JKCI kupunguza msongamano wa wagonjwa kupitia kliniki zake
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi hiyo jana wakati wa kikao cha wafanyakazi kujadili maendeleo ya Taasisi hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisikiliza wakati wa kikao cha wafanyakazi kilichofanyika jana katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Kitengo cha
Tehama wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Lazaro Swai akielezea namna
mifumo ya Tehama inavyofanya kazi wakati wa kikao cha wafanyakazi kujadili
maendeleo ya Taasisi hiyo kilichofanyika jana katika ukumbi wa JKCI uliopo
jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Evarist Nyawawa akichangia mada wakati wa kikao cha wafanyakazi kujadili maendeleo ya Taasisi hiyo kilichofanyika jana katika ukumbi wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
**********************************************************************************************************
Wataalamu wa afya wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na
kuhakikisha msongamano wa wagonjwa waliopo JKCI unafanyiwa kazi kupitia kliniki
mpya za taasisi hiyo zilizofunguliwa Oystebay na Kawe.
Akizungumza wakati wa
kikao cha wafanyakazi jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema menejimenti ya JKCI
imefanya kazi kubwa kufungua matawi hayo kutokana na idadi ya wagonjwa wa moyo
kuongeza na uhitaji wa huduma za matibabu hayo kuwa kubwa.
“Kliniki za JKCI
zilizopo Oysterbay na Kawe zimelenga kupunguza msongamano wa wagonjwa hapa
makao makuu lakini pia kusogeza huduma karibu na wananchi ili wasipate usumbufu
kufuata huduma hizi mbali na wanapoishi”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema JKCI
imeendelea kutambulika ndani na nje ya nchi hivyo kuzifanya nchi za Afrika
kushirikiana nayo katika kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na
nyingine kushirikiana na JKCI katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo.
“Taasisi yetu kwa mwaka
2024 imeweza kufanya kambi ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo nchini Comoro
ambapo wagonjwa zaidi ya 2000 walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa hayo na kufanya
upasuaji wa moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo nchini Zambia”, alisema Dkt.
Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge
alisema mwaka 2024 JKCI ilifanya mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo
ambapo zaidi ya washiriki 500 kutoka nchi zaidi ya 12 waliweza kushiriki na
kubadilishana ujuzi.
Akizungumzia mifumo ya
Tehama iliyopo katika Taasisi hiyo Mkuu wa Kitengo cha Tehama Lazaro Swai
alisema kitengo hicho kinaendelea kuboresha mifumo hiyo kurahisisha huduma kwa
wagonjwa na kupunguza matumizi ya karatasi katika kutoa huduma.
Swai alisema mifumo ya
Tehama katika sekta ya afya inasaidia kutunza taarifa za mgonjwa kwa kipindi
cha muda mrefu tofauti na kama taarifa hizo zikihifadhiwa kwa njia ya faili.
“Mifumo yetu inaendelea
kuboresha kila siku na kuondoa changamoto zote zinazojitokeza ili tuweze
kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia”, alisema Swai
Naye Kaimu Mkurugenzi
wa Utawala na Rasilimali watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Joachim
Asenga aliwataka wafanyakazi wa Taasisi hiyo kufanya kazi kwa kufuata kanuni,
sheria na taratibu za utumishi wa umma.
Asenga alisema uongozi
wa JKCI unatambua mchango mkubwa unaofanywa na wafanyakazi hivyo katika bajeti
ya mwaka 2025/2026 wafanyakazi watapata ongezeko katika motisha zinazotolewa na
taasisi.
Comments
Post a Comment