Idadi ya Wagonjwa wa moyo wanaotibiwa nchini India yapungua
Idadi ya wagonjwa wa moyo wanaotibiwa nchini India yapungua
kutokana na uwepo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inayotoa matibabu ya
kibingwa ya magonjwa hayo.
Hali hiyo imejidhihirisha baada ya Taasisi hiyo kupokea
wagonjwa ambao zamani walikuwa wakienda nchini India kwa ajili ya matibabu
mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mgonjwa aliyefanyiwa
upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa
na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na
mwenzao kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India Nahida Mohamed alisema
aliwahi kusumbuliwa na matatizo ya miguu na kwenda nje ya nchi kwa ajili ya
kupatiwa matibabu lakini baada ya kupata matatizo ya moyo familia yake
ilimshauri asiende tena nje ya nchi kwani sasa huduma bora za matibabu
zinapatikana hapa nchini.
Nahida alisema kutokana na huduma zinazotolewa JKCI wagonjwa
wanaoenda nchini India kwa ajili ya matibabu imepungua kwani wataalamu wa JKCI
wanawapa matumaini na faraja wagonjwa jambo ambalo hakuliona alivoenda kutibiwa
nje ya nchi kwa nyakati tofauti kutokana na matatizo ya miguu aliyokuwa nayo.
“Nimeshuhudia huduma nzuri za matibabu hapa JKCI kwani
wagonjwa tunahudumiwa vizuri, wataalam wa afya hapa wanafanya kazi kwa wito,
wanapita katika vitanda vyetu kila mara kuulizia kama tunahitaji huduma yoyote
sikutegemea kama ningepata huduma nzuri hivi”, alisema Nahida
Akizungumza kuhusu kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya
moyo na mfumo wa umeme wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Yona Gandye alisema katika kambi hiyo wagonjwa 13 wenye matatizo mbalimbali ya
moyo wamefanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab.
Wagonjwa hao walikuwa na matatizo ya hitilafu ya mfumo wa
umeme wa moyo, matatizo ya moyo kwenda kasi, matatizo ya moyo kuchoka na
kushindwa kufanya kazi, na matatizo ya mishipa ya damu kuziba kwa muda wa siku
90 hivyo kufanya upasuaji wake kuwa mgumu.
Dkt. Gandye alisema upande wa wagonjwa wenye hitilafu ya
mfumo wa umeme wa moyo walikuwepo wagonjwa ambao mapigo yao yalikuwa
yamevurugika (Atrial Fibrillation - AF), wagonjwa ambao husikia mioyo yao ikidunda
na ghafla kusikia ukimya hivyo kuhisi mioyo yao imesimama (PVC), na wagonjwa
ambao wamezaliwa wakiwa na njia ya ziada ya kutengeneza mapigo ya moyo.
“Wagonjwa ambao wamezaliwa wakiwa na njia ya ziada ya
kutengeneza mapigo ya moyo huweza kuwa na tabia mbalimbali kama vile kusababisha
moyo kwenda kwa kasi zaidi, ama wengine kutokuwa na dalili yoyote ambayo huweza
kusababisha vifo vya ghafla”, alisema Dkt. Gandye
Dkt. Gandye alisema wamekuwa wakifanya kambi maalum za
matibabu ya moyo kwa wagonjwa wanaowahudumia kwa pamoja na wataalamu wabobezi
kutoka hospitali mbalimbali duniani wakiwa na lengo la kubadilishana ujuzi
pamoja na kuwasaidia wagonjwa kupata huduma bora.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka
Hospitali ya Max iliyopo nchini India Viveka Kumar alisema hii ni mara yake ya
pili kushirikiana na madaktari wa JKCI ambapo anaona mafanikio makubwa yamekuwa
yakifanyika upande wa upasuaji mdogo wa moyo kwa kutumia tundu dogo.
Dkt. Viveka alisema wataendelea kuwapa ushirikiano wataalam
wa JKCI pale wanaohitaji ujuzi kutoka kwao ili wagonjwa wote wenye matatizo ya
moyo waliopo hapa nchini pamoja na nchi za jirani wafike katika Taasisi hiyo
kwa ajili ya kupatiwa matibabu kwani taasisi hiyo imewekeza vifaa vya kisasa
kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa moyo.
“Maono yangu katika siku za hivi karibuni wataalam wa afya wa
hapa JKCI watakuwa na uwezo wa kufanya upasuaji wa aina nyingi zaidi kama
wazawa kutokana na kasi waliyonayo ya kujifunza wakati tunabadilishana uzoefu”,
alisema Dkt. Viveka
Dkt. Viveka alisema kuwa kabla ya Taasisi hiyo kuanzishwa
India ilipokea wagonjwa wengi wa moyo kutoka Tanzania lakini baada ya uwekezaji
uliofanywa katika Taasisi hiyo na wataalam kubobea katika kutoa matibabu ya
kibingwa ya moyo sasa wagonjwa wa moyo hawana haja ya kwenda nchini india kwa
ajili ya matibabu ya moyo.
Comments
Post a Comment