Wafanyakazi wa Benki ya Exim Idara ya Fedha wachangia gharama za matibabu ya mtoto mwenye matatizo ya moyo
Mkuu
wa Idara ya Fedha kutoka Benki ya Exim
Issa Hamisi akimkabidhi Mhasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Mohamed Isimbula kiasi cha Tshs. 3,000,000/= fedha zilizochangwa na baadhi ya wafanyakazi wa Benki hiyo Idara ya Fedha kwa ajili ya kulipia gharama za
upasuaji wa moyo kwa mtoto aliyezaliwa na tatizo la tundu kwenye moyo.
Taasisi
zinazotegemea watu ili ziweze kujiendesha zimeombwa kuisaidia jamii yenye
uhitaji wa matibabu ya magonjwa mbalimbali ili iweze kuwa salama na yenye afya
bora kwani jamii iliyo salama itaendelea kuwa sehemu ya Taasisi hizo na
kuzifanya ziweze kufikia malengo ya kazi waliyojipangia.
Rai
hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mhasibu wa Benki ya Exim Beatus Temba alipokuwa akizungumza na
uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wafanyakazi wa benki
hiyo kutoka Idara ya Fedha walipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuchangia
gharama za upasuaji wa moyo kwa mtoto aliyezaliwa na matatizo ya moyo.
Temba
alisema kupitia Redio Clouds kipindi cha Njia panda alipata taarifa za mtoto
aliyezaliwa na tundu kwenye moyo ambaye familia yake ilikosa fedha za kumlipia gharama za matibabu akawashirikisha wafanyakazi wenzake ili waweze kuokoa maisha
ya mtoto huyo.
“Baada
ya kuwashirikisha wafanyakazi wenzangu ofisini walilipokea wazo langu ndipo
tukaamua kuchangishana fedha za matibabu ya mtoto huyo ili aweze kupata
matibabu na kuwa na maisha ya furaha kama watoto wengine”,.
“Bila
Jamii Taasisi zetu haziwezi kujiendesha inatupasa kuhakikisha kuwa jamii yetu
ipo salama na yenye afya bora, nawashukuru wafanyakazi wenzangu kutoka Idara ya
Fedha ambao kwa pamoja tumeweza kukusanya kiasi cha Tshs. 3,400,000/= fedha
ambazo zitatumika katika matibabu ya mtoto huyu”, alisema Temba.
Aidha
Temba aliipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma za matibabu
ya moyo inazozitoa kwa wagonjwa na kuishukuru kwa kupokea mchango wao walioutoa
ambao utasaidia kuokoa maisha ya mtoto huyo.
“Kiasi
cha fedha tuliyokusanya ni Tsh. 3,400,000/= fedha ambazo tumeikabidhi JKCI ni shilingi
3,000,000/= ikiwa ni gharama za upasuaji wa moyo pamoja na gharama nyingine za
matibabu na kiasi cha shilingi 400,000/= tumemkabidhi mama wa mtoto kwa ajili
ya matumizi ya chakula na mahitaji mengine atakayotumia kabla na baada ya
upasuaji.
Kwa
upande wake Msimamizi wa Wodi ya Watoto
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Theresia Marombe aliwashukuru
wafanyakazi wa Benki ya Exim kwa moyo wao wa upendo wa kumsaidia mtoto huyo gharama za matibabu na
lishe kwani ni kitu cha kipekee watu kusaidia gharama za matibabu na kukumbuka
upande wa lishe.
“Watoto
wetu wengi tumekuwa tukiwapokea wakiwa na lishe duni, hivyo kuchukuwa muda
mrefu wodini kuwahudumia ili kuhakikisha wanafikia uzito ambao utawawezesha
kwenda kufanyiwa upasuaji lakini nyie mmekuja mkiwa mmefikiria kusaidia katika
upande wa matibabu na lishe”, alisema Theresia.
Theresia
aliwaahidi wafanyakazi hao wa Banki ya Exim kuwa JKCI itaendelea kuwapa taarifa
zote za matibabu ya mtoto huyo hatua kwa hatua hadi pale matibabu yake
yatakapokamilika na kuwaomba kwenda kumuona mtoto huyo mara atakapofanyiwa
upasuaji.
Comments
Post a Comment