CRDB Marathon yachangia milioni 250,000,000 matibabu ya moyo kwa watoto


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango akimkabidhi kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo hundi ya shilingi milioni 250 iliyotolewa leo katika Viwanja vya Farasi Oyster bay Jijini Dar es Salaam na Benki ya CRDB fedha zilizokusanywa kutoka kwa washiriki wa mbio za CRDB Marathon kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto 125 wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwaongoza viongozi wengine katika matembezi ya kilometa 5 wakati wa mbio za CRDB Marathon kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI na wanawake wenye ujauzito hatarishi wanaotibiwa CCBRT leo Jijini Dar es Salaam


Washiriki wa mbio za CRDB Marathon wakishiriki mazoezi ya viungo mara baada ya kumalizika kwa mbio hizo zilizofanyika katika Viwanja vya Farasi Oyster bay leo Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuchangia watoto 125 wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)


Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Mkumbo akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyeshiriki mbio za CRDB Marathon kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI leo katika Viwanja vya Oyster bay Jijini Dar es Salaam



 Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji akimwelezea lishe bora na mfumo bora wa maisha mwananchi aliyeshiriki mbio za CRDB Marathon kwa ajili ya kuchangia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI leo katika viwanja vya Farasi vilivyopo Jijini Dar es Salaam

Picha na: Othman Michuzi na Khamis Mussa

********************************************************************************************

Na: Genofeva Matemu

Shilingi Milioni 250,000,000 zimetolewa na Benki ya CRDB kupitia mbio za CRDB Marathon msimu wa tatu kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.

Akikabidhi hundi ya fedha hizo leo katika viwanja vya Farasi vilivyopo Oyster bay Jijini Dar es Salaam Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alisema kuwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ina uwezo wa kuwafanyia upasuaji mkubwa na mdogo wa moyo watoto 250 hadi 300 kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 10 yamahitaji yote ya nchi kwa mwaka

Mhe. Dkt. Mpango alisema kuwa gharama za upasuaji wa moyo kwa mtoto mmoja ni kati ya shilingi milioni mbili hadi milioni kumi na moja ikitegemea na ukubwa wa tatizo hivyo kuishukuru Banki ya CRDB kuona umuhimu wa kusaidia matibabu ya watoto wenye uhitaji wa kufanyiwa upasuaji wa moyo.

“Kwa takwimu zilizopo mpaka kufikia mwezi juni mwaka huu Taasisi ya Moyo ina wagonjwa wa moyo takribani 750 ambao walihitaji kufanyiwa upasuaji mkubwa na mdogo wa moyo kwa hiyo hii inadhihirisha ni kwa kiasi gani fedha hizi mnazochangia kupitia CRDB Marathon zinaenda kupunguza changamoto ya huduma ya matibabu katika jamii yetu”, alisema Mhe. Dkt. Mpango

“Nimefurahishwa kuona watanzania wengi pamoja na wananchi kutoka nchi jirani wakijitokeza kuchangia watoto wetu ili waweze kupata huduma ya upasuaji wa moyo kupitia ushiriki wenu kwenye mbio za CRDB Marathon, nawaomba muendelee kuwa na moyo ya kujitoa kama huu kwa ajili ya kurejesha tamasamu kwa wale ambao wanakutana na changamoto za kiafya” Mhe. Dkt. Mpango

Aidha Mhe. Dkt. Mpango alisema kuwa uamuzi wa CRDB Bank kutumia marathon ya mwaka huu kuchangisha fedha kwa ajili ya akina mama wenye ujauzito hatarishi ni sehemu ya kurejesha matumaini kwa akina mama ili waweze kupata huduma stahiki katika hospitali ya CCBRT.

“Michango yenu itaokoa maisha ya akina mama na watoto wengi, kwani mbio hizi zinatupa nafasi kama serikali kushirikiana na wadau kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa huduma za jamii”,

“Maendeleo ya nchi yanahitaji nguvu kazi yenye afya njema, lakini watanzania wengi hasa sisi tunaoishi mijini tunakabiliwa na uzito uliozidi na inasikitisha kuona vijana wengi wanapoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari na shinikizo la damu magonjwa ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na mtindo wa maisha, ulaji usiofaa, na kutokufanya mazoezi ya mara kwa mara”, alisema Mhe. Dkt. Mpango

Mhe. Dkt. Mpango alisema kuwa kupitia mbio za CRDB Marathon CRDB wamekuwa sehemu ya kuelimisha watanzania juu ya kutunza afya kupitia mbio hizo, kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi kuwa wa kudumu kwa kila mmoja ili kujiepushe na maradhi lakini pia kupunguza mzigo wa gharama za matibabu ya magonjwa yanayoweza kuepukika kwa kufanya mazoezi mara kwa mara.

“Hata baada ya leo muendelee kuwahimiza watanzania kuishi maisha yanayofuata misingi ya afya bora, kuendelea kufanya mazoezi, pamoja na kuwa na bima za afya ili kurahishisha upatikanaji wa huduma za matibabu wakati tunapofikwa na changamoto za kiafya”, alisema Mhe. Dkt. Mpango

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema kuwa moja ya malengo iliyojiwekea CRDB wakati inandaa mbio hizo za msimu wa tatu ilikua ni pamoja na kufanikisha huduma za matibabu ya moyo kwa watoto 125 kwa kuchangia kiasi cha shilingi milioni 250,000,000 jambo ambalo limefanikiwa kwa asilimia 100.

“Kipekee kabisa nawashukuru wote walioungana nasi katika mbio za CRDB Marathon msimu wa tatu kwa ajili ya kufanikisha lengo hili, kujitokeza kwenu kwa wingi kumeonesha dhamira ya kuwa watanzania tuna upendo wa dhati kwa ndugu zetu hawa ambao wanahitiji huduma za matibabu”,

“Tunafahamu kwenye mbio hizi wamekuja washiriki zaidi ya 6,000 kutoka Tanzania pamoja na majirani zetu Kenya, huu ni upendo usiopimika kuona hata majirani zetu wanashirikiana nasi kuchangia huduma za matibabu kwa watoto na wanawake, tunawashukuru sana”, alisema Nsekela

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya bima ya maisha ya Sanlam Julius Magabe alisema kuwa Sanlam imekuwa washirika wakuu katika mbio za CRDB Marathon kwasababu sera yeo ya huduma za jamii inaamini katika kurudisha katika jamii yenye uhitaji.

“Tunaipongeza CRDB Bank kwa kutuongoza katika taratibu hizi za kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, naipongeza pia taasisi hii kwa juhudi zao za kuokoa maisha ya watoto”, alisema Magabe

 


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Maabara ya JKCI yapata ithibati ya kimataifa (ISO 15189:2012)