Wakazi wa Zanzibar waishukuru Serikali kwa kuwapelekea huduma ya kibingwa ya matibabu ya moyo
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) George Longopa akimfanyia mgonjwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography - ECHO) leo wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya moyo ya siku tano inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar.
Daktari wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jackline Mathew akimfanyia mtoto kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography - ECHO) leo wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya moyo ya siku tano inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar.
Afisa Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar Amina Hassan akimpima urefu na uzito mtoto aliyefika katika hospitali hiyo leo kwa ajili ya kupata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo. Kulia ni mama wa mtoto Salma Ali.
Fundi sanifu wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Paskal Kondi akimfanyia mwananchi kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography - ECHO) wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya moyo ya siku tano inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar.
Wakazi wa Zanzibar waishukuru
Serikali kwa kuwapelekea huduma ya matibabu ya moyo
Wakazi wa Zanzibar wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea huduma ya kibingwa ya upimaji na matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima inayotolewa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo visiwani humo.
Huduma hiyo inatolewa bila malipo katika kambi maalumu ya
siku tano inayofanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Mnazi Mmoja
Zanzibar.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo Visiwani Zanzibar wananchi
waliofika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata huduma ya upimaji na
matibabu ya moyo walisema kupatikana kwa huduma hiyo kumewarahisishia tofauti
na ambavyo wangeifuata huduma hiyo Dar es Salaam.
Saada Simba mkazi wa Fuoni alisema baada ya kusikia wataalamu
wa moyo watakuwepo katika Hospitali hiyo alifika kwa ajili ya kupima afya yake
amefarijika kwani amepata huduma nzuri na kwa wepesi.
“Mimi ninatatizo la
shinikizo la juu la damu (BP) baada ya kufanyiwa vipimo leo nimekutwa sina
tatizo lolote zaidi ya hili nililokuwa nalo, nashukuru sana nimepewa ushauri na
nimeongezewa dawa nyingine ya kutumia ambayo ninaenda kuichukuwa dirishani bila
malipo yoyote yale”, alisema Saada.
Naye Juma Amoor mkazi wa alisema akiwa kazini mwaka 2019 alipata mshtuko wa moyo
kwani mapigo yake yalikuwa yanadunda kwa kasi alifanyiwa uchunguzi na
kuandikiwa dawa za kutumia lakini alifika hapo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi
zaidi na kujua tatizo ni nini.
“Nawashauri wananchi wenzangu tujenge tabia ya kupima afya
zetu pindi tunaposikia wataalamu kama hawa wamefika katika maeneo yetu twendeni
kupima. Baada ya kufika hapa leo nimepima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya
kazi (ECHO), mfumo wa umeme wa moyo (ECG), kiwango cha sukari mwilini,
shinikizo la damu, urefu na uzito bila malipo yoyote yale”, alisema Amoor.
Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha utafiti na mafunzo cha
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo alisema taasisi hiyo
imekuwa na utaratibu wa kusogeza huduma zake kwa wananchi kwa kuwafuata mahali
walipo na kuwapatia huduma ya upimaji na matibabu ya moyo.
Dkt. Pedro alisema kuwepo kwa huduma hiyo kumewasaidia
wananchi kupata huduma ya ushauri wa lishe na matumizi sahihi ya dawa, vipimo
na matibabu ya moyo kwa wakati tofauti na ambavyo wangesafiri na kuifuata
huduma hiyo Dar es Salaam pia wanaokutwa na matatizo wanapewa rufaa ya kwenda
kufanyiwa uchunguzi zaidi katika Taasisi hiyo.
Dkt. Pedro alisema, “Ninatoa wito kwa wananchi kufuata mtindo
bora wa maisha kwa kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kupunguza matumizi
makubwa ya sukari, chumvi na vyakula vyenye mafuta, kupunguza unywaji wa pombe
na kuacha kutumia bidhaa aina ya tumbaku kwa kufanya hivyo wataepukana na
magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo”,.
Katika kutoa huduma ya kuwafuata wananchi mahali walipo
Taasisi hiyo kwa mwaka 2022 ilifanya upimaji na matibabu ya moyo kwa watoto na
watu wazima katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Geita, Mtwara na
Lindi na kuwahudumia watu 3,935 kati ya hao 1,391 walikutwa ma magonjwa
mbalimbali ya moyo ikiwemo shinikizo la damu, kutanuka kwa misuli ya moyo,
kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo, matundu ya moyo hasa kwa watoto na valvu za
moyo zilizoharibika. Wagonjwa 335 walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.
Comments
Post a Comment