Wahudumu wa afya nchini watakiwa kuwa wakarimu wakati wanawahudumia wateja na wagonjwa katika vituo vyao vya kazi – Dkt. Gwajima
Wahudumu wa afya nchini wametakiwa kuwa wakarimu wakati
wanapowahudumia wateja na wagonjwa kwani kufanya hivyo wataongeza idadi ya watumiaji wa
huduma watakaokwenda kutibiwa katika vituo vyao na kuvutiwa wajiunge na bima za
afya na hivyo kuongeza mapato ya vituo husika na kupitia kuvutia wateja wa
kimataifa watainua uchumi wa nchi kwa ujumla wake.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam
na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth
Gwajima wakati akizindua timu ya kuratibu hatua za Tanzania kuelekea kwenye utalii wa tiba katika ukumbi wa mikutano
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Waziri Dkt. Gwajima alisema asili ya binadamu
yeyote yule anahitaji kujaliwa, kuthaminiwa na kutambuliwa kama wahudumu hao wa afya
wakifanya hivyo watapiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa.
“Hospitali zetu zina majengo mazuri, zina
wataalamu wa kutosha na vifaa tiba vya kisasa vya kutosha kitu kinachokosekana ni ukarimu kwa wagonjwa,
ili tuingie katika utalii wa matibabu kwa
kila hospitali tunatakiwa kuwe na mabadiliko katika utendaji wa kazi ili mgonjwa achaguwe kwenda kutibiwa katika Hospitali yako”,.
“Imefika wakati sasa kwa hospitali kufungua kitabu cha utoaji huduma kwa mteja ili kila
mfanyakazi anayelalamikiwa kwa kutoa huduma mbaya na anayesifiwa kwa kutoa
huduma nzuri jina lake liandikwe humo, yule atakayelalamikiwa mara nyingi aweze
kuchukuliwa hatua na yule ambaye jina lake litaongoza kwa kutoa huduma nzuri
apongezwe”, alisema Dkt. Gwajima.
Waziri huyo wa Afya alisema utalii tiba siyo ngeni hapa nchini na tayari umeanza
kufanyika, katika utalii huu mgonjwa anachagua hospitali ambayo inatoa huduma bora na nzuri na kwenda kutibiwa huko.
Utalii huu unafanyika kwa watanzania
wenyewe na kwa wagonjwa wanaotoka nje ya nchi na kuja kutibiwa hapa nchini kwa kufanya hivyo
nchi inaongeza mapato pia tunaimarisha undugu kati ya nchi na nchi.
Dkt. Gwajima pia aliipongeza timu hiyo ya
kuratibu hatua za Tanzania kuelekea katika utalii wa tiba na kusema
inawataalamu wa kada mbalimbali wakiwemo kutoka sekta binafsi na kuwaagiza katika
utekelezaji wa utalii tiba wasiziache Hospitali binafsi kwani nazo zina majengo
mazuri, wataalamu wa kutosha na vifaa vya kisasa jambo la muhimu ni kushirikiana kwa
pamoja ili kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya utalii tiba kama zilivyo nchi zingine Duniani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo
Prof. Mohamed Janabi alisema kamati hiyo imependekeza utalii huo uanze
kufanyika katika tiba ya moyo inatolewa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI), matibabu ya figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), tiba ya
upasuaji wa ubongo inayotolewa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na matibabu ya
mionzi ya saratani yanayotolewa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road na
baadaye ufanyike katika hospitali za kanda, mikoa na wilaya.
Prof. Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi
Mtendaji wa JKCI alisema katika utalii tiba kuna watalii wa aina tatu ambapo kuna wagonjwa
wanakuja kutibiwa nchini kutoka nje ya nchi na baada ya kupona wanarudi nchini
kwao, kuna wagonjwa watakuja kutibiwa na baada ya kupona watakwenda kutalii
katika vivutio mbalimbali vya utalii na kuna watalii ambao wanakuja kutalii
nchini ambao wakipata matatizo ya kiafya watapata huduma za matibabu hapa
nchini.
“Jambo
la muhimu ni kuangalia ni jinsi gani Hospitali zetu zitatoa huduma ambazo
zitawavutia watanzania pamoja na nchi mbalimbali za Afrika kutibiwa hapa nchini
na siyo kwenda kutibiwa mahali pengine kwani tuna wataalamu wa kutosha, vifaa tiba vya kisasa na majengo mazuri”, alisema Prof.
Janabi.
Naye Abdulmalik Mollel ambaye ni mjumbe wa timu hiyo na mwanzilishi
na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya utalii tiba ya GEL alisema hapa nchini kuna huduma nzuri
za matibabu lakini kitu kinachokosekana ni lugha zinazotolewa kwa wagonjwa na
wahudumu wa afya pamoja na namna ya utoaji wa huduma husika.
Alitoa mfano wa raia wengi wa visiwa vya
Comoro wanavyotegemea kupata huduma za matibabu hapa nchini lakini changamoto kubwa
wanayokutana nayo ni lugha wao wanazungumza lugha ya Kifaransa na Tanzania
lugha zinazotumika ni za Kiswahili na Kiingereza.
“Umbali kutoka uwanja wa ndege hadi zilipo
Hospitali zetu za Taifa ambazo ni
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Taasisi ya Saratani Ocean Road ni
kilomita kama 10, Hospitali tatu kati ya hizi
zipo katika eneo moja mahali ambapo mtu anatembea kwa miguu kutoka
hospitali moja hadi nyingine”,.
“Mahali ilipo Taasisi ya Saratani Ocean Road
siyo mbali na zilipo hospitali hizi zingine, hii ni tofauti na nchi zingine ambako umbali
wa kutoka uwanja wa ndege hadi hospitali ni mrefu pia ilipo hospitali moja na
nyingine ni mbali. Tatizo lililopo hapa kwetu ninamfahamu nani ili niende
kupata huduma nzuri za matibabu lakini kama tutaamua kubadilika utalii wa
matibabu unawezekana kabisa kufanyika”, .
Katikati ya mwezi wa sita mwaka huu Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan wakati akizindua mtambo wa Cathlab uliopo katika Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alisema ni
wakati sasa umefika kwa Tanzania kuwa nchi ya utalii tiba kwani vifaa tiba vya kisasa vipo, wataalamu
wapo pamoja na hospitali nzuri zipo.
Timu ya kuratibu hatua za Tanzania
kuelekea kwenye utalii tiba inawajumbe 13
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Saratani Ocean Road, Bodi
ya Utalii na sekta binafsi.
Mwenyekiti
wa timu ya kuratibu hatua za Tanzania kuelekea kwenye Utalii tiba ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akielezea namna ambavyo
kamati yake imejipanga wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo uliofanywa na Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima leo
katika Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.
Katibu
wa timu ya kuratibu hatua za Tanzania kuelekea kwenye Utalii tiba Peruzy Roche akiwasilisha mpango
kazi utakaofanywa na kamati hiyo kuiweka Tanzania katika hadhi ya utalii tiba wakati wa uzinduzi wa timu hiyo uliofanywa na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima
katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo Jijini Dar es Salaam.
Mjumbe
wa timu ya kuratibu hatua za Tanzania kuelekea kwenye Utalii tiba Joseph Kahama akitoa neno la
shukrani mara baada ya kuzinduliwa kwa kamati ya utalii tiba uliofanywa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima katika ukumbi wa mikutano wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo Jijini Dar es Salaam
Comments
Post a Comment