RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt.Peter
Kisenge, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe.Hassan Khamis Hafidh, baada ya kumalizika kwa
Matembezi ya Kuhamasisha Upimaji wa Moyo, Kufanya mazoezi “Tembea na JKCI Linda
Afya ya Moyo Wako” na Ufungaji wa Kambi ya Upimaji wa Moyo iliyofanyika tarehe 23-27
Januari 2023 , katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali pamoja
na wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) mara baada ya
kumalizika kwa Matembezi ya Kuhamasisha Upimaji wa Moyo, Kufanya mazoezi “Tembea
na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” na Ufungaji wa Kambi ya Upimaji wa Moyo
iliyofanyika tarehe 23-27 Januari 2023 , katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja
Unguja Jijini Zanzibar.
*******************************************************************************************************************************************************************************************************************
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.
Hussein Ali Mwinyi amesema magonjwa ya moyo yameongezeka kwa wingi na yanathiri
afya za wananchi, utendaji kazi na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Dk. Mwinyi alieleza hayo wakati akifunga kambi ya upimaji wa
moyo pamoja na matembezi ya kampeni maalum ya zuia magonjwa yasioambukiza
yaliyoanza katika viwanja vya Maisara hadi viwanja vya Amani Stadium.
Alisema kutokana na hali hiyo taifa limekuwa likitumia fedha
nyingi za kigeni kugharamia matibabu ya moyo na magonjwa mengine nje ya nchi.
Aidha alisema takwimu mbalimbali zilizokuwepo zinaonesha kuna
ongezeko kubwa la magonjwa yasiambukuza hutokana na mfumo wa maisha na aina ya
vyakula vinavyoliwa.
Hivyo, aliipongeza Taasisi ya JKCI kwa mipango mizuri na ubunifu
wa kinga na tiba ya maradhi hayo hapa nchini na kuendelea kuwajengea uwezo
watumishi wa Zanzibar katika kutoa huduma.
Aliwasihi kufika na kisiwa cha Pemba kwa ajili ya uchuguzi na
kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi kama njia bora ya kuimarisha afya za wananchi
kwani wanahitaji huduma hizo kama walivyofanya Unguja.
Hivyo aliishauri taasisi hiyo kufikisha huduma hizo za upimaji
kwa jamii pana zaidi kwani hatua hiyo itasaidia kupambana na matatizo
mbalimbali ya kiafya ambayo jamii imekuwa ikikumbana nayo.
Alisema hatua hiyo ya kufanya kambi za mara kwa mara katika
mikoa ya pembezoni itapunguza wagonjwa wanaohitaji rufaa kwenda Dar es salam
kwa matibabu na badala yake watatibiwa walipo.
Akizungumzia utaratibu wa kuleta timu ya madaktari bingwa
alisema ni utaratibu mzuri wa kuanza kujenga uwezo wa Zanzibar hasa katika
hospitali ya Mkoa ya Lumumba kuona inaanza kutoa huduma za matibabu ya moyo.
Hivyo aliiomba taasisi hiyo kutoa msaada kwa madaktari bingwa
watakaonza katika hospitali hiyo ili waweze kujenga uwezo kuona jambo hilo
linafanikiwa
Rais Mwinyi alisema ni matumaini yake kwamba kambi hiyo
haitakuwa ya mwisho na wataendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili lengo
la kuanzishwa kwa tasisi hiyo liweze kufikiwa.
Hata hivyo, aliishauri taasisi hiyo kuendelea kuimarisha
utendaji wao ili wananchi wengi waweze kunufaika na huduma bora wanazozitoa
zenye kiwango cha kimataifa.
Aliwasihi wananchi kuendelea kushiriki katika kambi mbalimbali
za upimaji wa magonjwa na matembezi kama hayo kwani kufanya mazoezi ni kinga
muhimu ya kujikinga na magonjwa mbalimbali hasa yasioambukiza.
“Sote kwa pamoja tuhimizane kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi
ili kuimarisha afya zetu na kuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili
kubaini mapema kama tuna matatizo na kuchukua hatua za matibabu mapema,”
alisisitiza.
Alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo na wizara ya
afya kuanzisha program hiyo ambayo inakuwa ni mfano mzuri kwa jamii kufanya
mazoezi ili kujikinga na maradhi yasiambukiza.
Akimkaribisha Rais Mwinyi, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed
Mazrui alisema ipo haja ya kuwa na taasisi ya moyo hapa Zanzibar kwani kwa
mwaka 2021/2022 jumla ya wagonjwa 584 wanaohitaji huduma tofauti na matibatu ya
kibingwa walisafirishwa nje ya Zanzibar kati ya hao ugonjwa wa moyo unaongoza
kwa rufaa ya asilimia 28.
Alisema hadi kufikia Disemba 2022 jumla ya watoto 2030
walionekana kuwa na maradhi hayo huku waliofanyiwa upasuaji walikua 1,125 kati
ya hao 800 walifanyiwa Izrael, 275 walifanyiwa India na 50 katika taasisi ya
JKCI.
Aidha alisema wastani wa watoto watatu hadi watano hufariki
dunia kila mwezi katika hospitali ya Mnazimmoja na wastani wa kesi 110 mpaka
150 za watoto wapya hugundulika na magonjwa ya moyo kila mwaka katika hospitali
hiyo huku gharama zinazotumika kutibu wagonjwa wa moyo Tanzania bara kwa mwaka
ni milioni 650 hadi milioni 850.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Dk.
Peter Richard Kisenge, alisema taasisi hiyo imekuwa ikipata wagonjwa wanaotoka
nchi mbalimbali ikiwemo Comoro, Zimbabwe, Malawi, Zaire na sehemu za Ulaya.
Alibainisha kuwa mwaka 2021/2022 walipokea wagonjwa 1,087 kutoka
Zanzibar huku wagonjwa 570 walilipiwa na serikali kupata huduma huku wagonjwa
519 walikuwa na bima za afya na wengine walijitolea wenyewe.
Aliipongeza serikali inavyojitoa katika kuwahudumia wananchi wa Zanzibar
kwani matatizo ya magonjwa ya moyo hapa Zanzibar yanaongezeka kwa kasi kubwa.
Hivyo alimuhakikishia Rais Mwinyi kuwa taasisi hiyo kwa
kushirikiana na hospitali ya rufaa Mnazimmoja katika kutoa huduma hiyo kwani
wanataka hospitali hiyo nayo iweze kutoa matibabu ya ubingwa wa moyo na hata
kufanya upasuaji wa moyo.
“Tunaweza kusimika mtambo wa Cathlab kufungua upasuaji wa moyo
kwani Jakaya Kikwete ilianza kwa chumba katika hospitali ya mifupa Moy hivyo
tutumie utaratibu huo huo kuanza katika hospitali ya Rufaa Mnazimoja,”
alishauri.
Mbali na hayo alisema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na
serikali kupitia wizara ya Afya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za
matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo kwa kufuata walipo na sasa
wameshahudumia zaidi ya wagonjwa 3000.
Alisema katika kambi hiyo walihudumia wagonjwa 718 kati ya hao
wagonjwa watu wazima walikuwa 627 na watoto 91 huku watu wazima 549
waligundulika na matatizo ya moyo huku rufaa 75 wakiwemo watu wazima 49 na
watoto 26.
Akizungumzia lengo la kuanzisha program ya tembea na Jakaya
Kikwete Linda moyo wako alisema inalenga kuwahamisha wananchi kufanya mazoezi,
ili kujikinga na magonjwa hayo yasioambukiza kwani karibu watu 17,000,000
wanapoteza maisha kutokana na matatizo hayo.
Aliahidi kwamba taasisi hiyo itaendelea kuhakikisha wananchi
wanapata huduma bora za matibabu ya moyo na kutoa elimu kwa wananchi juu ya
kujikinga na magonjwa hayo.
Comments
Post a Comment