Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete yatoa elimu ya chanjo kwa wafanyakazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB)
Na: JKCI
Serikali
imeandaa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa
wa UVIKO – 19 kwa kuwafuata wananchi wanaohitaji huduma ya chanjo mahali walipo
ili kuongeza kasi na kuwapa wananchi nafasi ya kuchanja.
Hayo
yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume wakati wataalam wa afya kutoka
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walipoalikwa na uongozi wa Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya kutoa elimu ya umuhimu wa
chanjo pamoja na kutoa chanjo ya UVIKO - 19 kwa wafanyakazi wa benki hiyo jana
Jijini Dar es Salaam.
Dkt.
Mfaume alisema kitendo kilichofanywa na JKCI kwa kushirikiana na TADB ni
maelekezo ya Serikali kwamba lazima sasa wataalam wa afya watoke na kuwafuata
wananchi wenye uhitaji wa chanjo ya UVIKO – 19 pale walipo.
“Tunawapongeza
sana uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa kuratibu utapikanaji
wa chanjo kwa wafanyakazi, sio benki zote ambazo zinaweza kuratibu upatikanaji
wa chanjo eneo la kazi, hii inaonesha utofauti wa benki hii na benki nyingine”,
“Wafanyakazi
hawawezi wakafanya kazi wasipokuwa na afya njema, maamuzi mliyoyafanya ya
kupata chanjo kwa namna moja ama nyingine mtakuwa mnatekeleza sera zenu”,
alisema Dkt. Mfaume.
Akitoa
elimu ya umuhimu wa chanjo ya UVIKO – 19 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema mtu anapopata chanjo
anakua kwenye nafasi ndogo ya kupata changamoto kubwa za kiafya pale
atakapopata ugonjwa wa UVIKO – 19.
“Watu
wengi waliopata ugonjwa wa UVIKO – 19 asilimia 85 walipata maradhi madogo
madogo kama vile kuumwa kichwa, mafua na homa za hapa na pale, asilimia 10
walifikia hatua za kupata huduma za hospitali kama vile kulazwa na kadhalika,
lakini asilimia 5 walifikia hatua za kutumia msaada wa mashine kupumua”,
“Kama
leo wote tutachanja ni matumaini yangu hata ikitokea tukapata ugonjwa huu
tutaishia kwenye ile asilimia 85 ya kusumbuliwa na maradhi madogo madogo”,
alisema Dkt. Waane
Aidha
Dkt. Waana amewataka wafanyakazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania
kuendelea kuchukua taadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO – 19 kwa kuendelea kunawa
mikono yao kwa maji safi na tiririka, kutumia vitakasa mikono, kuepuka
misongamano pamoja na kuvaa barakoa.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Frank
Nyabundege alisema menejimenti ya Benki
yake imeona ni vyema kuwapa nafasi wafanyakazi wa benki hiyo ili waweze kupata elimu
juu ya ugonjwa wa UVIKO – 19 pamoja na chanjo, kwani kupitia elimu sahihi
waliyoipata wengi wao watabadili mawazo potofu waliyokuwa nayo.
“Sisi
kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania tumeona kwasababu tuna wadau
mbalimbali na tunajihusisha na wakulima wa nchi nzima tusipokuwa mfano kwa
wadau wetu uchumi wa nchi yetu unaweza ukatetereka maana watu ambao ni
wazalishaji katika mashamba kwa ajili ya kuinua uchumi wetu utuchukulia sisi kama
mfano katika maisha yao”,
“Ninaamini
baada ya kupata elimu hii ya kisayansi kutoka kwa daktari bingwa wa JKCI Tatizo
Waane juu ya chanjo ya UVIKO – 19 hata wale tuliokuwa na mashaka leo tutachukua
hatua ya kuchanja, mimi leo nitakuwa mfano hapa kwa kuchanja”, alisema
Nyabundege.
Comments
Post a Comment