Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete yapongezwa kwa kuanzisha duka la kuuza dawa za magonjwa mbalimbali ya binadamu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuanzisha duka la dawa linalouza dawa za kutibu magonjwa mbalimbali na kuzitaka Hospitali zingine kuiga mfano huo.
Waziri Dkt. Gwajima amezitoa pongezi hizo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua
maktaba ya watoto wanaosumbuliwa na maradhi ya Moyo na saratani wanaotibiwa katika
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Dkt. Gwajima alisema kuwepo kwa duka hilo la dawa kutawasaidia
wagonjwa wanaotibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Mifupa
Muhimbili (MOI) badala ya kwenda kununua dawa nje ya Muhimbili watakwenda
kuzinunua katika duka hilo.
“Kuna dawa ambazo hazipatikani ndani ya Hospitali , mgonjwa
akiandikiwa dawa hizi na daktari analazimika kwenda kuzinunua nje ya Muhimbili .
Kuwepo kwa duka hili kutawasaidia wagonjwa kupata dawa hizi ndani ya Muhimbili
na kuweza kuokoa muda wa kutembea kwenda
kutafuta dawa”, alisisitiza Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima pia aliipongeza compounding Unit ambao wanatengeneza
dawa za watoto za moyo kutoka kidonge cha mtu mzima hadi kuwa kwenye matumizi
ya watoto na kutengeneza vitakasa mikono “sanitizer” ambazo zinatumika katika
Taasisi hiyo na zingine zinauzwa katika duka hilo la dawa.
“Hospitali zingine ziige mfano wa JKCI kwani kuwepo kwa duka la
dawa ambalo mtu ananunua kwa kulipia na compounding unit ambao wanazalisha dawa
na pamoja na vitakasa mikono kutasaidia Hospitali kuongeza kipato pamoja na
kurahisisha upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa”, alisisitiza Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi
alisema kabla ya kuanzishwa kwa duka hilo waliangalia ni aina gani za dawa
ambazo hazipatikani MNH, JKCI na MOI na kuziweka katika duka hilo ili
kuwarahisishia wagonjwa pamoja na watu wengie kupata dawa hizo kirahisi.
“Dawa hizi pamoja na bidhaa zingine ambazo zinatakiwa kuuzwa
katika duka la dawa zinauzwa kwa kulipia, mtu yeyote anafika katika duka hili
na kununua dawa anazozitaka. Kuna dawa ambazo unanunua moja kwa moja bila ya
kuandikiwa na daktari na kuna dawa ambazo unaandikiwa na daktari”, alisema Dkt.
Janabi.
Akizungumzia kuhusu Compounding Unit Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi
katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Delila Kimambo alisema imewasaidia katika upatikanaji wa dawa za
moyo za watoto kwani dawa hizo hazipatikani kwenye soko la dawa nchini kutokana
na dawa hizo kutozalishwa viwandani.
Dkt. Delila ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema duka hilo la dawa limeanza kufanya kazi mwanzoni mwa mwezi Juni na linahudumia zaidi ya watu 100 kwa siku.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Doroth Gwajima akisoma fomu ya mgonjwa aliyetembelea duka la dawa lililoanzishwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya kuuza dawa za magonjwa yote kwa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika Hospitali Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) pamoja na watu wengine watakaohitaji huduma hiyo.
Comments
Post a Comment