linawalazimu wafanyakazi wa sekta hiyo kutafuta namna ya kuongeza ujuzi ili
huduma wanazozitoa ziweze kuendana na kasi ya maendeleo duniani.
“Kwenda kuongeza elimu katika fani zetu ni sehemu ya
kuongeza ujuzi katika utendaji wetu wa kazi lakini pia kunatusaidia kubadilisha
mazingira tuliyoyazoea na kutupa motisha ya kujifunza vitu vipya ambavyo katika
mazingira yetu havikuwepo hii yote ikiwa ni kwa maslahi ya huduma tunazozitoa
kwa wagonjwa wetu,” alisema Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt.
Kisenge aliwataka wafanyakazi wa Idara ya Ununuzi na Ugavi kuyatembelea makampuni yanayotengeneza bidhaa zinazotumiwa
na Taasisi hiyo zikiwemo dawa na vifaa tiba ili kupunguza gharama kwa kununua
bidhaa hizo kwa watu ambao nao wanaziagiza kutoka katika makampuni hayo.
“Bajeti hii ya mwaka wa fedha 2023/24 tutaitekeleza
kwa asilimia 100 kama wafanyakazi wa Idara ya Ugavi na Ununuzi wataangalia
namna ya kubana matumizi kwa kuzifikia kampuni zinazozalisha dawa na vifaa tiba
ili kupunguza gharama kubwa tunazotumia kununua bidhaa hizo kwa wadau ambao nao
wanachukua vifaa hivyo katika makampuni mengine,” alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa
Taasisi hiyo CPA. Agnes Kuhenga alisema katika bajeti ya mwaka 2022/23 JKCI
imefanikiwa kuongeza duka la dawa linalohudumia wagonjwa wote wanaohitaji dawa
(Community Pharmacy), pamoja na kupanua eneo la kutakatisha vifaa tiba
(Sterilization unit).
CPA. Agnes alisema kupitia hela ya mradi wa uviko 19
JKCI imeweza kukarabati na kuweka vifaa vya kisasa katika chumba cha wagonjwa
wanaohitaji uangalizi maalum baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo (ICU) pamoja na
chumba maalum cha kuwahudumia wagonjwa wa moyo wanaohitaji uangalizi wa karibu
(Coronary Care Unit - CCU)
“Katika mafanikio tuliyoyapata kupitia huduma
tunazozitoa kwa wagonjwa wetu tulijiwekea kwa mwaka wa fedha 2022/23 tufanye
upasuaji wa tundu dogo kwa wagonjwa 1700 hivyo ukichukua miezi mitano ya Julai
hadi Novemba 2022 tumeshafanya upasuaji huo kwa wagonjwa 889 haya ni mafanikio makubwa
kwetu”,.
“Kwa upande wa upasuaji wa kufungua kifua tulijiwekea malengo ya kufanya upasuaji kwa
wagonjwa 700 ambapo ukigawa kwa miezi 12 kwa kipindi hiki cha miezi mitano
yaani Julai hadi Novemba 2022 tumeshafanya upasuaji kwa wagonjwa 278”, alisema CPA. Agnes.
Naye mkuu wa kitengo cha matibabu ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete Dkt. Sulende Kubhoja alisema kupitia bajeti ya mwaka wa fedha
2023/24 JKCI iangalie namna ya kuongeza vyumba vya wagonjwa wanaohitaji
uangalizi maalum pamoja na vifaa vyake ili itakapotokea janga linalohitaji
huduma za ICU kama lile la UVIKO 19 Taasisi hiyo iweze kupokea wagonjwa hao na
kuwahudumia.
“Wakati wa UVIKO 19 tuliona ambavyo huduma za ICU
pamoja na mashine za kusaidia kupumua (Ventilator) zilivyokuwa zinahitajika kwa
wagonjwa wa hivyo sasa ni wakati wetu kupitia bajeti hii na ili na sisi
tuongeze mashine hizo pamoja na vyumba hivyo ili kama Taasisi ya Umma tuwe
msaada kwa wagonjwa kipindi linapoibuka janga la kitaifa,” alisema Dkt.
Kubhoja.
Comments
Post a Comment