Watu wenye ulemavu 188 wapima moyo Dar
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce akizungumza na mtu mwenye ulemavu mara baada ya
kupima vipimo vya moyo wakati wa hafla fupi ya chakula cha mchana na zawadi kwa
watu hao iliyoandaliwa na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao na kufanyika jana
katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group Fatma Suedy akimpima shinikizo la damu msanii wa muziki
wa dansi Patcho Mwamba wakati wa hafla fupi ya chakula cha mchana na zawadi kwa
watu wenye ulemavu iliyoandaliwa na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao na
kufanyika jana katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group Happiness Shirima akimpima wingi wa sukari kwenye damu
msanii wa muziki wa dansi kutoka bendi ya FM Academia Pablo Masai wakati wa
hafla fupi ya chakula cha mchana na zawadi kwa watu wenye ulemavu iliyoandaliwa
na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao na kufanyika jana katika viwanja vya
Karemjee jijini Dar es Salaam.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Khairoon
Mohamed akizungumza na mtu mwenye ulemavu mara baada ya kupima vipimo vya moyo
wakati wa hafla fupi ya chakula cha mchana na zawadi kwa watu hao iliyoandaliwa
na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao na kufanyika jana katika viwanja vya
Karimjee jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
**********************************************************************************************************
Watu wenye ulemavu 188 wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya
magonjwa ya moyo, sukari na shinikizo la damu.
Matibabu hayo yamefanyika jana wakati wa hafla fupi ya
chakula cha mchana na zawadi kwa watu hao iliyoandaliwa na Taasisi ya Mama
ongea na mwanao katika viwanja vya Karimjee vilivyopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Mohamed Aloyce alisema katika upimaji huo watu wenye ulemavu 20 wamepewa rufaa
kufika katika Kliniki ya Taasisi hiyo iliyopo Kawe kwaajili ya matibabu zaidi.
“Tumewakuta baadhi ya watu wana matatizo ya shinikizo la juu
la damu, lakini kutokana na vipato vyao kuwa chini wanashindwa kwenda hospitali
kwaajili ya matibabu ama hata wakienda na kupewa dawa mara moja hawarudi tena”,
alisema Dkt. Aloyce
Dkt. Aloyce alisema kupitia hafla hiyo watu wenye ulemavu
wameweza kupata huduma za afya lakini bado kuna uhitaji wa kuwa na bima za afya
kwa kila mmoja ili pale wanaopopata changamoto za afya waweze kutibiwa kirahisi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama ongea na mwanao
Stevene Mengele alisema Taasisi hiyo imeweza kuwakusanya watu wenye ulemavu kukaa
nao pamoja na kuwapa faraja.
Stevene alisema kundi la walemavu lilisahaulika ndio maana
baada ya kuwakusanya wakaona kuna umuhimu nao waweze kupimwa magonjwa ya moyo,
kucheza nao pamoja na kuwapa faraja ili wajisikie kuwa sawa na wengine.
Stevene aliwapongeza wataalamu wa afya kwa kuwa na moyo
wakujitoa kwa watu hao kuhakikisha wote waliohitaji huduma ya uchunguzi wa afya
wamepata kwa wakati.
“Kazi ya kutibu ni ngumu, Mungu awasimamie, tunaomba sana
msituache hata hapo baadaye tukiwataka tena mtukubalie ili kwa pamoja tuweze
kuwafikia watu wa kundi hili kupata huduma hizi muhimu za afya”, alisema
Stevene
Wakiongea mara baada ya kupima afya watu wenye ulemavu
wameishukuru serikali kwa kutoa huduma hiyo kwao kwani wengi wao hawakuwahi
kufanya vipimo hivyo na hawakuwa na matarajia ya kupima moyo katika maisha yao.
Joseph Jackson mkazi wa mbagala alisema hakujua kama ana
tatizo la sukari hadi baada ya kupima na kupata majibu katika hafla hiyo ndio
amegundua kuwa na tatizo la sukari.
“Naishukuru sana serikali yangu kwa kutusaidia kupata huduma
za afya, leo nimepima magonjwa ya moyo, sukari, na shinikizo la damu na kukutwa
na tatizo la sukari. nimepewa rufaa na nina ahidi kwenda kuchunguza zaidi.
Naye Agnes Mwanuke mkazi wa Temeke ameishukuru JKCI kwa kutoa
huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa walemavu kwani amekuwa
akisikia maumivu makali upande wa kushoto wa moyo lakini kutokana na utafutaji
wake kuwa wa shida hakufikiria kwenda hospitali kutibiwa.
“Sisi watu wenye ulemavu utafutaji wetu ni washida sana hivyo
kushindwa kupata kipato cha kutupeleka hospitali kupata huduma za matibabu
lakini walivyotusogezea hapa tunawashukuru sana kwani tumechunguza afya zetu”,
aliema Agnes.
Agnes aliomba huduma hizo zisiishie kwa walemavu hao bali
taasisi iangalie namna ya kuwafikia walemavu wengine nchini ili nao waweze
kupima afya zao kwani afya ndio mtaji wa maisha.
Comments
Post a Comment