Serikali yaombwa kutoa uelewa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ukiwemo ugonjwa wa moyo kwa wananchi
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane akimpa kitabu cha jinsi ya kuepukana na
magonjwa yasiyo ya kuambukiza mwananchi
aliyetembelea banda la taasisi hiyo kwa
ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 45 ya
Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyomalizika hivi karibuni katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Serikali imeombwa kutoa uelewa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo kupitia vyombo vya habari, makongamano na mikutano ya hadhara kwa kufanya hivyo watu wengi wataepukana na magonjwa hayo.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na baadhi ya
wananchi waliotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili
ya upimaji wa magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 45 ya kimataifa ya Dar es Salaam yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Wananchi hao walisema hivi sasa watu wengi
wanatembea bila ya kufahamu afya zao zikoje na mwisho wa siku wanakufa vifo vya
ghafla au kupata tatizo kubwa la kiafya na kusema kuwa wamerogwa kitu ambacho
siyo kweli.
Yusta Ngoruno mkazi wa Kimara alisema yeye
alifika katika banda hilo kwa ajili ya kupima afya anashukuru amefahamu afya
yake ya moyo ikoje na ushauri wa lishe alioupata wa jinsi ya kuepukana na
magonjwa hayo atautumia kuelimisha wengine.
“Mtaalamu kaniambia magonjwa ya moyo ni
magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kwa uelewa ambao mimi nimeipata leo hii kuhusu magonjwa haya
utanisaidia kuelimisha na wengine. Ninaiomba
Serikali kupitia wataalamu wake watoe
elimu hii kwa wananchi ili nao wawe na uelewa kama nilioupata mimi siku ya hii
ya leo”,.
“Nimepata ushauri wa jinsi ya kuandaa chakula
bora kwa familia yangu na aina gani ya vyakula ninavyotakiwa kula ili niepukane
na magonjwa ya moyo, ushauri huu nitaufanyia kazi pia nitawafundisha wanawake
wenzangu katika vikundi vyetu vya maendeleo”, alisema Yusta.
Naye Mzee Ali Hamisi mkazi wa Hale mkoani
Tanga alisema baada ya kutembelea maonesho hayo akaona atembelee banda la JKCI
na kupima magonjwa ya moyo kwani hajawahi kufanya hivyo katika maisha yake.
“Nimefika katika banda hili nimepokelewa
vizuri na wauguzi wamenipima vipimo mbalimbali na kunipa ushauri nikaenda
kuonana na daktari. Kwa namna ya kipekee ninawashukuru wauguzi hawa kwani mara nyingi huwa hatuwashukuru lakini hata
ukiwa Hospitali muuguzi ndiye mtu anayekaa muda mrefu na mgonjwa na kumpatia huduma
tofauti na daktari ambaye anakaa na mgonjwa muda mfupi”, .
“Baada ya kupima nimekutwa na tatizo la
shinikizo la juu la damu kabla ya hapo sikuwa nafahamu kuwa ninaugonjwa huo, nimepewa
dawa ambazo nitaenda kuzitumia ninashukuru. Ombi langu kwa Serikali ni elimu ya
magonjwa haya itolewe kwa wananchi kwa njia ya vyombo vya habari hii itawasaidia
kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara”, alisema Mzee Hamisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Magonjwa ya
Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Tatizo Waane ambaye alikuwa
katika banda hilo kwa ajili ya kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi alisema
taasisi hiyo imekuwa ikitoa huduma za ushauri, upimaji na kutibu magonjwa ya
moyo mara kwa mara kwa wananchi.
“Huduma hii ya upimaji huwa ni endelevu kwani
tunaitoa wakati wa maadhimisho na maonesho mbalimbali ikiwemo siku ya shinikizo
la juu la damu Duniani, siku ya shinikizo la juu la damu Duniani, siku ya
wanawake Duniani na katika mikutano mbalimbali
ambayo Taasisi inaalikwa kwenda kutoa huduma hizo”, alisema Dkt. Waane ambaye
pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo.
Taasisi hiyo katika maonesho hayo ilitoa huduma
mbalimbali za ushauri na upimaji wa magonjwa ya moyo ikiwa ni pamoja na vipimo
vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO), mfumo wa
umeme wa moyo (Electrocardiography - ECG), urefu, uzito, kiwango cha sukari
mwilini, shinikizo la damu na vipimo vya
damu ili kuangalia utendaji kazi wa ini, figo, homa ya ini, kundi la damu na
full blood picture.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Fredy Tupa akimpima shinikizo la damu (BP) mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyomalizika hivi karibuni katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Wananchi wakipata huduma za ushauri na upimaji wa viashiria vya magonjwa ya moyo katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyomalizika hivi karibuni katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Martha Mbona akimpima kiwango cha sukari mwilini mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyomalizika hivi karibuni katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji akitoa ushauri wa lishe kwa wananchi waliotembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyomalizika hivi karibuni katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Comments
Post a Comment