JKCI wafundishwa teknolojia ya kisasa ya kuziba matundu ya moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na Wataalamu wa afya kutoka
Hospitali ya Fuwai iliyopo Beijing China na wengine wa JKCI mara baada ya mafunzo
ya jinsi ya kuziba matundu na kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba bila
kutumia mashine ya mionzi leo katika taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
akizungumza na wataalamu wa afya kutoka Hospitali Fuwai iliyopo Beijing China
leo wakati wataalamu hao walipofika JKCI kwaajili ya kubadilishana ujuzi na
wenzao wa JKCI katika kutoa huduma za upasuaji mdogo wa moyo bila kutumia
mashine ya mionzi kwa watoto wenye magonjwa ya moyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Fuwai iliyopo Beijing China prof. Xiangbin Pan akielezea namna huduma za upasuaji mdogo wa moyo bila kutumia mionzi zinavyoweza kufanyika kirahisi kutokana na maendeleo ya teknolojia wakati wa mafunzo ya jinsi ya kuziba matundu na kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba bila kutumia mashine ya mionzi yaliyokuwa yakitolewa leo kwa wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Fuwai iliyopo Beijing China Prof. Xiangbin Pan akimpatia zawadi kutoka china Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge baada ya mafunzo ya jinsi ya kuziba matundu na kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba bila kutumia mashine ya mionzi kwa wataalamu wa JKCI leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi wa wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Fuwai iliyopo Beijing China na wenzao wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisikiliza wakati wa mafunzo ya jinsi ya kuziba matundu na kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba bila kutumia mashine ya mionzi leo katika taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
*****************************************************************************************************************
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamepewa mafunzo ya jinsi ya kuziba matundu na kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba bila ya kufanya upasuaji wa kufungua kifua na bila ya kutumia mashine zenye mionzi.
Upasuaji
huo unafanyika kwa njia ya tundu dogo kwa kutumia mashine ya kuangalia jinsi
moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO).
Akizungumza
kuhusu mafunzo hayo yaliyotolewa leo jijini Dar es Salaam, Prof. Xiangbin Pan ambaye ni Mkurugenzi Mkuu kutoka
hospitali ya Fuwai iliyopo Beijing nchini China alisema hivi sasa teknolojia ya
matibabu ya moyo imekuwa na imefikia hatua uwekezaji wake hauhitaji kuwa na mashine za gharama kubwa katika kufanya
upasuaji.
Prof. Pan alisema wagonjwa wengi wa moyo wako vijijini na
wanazifuata huduma za matibabu na upasuaji mijini mahali ambako kuna hospitali
kubwa zenye wataalamu wabobezi, kufanyika kwa upasuaji huo kunawapunguzia
wananchi gharama ya kusafiri na kukaa hospitali muda mrefu.
Dkt.
Kisenge alisema ushirikiano uliopo kati ya China na Tanzania ni wa muda mrefu
na unafaida nyingi moja ya faida iliyopo ni katika sekta ya afya ambapo serikali
ya China ilijenga jengo la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kila baada
ya miaka miwili madaktari bingwa kutoka nchini humo wanakuja hapa nchini kutoa huduma
za matibabu ya kibingwa kwa wananchi.
“Matibabu
haya ni ya teknolojia ya hali ya juu na ni rahisi kufanyika kwani hayatumii
mionzi ambayo inaweza kusababisha madhara kwa mgonjwa pamoja na mtoa huduma na
yanapunguza gharama za matibabu”.
“Ninawashukuru sana kwa kuja katika taasisi
yetu kutoa mafunzo na kufanya kambi maalumu ya matibabu ya moyo kwa watoto, hii
siyo mara ya kwanza kwa nyinyi kuja hapa mlishakuja zaidi ya mara tatu mkatoa
huduma za matibabu, mkatupatia vifaa tiba na kutoa mafunzo kwa wataalamu wetu”,
alishukuru Dkt. Kisenge.
Daktari
bingwa wa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Theophylly
Ludovick ambaye alipata mafunzo hayo kwa muda wa miezi mitatu katika ya Hospitali
ya Fuwai nchini China alisema utaalamu alioupata ni wa hali ya juu na atautumia
kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
“Nimejifunza
jinsi ya kutumia mashine ya ECHO kuziba matundu ya moyo ambayo ni teknolojia ya
kisasa, inayomlinda mgonjwa na mtoa huduma kutokupata madhara yatokanayo na
mionzi pia mgonjwa anapata huduma ya matibabu kwa gharama naafuu ukilinganisha
na njia ya kutumia mionzi”, alisema Dkt. Theophylly.
Dkt.
Theophylly alisema teknolojia hiyi ya upasuaji inafanyika kwa watu wazima na
watoto wenye matatizo ya tundu kwenye moyo.
Mafunzo
hayo yanakwenda sambamba na kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo kwa watoto, ambapo wataalamu
wa JKCI na wenzao wa hospitali ya Fuwai watashirikiana
kutoa huduma hiyo.
Comments
Post a Comment