Wananchi wa Mwanza wafikiwa na huduma bingwa za matibabu ya moyo
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Mlagwa Yango akimsikiliza mwananchi aliyefika
kufanya uchunguzi wa afya wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya magonjwa ya
binadamu iliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge wa Nyamagana Mhe. John Nzilanyingi
kwa ushirikiano na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa Mwanza inayofanyika katika
uwanja wa Nyamagana uliopo jijini Mwanza.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Witnes Lyaruu akimpima shinikizo la damu (BP) mkazi wa Mwanza aliyefika
kufanya uchunguzi wa afya wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya magonjwa ya
binadamu iliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge wa Nyamagana Mhe. John Nzilanyingi
kwa ushirikiano na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza inayofanyika katika
uwanja wa Nyamagana uliopo Jijini Mwanza.
Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mwanza wakisubiri
kupata huduma walipotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati
wa kambi maalumu ya matibabu ya magonjwa ya binadamu iliyoandaliwa na Ofisi ya
Mbunge wa Nyamagana Mhe. John Nzilanyingi kwa ushirikiano na Ofisi ya Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza inayofanyika katika uwanja wa Nyamagana uliopo Jijini
Mwanza.
******************************************************************************************
Wananchi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo jirani wamehimizwa
kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo, kufahamu namba zao
na kupata elimu itakayowasaidia kujilinda na magonjwa yasiyoambukiza.
Rai hiyo imetolewa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mlagwa Yango wakati wa kambi maalumu ya siku tano
iliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge wa Nyamagana Mhe. John Nzilanyingi kwa
kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Dkt. Yango alisema kupitia kambi hiyo JKCI inatoa huduma za
uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa watoto na watu wazima na kuwafanyia vipimo
vya kuchunguza mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography - ECG), kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography - ECHO) pamoja na
vipimo vya kupima namba zao muhimu za afya.
“Tunawashauri wananchi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo ya jirani
kutumia fursa hii kujitokeza kwa wingi kwa sababu muda wa kambi ni mfupi na
lengo letu ni kuwasaidia wananchi kufahamu hali za afya zao”, alisema Dkt.
Yango.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliopata huduma
katika banda la JKCI waliishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwachagua viongozi wanaojali wananchi na kuwapa
fursa ya kuchunguza afya zao bila malipo karibu na maeneo wanayoishi.
Kassimu Mohammed mkazi wa Mwanza alisema amefanya maamuzi ya
kufika kupima afya yake hususani moyo ili waweze kupata ushauri sahihi kutoka
kwa wataalamu mabingwa kutoka JKCI.
“Tunamshukuru sana Mbunge wa Nyamagana Mhe. John Nzilanyingi walioandaa kwa kuandaa kambi hii kwa ajili ya
wananchi wa Mwanza, kambi hili inatusaidia sisi wananchi kuyajua magonjwa kwa
kina lakini pia hata kutambua dalili za magonjwa yasiyoambukiza”, alisema
Kassimu.
Naye
Muhidha Juma alisema ameridhishwa
na huduma alizopata katika banda la JKCI kutokana na ukarimu wa wataalamu hao
kutoa huduma kwa upendo, kufuata taratibu walizoweka na kuhakikisha watu wote
wanapata huduma.
Kambi hiyo maalumu ya matibabu ya magonjwa ya binadamu
inayofanyika kwa siku tano ni sehemu ya juhudi za Serikali kusogeza huduma za
kibingwa karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu magonjwa yasiyoambukiza na
kuhamasisha jamii kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini mapema
matatizo yanayoweza kuathiri afya zao.
-
Mwisho
-

Comments
Post a Comment