Waziri Ummy: Tafuteni eneo kubwa la matibabu ya moyo
Daktari wa wagonjwa waliolazwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Iddi Makapu akiwaeleza wajumbe wa bodi ya wadhamini ya Taasisi hiyo huduma zinazotolewa katika chumba hicho walipotembelea ICU kabla ya uzinduzi wa bodi hiyo uliofanyika leo katika Ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo.
Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu akizungumza na wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipofika katika taasisi hiyo leo jijini Dar ea Salaam kwaajili ya kuzindua Bodi ya Wadhamini ya JKCI.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwaeleza wajumbe wa bodi ya wadhamini ya Taasisi hiyo huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa kwa watoto wanaolazwa katika Taasisi hiyo wakati wajumbe hao walitembelea wodi ya watoto ya JKCI.
Picha na Khamisi Mussa
*******************************************************************************************************************************************
Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu ameiagiza Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutafuta eneo kubwa litakalotosha kuwaruhusu wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji kupata mazingira rafiki ya kufanyia mazoezi baada ya matibabu.
Waziri amependekeza eneo hilo litafutwe ndani ya eneo la Hospitali
ya Mlonganzila kwa kuwa mahali ilipo Taasisi hiyo pamejaa kwa sasa.
Mhe. Ummy Mwalimu alitoa mapendekezo hayo leo alipozindua bodi ya
wadhamini ya JKCI katika ukumbi wake wa mikutano jijini Dar es Salaam.
Mhe. Ummy alisema mahali ilipo JKCI kwasasa si rafiki kwa wagonjwa
kwani pamezungukwa na majengo mengi hivyo kubakiwa na nafasi finyu inayowanyima
wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo uhuru wa kufanya mazoezi.
Wajumbe hao pia wamepewa jukumu la kuhakikisha wataalamu mabingwa
wa magonjwa ya moyo kutoka JKCI wanawajengea uwezo na kuwasimamia wataalam wa
afya kutoka hospitali za kanda na wilaya kwa kuanza na hospitali ya kanda ya
Chato, hospitali ya rufaa ya kanda ya Mtwara na hospitali ya kanda ya mwalimu
Nyerere Memorial Hospital iliyopo mkoani
Mara.
“Wagonjwa wengi wamekuwa wakifuata huduma hasa za vipimo JKCI
lakini kama wataalam waliopo katika hospitali za kanda na rufaa watajengewa
uwezo wa kutoa huduma hizi itapunguza
msongamano wa wagonjwa wanaofika hapa kwaajili ya matibabu”, alisema Mhe. Ummy.
Mhe. Ummy alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya
kuambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo ambapo takwimu zinaonesha wagonjwa wa nje
na wale wanaolazwa inaongezeka hii ni kwa sababu ya kuboresha huduma za
matibabu hapa nchini hivyo kuwawezesha
wananchi kufika katika vituo vya afya kupata huduma lakini pia ongezeko hili
linaweza kusababishwa na ukosefu wa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa
hayo.
“Moja ya jukumu la Bodi hii mpya kwa kushirikiana na menejimenti
ya Taasisi hii ni kuhakikisha mnaandaa mpango mkakati wa kuweza kuwafikia
watanzania wengi zaidi ili waweze kupata elimu ya namna ya kujikinga na
magonjwa haya yasiyoambukiza kwani mtu anaweza kuyaepuka kama atafuata mtindo
bora wa maisha na hivyo kupunguza ongezeko la wagonjwa ya moyo”,.
“Bodi hii pia iandae mpango mkakati ambao utawawezesha wataalam
mabingwa wa magonjwa ya moyo kuwafikia
watanzania wengi kupitia upimaji wa kuwafuata wananchi mahali walipo (outreach
program) kwa kufanya hivi kutasaidia wagonjwa kugundulika mapema na hivyo kupata matibabu kwa wakati kuliko
kusubiri hadi tatizo limekuwa kubwa”, alisema Mhe. Ummy.
Aidha Waziri huyo wa Afya aliwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa
bodi mpya ambao wamekubali kupokea uamuzi wake wa kuwateua kwani wangeweza
kusema hapana kutokana na majukumu waliyonayo lakini wakaona umuhimu wa Taasisi
hiyo na kukubali imani ambayo amewapa kuwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini.
“Naishukuru Bodi
ambayo imemaliza muda wake kwa kufanya kazi kubwa na nzuri ambayo tumeona
matokeo ya kazi iliyofanyika katika utoaji wa huduma za afya kwa watanzania
wanaohitaji huduma za matibabu ya moyo. Ninaamini Bodi hii mpya nayo itakuwa
mstari wa mbele kuiwezesha taasisi hii kutekeleza majukumu yake kikamilifu
hivyo kufikia malengo ya kuanzishwa kwake”, alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy alisema kwakuwa JKCI imeweza kupunguza rufaa za kuwapeleka wagonjwa nje ya
nchi sasa ni wakati wa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Bodi mpya ya wadhamini
kuona namna ambavyo fedha iliyokuwa imetengwa kwaajili ya kupeleka wagonjwa nje
ya nchi inaombwa Hazina ili fedha hizo ziweze kuwasaidia wagonjwa ambao hawana
uwezo wa kugharamia matibabu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif
Shakalaghe aliwapongeza wafanyakazi wa JKCI kwa kazi nzuri wanayoifanya tangu
kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2016 hadi sasa bila kuisahau bodi ambayo
imemaliza muda wake kwani matokeo mazuri ya JKCI ni kwasababu ya ushirikiano
mzuri uliofanywa na Bodi hiyo.
“Nawapongeza wataalam wa JKCI kwasababu mafanikio haya yaliyosemwa
hapa ya kuokoa maisha ya wagonjwa bila ya watendaji hawa nadhani yasingekuwepo,
mmekuwa chachu na mfano mzuri katika jamii yetu”,.
“Majukumu makubwa ya JKCI ni pamoja na kutoa elimu, utafiti na
matibabu ya moyo ambapo leo hii tumeona matokeo makubwa katika sehemu ya
matibabu hili halipingiki lakini eneo la elimu na utafiti tungependa kuona
matokeo zaidi hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa ambayo tumeona kila mwaka
inaongezeka”, alisema Dkt. Shakalaghe.
Akisoma taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo Mkurugenzi
Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi alisema tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo
mwaka 2016 hadi sasa aina 30 za upasuaji
wa moyo zinafanyika hivyo kupunguza wagonjwa wanaokwenda nje ya nchi
kwaajili ya matibabu ya moyo.
“Taasisi imekuwa na mafanikio makubwa kwani tumeweza kuokoa kiasi
cha shilingi bilioni 51 baada ya kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi
kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya moyo”, alisema Prof. Janabi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini
ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof.William Mahalu aliwashukuru
wajumbe wa Bodi ya awali kwa ushirikikano mkubwa waliouonyesha hivyo kufanya
kazi ya uendeshaji wa Bodi hiyo kuwa nyepesi.
Prof. Mahalu ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na
mishipa ya damu alisema moja ya mikakati waliyojiwekea na Bodi iliyomaliza muda
wake ilikuwa ni kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi
kutibiwa magonjwa ya moyo ambapo lengo hilo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Leo hii tunajivunia kuwa sehemu ya kupunguza wagonjwa kwenda nje
ya nchi kwa ajili ya matibabu ya moyo, kama tulivyosikia idadi ya wagonjwa
wanaokwenda nje ya nchi imepungua na kufikia asilimia tano (5) ninaamini miaka michache ijayo hakutakuwa na
wagonjwa watakaokwenda kutibiwa magonjwa haya nje ya nchi”, alisema Prof.
Mahalu.
Comments
Post a Comment