Dkt.Mwinyi aongoza matembezi ya kuhamasisha upimaji wa moyo na kufanya mazoezi


 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwasalimia na wananchi wa mitaa ya Muembemimba akiwa katika Matembezi ya Kuhamasisha Ufanyaji wa Mazoezi  “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” na Kufunga Kambi ya Upimaji wa Moyo iliyofanyika katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja Jijini Zanzibar kuazia 23 - 27, Januari 2023. Matembezi hayo yalianzia  katika viwanja vya Maisra Suleiman na kumalizikia katika Uwanja wa Amaan Unguja leo 28-1-2023. Kushoto kwa  Rais ni  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akishiriki katika Matembezi ya Kuhamasisha Ufanyaji wa Mazoezi  “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” na Kufunga Kambi ya Upimaji wa Moyo iliyofanyika katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja kuazia 23-27, Januari 2023, matembezi hayo yaliyoanzia katika viwanja vya Maisara Suleiman na kumalizikia katika Uwanja wa Amaan Unguja leo 28-1-2023  (kushoto kwa Rais) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Peter Kisenge, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan K.Hafidh na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said na (kulia kwa Rais) Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Idrissa Mustafa Kitwana.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi, akishiriki katika mazoezi ya viungo yakiongozwa na Kocha Mkuu wa Mazoezi ya Viungo Zoni D. Ndg. Ahmad Rajab, baada ya kumalizika kwa Matembezi ya Kuhamasisha Upimaji wa Moyo na kufanya mazoezi  “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” yaliyoanzia katika viwanja vya Maisara Suleiman na kumalizikia katika Uwanja wa Amaan Unguja na(kulia kwa Rais) ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui na (kushoto kwa Rais) Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  Dkt.Peter Kisenge.

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishiriki katika mazoezi ya viungo baada ya kumalizika kwa Matembezi ya Kuhamasisha Upimaji wa Moyo na kufanya mazoezi  “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” yaliyoanzia katika viwanja vya Maisara Suleiman na kumalizikia katika Uwanja wa Amaan Unguja. Matembezi hayo yaliongozwa na RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia baada ya kumalizika kwa Matembezi ya Kuhamasisha Upimaji wa Moyo na ufanyaji wa Mazoezi “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” na kufunga Kambi ya Upimaji wa Moyo, iliyofanyika katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja Jijini Zanzibar 23-27,Januri 2023, matembezi hayo yalimalizika katika Uwanja wa Amaan Unguja.

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza baada ya kumalizika kwa Matembembezi ya Kuhamasisha Upimaji wa Moyo na kufanya mazoezi  “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” na ufungaji wa Kambi ya Upimaji wa Moyo iliyofanyika katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja iliyoaza 23-27,Januari 2023, ufungaji huo uliyofanyika katika uwanja wa Amaan Unguja Jijini Zanzibar. 

WAZIRI wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmin Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi, kuzungumza na Wananchi, baada ya kumalizika kwa Matembezi ya Kuhamasisha Upimaji wa Moyo na kufanya mazoezi “Tembea na JKCI Linda Afya ya Moyo Wako” na ufungaji wa Kambi ya Upimaji wa Moyo iliyofanyika katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja Jijini Zanzibar, iliyoaza 23-27,Januari 2023, matembezi hayo yaliyomalizikia katika uwanja wa Amaan Unguja.

**********************************************************************************************************************************************************************************

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kubadili mfumo wa maisha kwa kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa mbalimbali yasioambukiza ukiwemo ugonjwa wa moyo.

Alisema hatua hiyo imethibitishwa na wataalamu wa afya kupitia utafiti walioufanya unaoonesha moja ya hatua muhimu ya kukabiliana na magonjwa hayo ni kufanya mazoezi.

“Nawasihi nyote muendelee kushiriki kwenye kambi mbalimbali za upimaji wa magonjwa na matembezi kama haya, kwani ni muhimu kwa afya zenu, kila mtu huko anakoishi atambue kufanya mazoezi ni kinga muhimu katika kuepuka magonjwa mengi hasa yasio ambukiza, kwa hiyo sote tuhimizane tujenge utamaduni wa kufanya mazoezi na kupima afya zetu mara kwa mara ili kubaini mapema kama tuna matatizo ya kiafya, kuchukue hatua za matibabu” Alishauri Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo viwanja vya Amani, Zanzibar alipofunga kambi ya upimaji na matibabu ya moyo na kampeni ya kufanya mazoezi yenye kauli mbiu “Tembea JKCI, Linda Afya ya Moyo Wako”.

Alisema taifa linatumia pesa nyingi za kigeni kugharamia matibabu ya moyo na magonjwa mengine nje ya nchi. Hivyo aliipongeza taasisi ya JKCI kwa kubunifu mikakati mbali mbali ya kinga na tiba ya maradhi ya moyo nchini.

Aidha, aliishukuru taasisi hiyo kwa kuwajengea uwezo watumishi wa afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwasihi kuendeleza utamaduni huko kwa watumishi wa Pemba.

“Nawasihi JKCI mfike na Pemba kwa ajili ya uchunguzi na kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi kama njia bora ya kuimarisha afya, bila ya shaka wananchi wa Pemba nao wanahitaji huduma zenu na elimu hii kama mlivyofanya hapa Unguja” Alishauri Dk. Mwinyi.

Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi aliitaka  taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuongeza huduma zao kwenye maeneo mbalimbali ya nchi na kueleza kuwa kuwepo kwao kutasaidia kupambana na matatizo mbali mbali ya afya ambayo jamii wanakabiliana nayo.

Alieleza hatua hiyo itasaidia kuongeza uwezo na wataalamu watakao wahudumia vizuri wananchi na kupunguza madhara ya magonjwa haya ambayo yanaongezeka kila siku.

Alisema tokea kuanzishwa kwa taasisi hiyo, mwaka 2015 tayari imesaidia wagonjwa wengi wakiwemo waliotibiwa kwa dawa na waliofanyiwa upasuaji na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, hivyo aliitaka taasisi hiyo kuimarisha utendaji wao na kuongeza tija kwa watu wengi kunufaika na huduma zao.

“Nafahamu kuwa taasisi hii imekuwa na utendaji mzuri sana tokea ilipoanzishwa. Hata hivyo, bado kuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi ili kuyafikia malengo ambayo Tanzania tumejiwekea, katika kuimarisha afya za wananchi kwa kutoa huduma bora na zenye kiwango cha kimataifa”. Alieleza.

Akizungumza kwenya hafla hiyo, Waziri wa Afya, Nassor Mazurui alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar watashirikiana na taasisi ya JKCI, kuongeza wataalam wa matatizo ya moyo Zanzibar kutokana na uhaba wa wataalamu hao ambapo alieleza kwasasa wapo wawili tuu.

Alisema alisema Zanzibar kwa sasa ina madaktari bingwa wawili tuu wanaoshughulikia matatizo ya moyo.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Richard Kisenge, alisema taasisi yao kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar, kupitia hospitali kuu ya Mnazi Mmoja wataendeleza matibabu ya moyo kwa kutoa huduma za uzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo na upasuaji mkubwa wa moyo kwa wananchi ili kudumisha ushirikiano wao kwa vitendo.

Alisema kampeni walioifanya wiki nzima Unguja alieleza walifanikiwa kuwahudumia wagonjwa 718, wakubwa 627 na watoto 91 ambao walifanyiwa vipimo vya matibabu ya moyo, sukari na magonjwa mengine.

Dk. Kisenge aliongeza kati ya watu wazima 627 waliopimwa matatizo ya moyo, 549 waligunduliwa wana ugonjwa wa moyo alieleza katika hatua hiyo walitoa rufaa 75 kwa baadhi ya wagonjwa na kueleza kuwa 46 walipewa watu wazima na rufaa 29 walipewa watoto.

Kampeni ya upimaji magonjwa yasiyoambukiza ya (JKCI)na ufanyaji wa mazoezi  iliadhimishwa kwa kauli mbiu yao TEMBEA NA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI) na WIZARA YA AFYA, LINDA AFYA YA MOYO WAKO”.

IMETAYARISHWA NA IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

 

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari