Jengeni tabia ya kupima afya za mioyo yenu mara kwa mara - Prof. Janabi
Wananchi wameshauriwa kujenga mazoea ya kupima afya zao mara kwa mara ili kufahamu kama wana magonjwa ya moyo au la na kama wanamatatizo wataweza kupata matiba mapema kabla ya tatizo kuwa kubwa na kama hawana itawasaidia kujikinga ili wasipate magonjwa hayo.
Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akizungumza na waandishi
wa habari katika maonesho ya 45 ya
Kimataifa ya Dar es Salaama (Sabasaba) yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Prof. Janabi alisema ni muhimu kwa wananchi kutumia maonesho
hayo kupima afya zao na kupata uelewa wa jinsi ya kujikinga na magonjwa mbalimbali
ikiwemo moyo, figo na saratani.
“Katika banda letu tunapima vipimo mbalimbali vya magonjwa ya
moyo vikiwemo vipimo vya kuangalia jinsi
moyo unavyofanya kazi (Echocardiography - ECHO) , umeme wa moyo unavyofanya
kazi (Electrocardiography – ECG) , vipimo vya damu na vipimo vya urefu na uzito
na kuangalia kiangalia kiwango cha sukari kwenye damu”,.
“Pia tunatoa elimu ya lishe ambayo itamsaidia mtu kufahamu ni
vyakula gani anatakiwa kula ili aweze kutunza mwili na moyo wake, nawakaribisha
wananchi mtembelee katika banda letu ili mpate huduma hizi”, alisema Prof.
Janabi.
Prof. Janabi ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema katiba banda hilo mwananchi akipimwa na kukutwa na tatizo la moyo au
sukari anapewa dawa bila malipo yoyote pia anapewa rufaa ya moja kwa moja ya
kwenda kutibiwa matibabu ya kibingwa katika Taasisi hiyo.
Kwa upande wa wananchi waliopata huduma ya kufanyiwa
uchunguzi wa magonjwa ya moyo na wataalamu wa Taasisi hiyo walishukuru kwa
huduma waliyoipata.
“Nimefika hapa sikuwa najua kama ninatatizo la ugonjwa wa
kisukari, nimepima na kupata msaada mkubwa wa vipimo na elimu wataalamu
wanakusikiliza kwa umakini , kama una swali unauliza wanakujibu”,.
“Nimepewa dawa za ugonjwa wa kisukari ambazo nitaenda
kuzitumia sijalipia fedha yeyote ile. Ninaiomba Serikali izidishe elimu kwa
wananchi ili wajue umuhimu wa kupima afya zao mara kwa mara kama mimi
nisingepima leo hii nisingefahamu kama ninatatizo la kisukari”, alishukuru
Salehe Abdala mkazi wa Ukonga jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce akimpima
mwananchi aliyetembea banda la Taasisi hiyo kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (Echocardiography - ECHO) wakati wa maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Dar es Salaama (Sabasaba)
yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara
ya Kilwa.
Comments
Post a Comment