Warembo wa Miss Tanzania wakabidhi maktaba ya watoto wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo na saratani
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.
Dkt. Doroth Gwajima akizungumza na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Fr’ederic
Clavier na mwanzilishi wa Taasisi ya Beauty Legacy Miss Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi
kabla ya kuzindua maktaba ya watoto wanaolazwa hospitali kwa muda mrefu wakati
wa uzinduzi wa maktaba hiyo uliofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) leo Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ameziomba sekta binafsi kuwekeza katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kujenga maktaba za watoto katika Hospitali na vituo vya Umma vya kulelea watoto ili kuwasaidia kujenga afya ya akili kwa kujisomea, na kuwajenga kisaikolojia wakati wakipatiwa matibabu ya muda mrefu.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua maktaba ya watoto wanaosumbuliwa na maradhi ya Moyo na saratani wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Dkt. Gwajima alisema yuko tayari kushirikiana na sekta binafsi ili sekta ya afya iweze kwenda mbele zaidi, jambo la muhimu ni kwa wadau hao kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizopo.
“Leo hii nimezindua maktaba ya watoto wanaotibiwa katika Hospitali za JKCI na MNH lakini kuna watoto wanatibiwa katika Hospitali ya Saratani Ocean Road na Hospitali tano za kanda ambazo ni Bugando, Mbeya, KCMC, Benjamini Mkapa na wengine wapo kwenye vituo vyetu vya malezi. Hivyo Hospitali na vituo hivi vina watoto ambao kutokana na maradhi yao hujikuta wanakaa hospitalini muda mrefu wakipata matibabu”,.
“Ninawaomba wadau wa sekta binafsi mjitokeze kujenga maktaba za watoto katika Hospitali hizi, kwani mtoto wakati anapata matibabu au akiwa anasubiri matibabu yake akipata vitabu vya kujisomea vitamfariji na kumjenga kisaikolojia kuwa ingawa anaumwa lakini anapata fursa ya kumpatia maarifa yaliyomp kwenye vitabu mbalimbali vya rika lake kama wanavyopata watoto wengine”, alisema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima aliwashukuru warembo waliowahi kushinda taji la Miss Tanzania miaka mbalimbali wakiongoza na Miss Tanzania wa mwaka 2000, Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi kwa moyo wao wa upendo na kuona umuhimu wa kujenga maktaba na kuweka vitabu ili kuwasaidia watoto waliolazwa Hospitalini muda mrefu kwa ajili ya matibabu.
“Ninawashukuru sana kwa huduma hii mliyoitoa kwa watoto wetu, pamoja na kushiriki katika mashindano ya urembo nyinyi pia ni kina mama mmeguswa na kuamua kuwasaidia wahitaji. Watoto hawa wakati wanapata matibabu wanakosa muda wa kwenda shule na hivyo kuwa nyuma kimasomo ukilinganisha na wenzao wanaokwenda shule muda wote lakini kwa vitabu hivi mlivyovitoa watapata muda wa kujisomea”, alishukuru Waziri Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake kiongozi wa warembo hao (Beauty legacy) Miss Tanzania mwaka 2000 Jacqueline Ntuyabaliwe alisema ndoto ya kujenga maktaba hiyo aliipata mwaka jana alipokuwa anatimiza miaka 20 tangu aliposhinda taji hilo kwa kushirikiana na wenzake wakaona ni vyema kutengeneza maktaba hiyo ili kuisaidia jamii.
Jacqueline alisema mamiss hao kila mtu anafanya kazi yake wakaona ni vyema waunganishe nguvu zao kwa pamoja ambapo mwaka jana waliandaa 'gala dinner' na kuchangisha fedha ambazo zimewasaidia kujenga maktaba hiyo pia wamekusanya vifaa vya watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza umri “njiti” ambavyo watavikabidhi hivi karibuni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Kuna watoto ambao wanakaa Hospitalini muda mrefu hawaendi shule tumenunua vitabu vya mitaala ambayo wanasoma shuleni, tunaamini vitabu hivi vitaleta faraja kwao. Maktaba iko wazi kwa yeyote ambaye ataona anavitabu alete kwa ajili ya watoto hawa ili waweze kujisomea”, alisema Jacqueline.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema Taasisi hiyo itaajiri mwalimu mmoja na mkutubi mmoja kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao waweze kusoma vitabu hivyo na kuvielewa.
Alisema kuwepo kwa vitabu hivyo ambavyo vitawafanya watoto wasome hadithi mbalimbali pamoja na masomo yao ya darasani ni sehemu ya tiba kwao ambayo itawajenga kisaikolojia na kuamini kuwa baada ya kupona watarudi shuleni na kuendelea na masomo yao kama kawaida.
Naye Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Fr’ederic Clavier ambaye Ubalozi wake umesaidia katika ujenzi wa maktaba hiyo alisema kuwepo kwa maktaba ya watoto katika Hospitali kunatoa faraja kwa familia na watoto ambao wako katika maumivu ya magonjwa ya moyo na saratani.
“Iwapo jamii nzima itaungana kwa pamoja sioni sababu ni kwa nini mtoto anakufa leo kwa magonjwa ya moyo na saratani, kuna haja ya kuungana kwa pamoja ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa haya katika familia kwa kufanya hivyo tutaokoa maisha ya watu na kutoa moyo kwa familia zenye watoto wagonjwa”, alisisitiza Balozi Clavier.
Mwishoni mwa mwaka jana warembo hao walitembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuwasilisha wazo lao la kujenga maktaba kwa ajili ya watoto wanaougua maradhi ya saratani, moyo pamoja na maradhi mengine yanayowafanya wakae Hospitali muda mrefu.
Jackqueline ana Taasisi ya Dkt.
Ntuyabaliwe ambayo aliianzisha kwa ajili ya kumbukumbu ya baba yake ambaye
alikuwa daktari wa kina mama katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia
Taasisi hiyo kazi yao ni kutengeneza maktaba na kugawa vitabu hapa nchini
wameshafanya kwa shule za Dar es salaam, Morogoro na Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.
Dkt. Doroth Gwajima akikata utepe kuashiria uzinduzi wa maktaba mpya ya watoto
wanaolazwa hospitali kwa muda mrefu iliyotengenezwa na Taasisi ya Beauty Legacy
pamoja na Ubalozi wa Ufaransa leo wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam
Baadhi ya watoto waliolazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya magonjwa ya moyo na wenzao kutoka
hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya Saratani
wakisoma vitabu katika maktaba mpya ya watoto wanaolazwa hospitali kwa muda
mrefu baada ya kuzinduliwa kwa maktaba hiyo iliyodhaminiwa na Ubalozi wa
Ufaransa pamoja na Taasisi ya Beauty Legacy leo Jijini Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment