Wananchi Tarafa ya Ngerengere wapewa elimu ya lishe bora kulinda afya ya moyo


Mtaalam wa lishe kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) akitoa elimu kuhusu lishe bora wakati wa kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na ofisi ya mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamisi Taletale kwa ushirikiano na JKCI katika Hospitali ya Tarafa ya Ngerengere iliyopo mkaoni Morogoro.

Daktari wa Tasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Daudi Gwilenza akimuandikia dawa mwananchi aliyefika maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na ofisi ya mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamisi Taletale kwa ushirikiano na JKCI katika Hospitali ya Tarafa ya Ngerengere iliyopo mkaoni Morogoro.

Mfamasia wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Baraka Mosi akimpatia dawa mkazi wa Tarafa ya Ngerengere aliyefika katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na ofisi ya mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamisi Taletale kwa ushirikiano na JKCI katika Hospitali ya Tarafa ya Ngerengere iliyopo mkaoni Morogoro.

Na JKCI

*******************************************************************************************************************************************

Wananchi wa Tarafa ya Ngerengere Wilaya ya Morogoro Vijijini wamepatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia lishe bora na kuchagua vyakula vinavyosaidia kulinda afya ya moyo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuzuia magonjwa yasiyoambukiza zinazotekelezwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupitia kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya moyo.

Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo Mtaalamu wa Lishe kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Neema Matemba alisema ulaji usiofaa ni miongoni mwa vihatarishi vinavyochangia magonjwa ya moyo hivyo ni muhimu kwa wananchi kuelewa aina ya vyakula wanavyopaswa kutumia ili kulinda afya zao.

Neema alisema katika kambi hiyo wananchi wamefaidiaka na elimu ya lishe ikiwemo namna bora ya kuzingatia mlo kamili, kuchagua vyakula vyenye virutubisho muhimu na kuepuka ulaji unaoweza kuongeza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza.

“Tumekutana na wananchi wenye changamoto mbalimbali za kiafya zikiwemo uzito uliopitiliza, lishe isiyofaa na kisukari, tumewapatia ushauri wa kitaalamu kuhusu namna ya kuboresha ulaji na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kusababisha magonjwa ya moyo”, alisema Neema

Kwa upande wake Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Daudi Gwilenza alisema wananchi wa Tarafa ya Ngerengere wametumia vizuri fursa ya kupata matibabu kwa kushiriki katika kambi hiyo kupata huduma za uchunguzi, ushauri na matibabu ya magonjwa ya moyo zinazotolewa bure na JKCI kwa kushirikiana na mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamisi Taletale.

Dkt. Gwilenza alisema katika kufanikisha utoaji wa huduma hizo wataalamu wa JKCI wameungana na wenzao kutoka Hospitali ya Wilaya ya Morogoro Vijijini ili kuongeza nguvu kazi na kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati.

Akielezea namna huduma hizo zilivyomnufaisha mkazi wa Ngerengere Magreth Malyaga alisema mwanae alipofanyiwa uchunguzi alibainika kuwa na changamoto ya kiafya inayohusiana na moyo hivyo kupewa rufaa ya kwenda JKCI kwaajili ya uchunguzi zaidi.

Nawashukuru madaktari na watumishi wa JKCI kwa huduma nzuri, upendo na ukarimu walioutoa kwa mtoto wangu, kupitia kambi hii nimeweza kufahamu hali ya afya ya mtoto wangu na kupata mwongozo wa nini natakiwa kufanya”, alisema Magreth

Leo ni siku ya mwisho kwa timu ya wataalamu wa JKCI kutoa huduma za uchunguzi, elimu na matibabu ya moyo katika Tarafa ya Ngerengere ambapo timu hiyo inatarajiwa kuhamia katika Tarafa ya Mikese na kuendelea na huduma hizo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusogeza huduma za kibingwa na bobezi za matibabu ya moyo karibu na wananchi.



Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma