JKCI yaokoa milioni 951 matibabu ya wagonjwa 25 nje ya nchi
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na Mishipa ya damu wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na mwenzao kutoka
Hospitali ya Max iliyopo nchini India Dkt. Sinha Kumar kuvuna mshipa wa damu
katika mguu wa mgonjwa utakaopandikizwa katika moyo wakati wa kambi maalum ya
siku tano ya matibabu ya moyo kwa wagonjwa ambayo mioyo yao inafanya kazi kwa
asilimia 17 hadi 45. Jumla ya wagonjwa 25 wamepatiwa matibabu katika kambi hiyo
Picha na: Khamis Mussa
****************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa zaidi ya
shilingi milioni 951 ambazo Serikali ingetumia kama wagonjwa 25 wenye matatizo
ya mishipa ya damu kuziba, matatizo ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo,
matatizo ya moyo kwenda kasi na matatizo ya moyo kuchoka na kushindwa kufanya
kazi wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu
Wagonjwa hao ambao viwango vya ufanyaji kazi wa mioyo yao ni
kuanzia asilimia 17 hadi 45 wamefanyiwa upasuaji katika kambi maalum ya siku
tano iliyofanywa na madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India.
Akizungumzia kambi hiyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema upasuaji wa moyo kwa
wagonjwa hao umefanyika kwa ufanisi mkubwa lakini pia kutoa nafasi kwa
wataalamu wa JKCI kujifunza namna ya kuwapatia huduma wagonjwa ambao mioyo yao
ufanyaji kazi wake upo chini.
“Katika kambi hii tulijikita kuwafanyia upasuaji wagonjwa
ambao viwango vya ufanyaji kazi wa mioyo yao imeshuka ambapo mgonjwa mmoja
tuliyemfanyia upasuaji kiwango chake cha ufanyaji kazi wa moyo kilikuwa
kimeshuka hadi asilimia 17”,
“Kadiri kiwango cha ufanyaji kazi wa moyo kinavyoenda chini
upasuji wake unakuwa mgumu na matokeo yake huwa ya hatari, hivyo hawa wenzetu
kutoka India wamekuwa wakifanya upasuaji kwa wagonjwa wa aina hii bila shida
kutokana na uzoefu na vifaa walivyonavyo”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela alisema gharama za upasuaji mkubwa wa moyo kwa
mgonjwa mmoja akifanyiwa hapa nchini umgharimu shilingi milioni 16, lakini kama
angeenda nje ya nchi ingemgharimu sio chini ya shilingi milioni 40.
Dkt. Angela aliongezea kuwa kwa upande wa upasuaji mdogo kwa
kutumia mtambo wa Cathlab mgonjwa mmoja umgharimu kiasi cha shilingi milioni 29
lakini kama angeenda nje ya nchi ingemgharimu hadi shilingi milioni 80
kufanyiwa upasuaji wa moyo.
“Hapo awali wagonjwa ambao ufanyaji kazi wa mioyo yao ulikua
umeshuka tulikuwa tunawapeleka nje ya nchi kwa ajili ya matibabu lakini
tunavyoendelea kupata ujuzi wagonjwa hawa watakuwa wakipatiwa matibabu katika
Taasisi yetu kwa ubora zaidi”, alisema Dkt. Angela
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa
ya damu kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India Sinha Subhash alisema
wataalam wa JKCI wamekuwa na shauku ya kujifunza mambo mapya katika upasuaji wa
moyo hivyo kuifanya Taasisi hiyo kukuwa kwa kasi.
“Nimekuwa nikiwafundisha njia tofauti za kufanya upasuaji wa
kuzibua mishipa ya damu kwa wagonjwa ambao ufanyaji kazi wa mioyo yao ni wa
asilimia ya chini na kwa madaktari wa hapa naona mabadiliko kwani sasa wanaweza
kufanya hata bila ya kusimamiwa”, alisema Dkt. Sinha
Aidha Dkt. Sinha aliongezea kuwa kutokana na uhusiano mzuri
alionao na watalaam wa JKCI ataendelea kushirikiana nao mara kwa mara kwani
Tanzania imekua sehemu anayoiona kama nyumbani kwake.
Naye Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Evarist Nyawawa alisema katika kambi hiyo
wamewafanya upasuaji wagonjwa ambao mishipa yao ya damu ilikuwa imeziba kwa kiwango kikubwa.
“Kutokana na uzoefu wa wataalam kutoka nchini India wamekuwa
wakichagua wagonjwa ambao mishipa yao imeziba kwa kiwango kikubwa hivyo kufanya
upasuaji wake kuwa mgumu tofauti na tunapokuwa peke yetu wakati mwingine
huwaacha wagonjwa wa aina hiyo ili waende nje ya nchi kwa ajili ya matibabu”,
“Tumepata uzoefu wa kiwango kikubwa kuwahudumia wagonjwa
ambao mishipa yao imeziba kwa kiwango kikubwa na utendaji wa kazi wa mioyo yao
ni wa asilimia ndogo, tunawashukuru sana wataalam hawa kutushika mkono na kuweza
kuhimili kuwatibu watanzania wenzetu”, alisema Dkt. Nyawawa
Comments
Post a Comment